Tuesday, January 5, 2010

UJAMBAZI WAITIKISA SONGEA

MATUKIO YA UJAMBAZI YANAANZA KUPIGA HODI NCHINI
Kundi la watu wanaodhaniwa kuwa Majambazi wamewavamia askari Polisi wawili na kuwapora Bunduki mbili aina ya SMG na risasi 60 alfajiri ya leo katika Mtaa wa MPATE uliopo katikati ya Mji wa SONGEA Mkoani RUVUMA.

Kufuatia tukio hilo hali ya taharuki imetanda katika Mji wa SONGEA na tayari Jeshi la Polisi limetangaza kutoa zawadi ya shilingi milioni 5 kwa mtu yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa watu hao

Askari walioporwa silaha ni PC GWAMAKA JOEL ambaye katika Purukushani hizo amepigwa risasi moja mguuni na PC Rajab ambaye amepigwa na kitu kizito kichwani hali iliyosababisha apoteze fahamu na amelazwa katika chumba cha wagonjwa Mahututi cha Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma kutokana na hali yake kuwa mbaya

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa RUVUMA MICHAEL KAMUHANDA amesema, askari hao wamevamiwa na kundi la watu wasiojulikana idadi majira ya saa kumi na moja na nusu alfajiri wakati wakitoka katika Lindo.

Aidha Kamanda Kamuhanda amesema Polisi wameimarisha Msako katika maeneo mbalimbali yakiwemo maeneo ya Mipakani mwa Mkoa wa RUVUMA na ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano katika kuzisaka bunduki hizo ili zipatikane kabla hazijatumika kwenye uhalifu. (Habari kwa Hisani ya Gerson Msigwa)

No comments:

Post a Comment