Monday, January 18, 2010

JK ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA WALIOUAWA UKEREWE!!!

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, kufuatia mauaji ya watu 12 katika Kisiwa cha Izinga, Wilaya ya Ukerewe, yaliyofanywa na majambazi, ambao pia wamejeruhi watu 15 katika shambulio hilo.

Rais Kikwete amesema kuwa mauaji hayo yaliyofanyika usiku wa kuamkia jana, Jumapili, ni kitendo cha kikatili na cha kulaaniwa kwa kila hali kwa sababu kimekatisha maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi habari za mauaji ya watu 12 katika Kisiwa cha Izinga. Napenda kutuma salamu za rambirambi zangu kwako wewe Mkuu wa Mkoa. Aidha, kupitia kwako, napenda kutoa pole kwa familia zote zilizopotolewa na wapendwa wao katika tukio hilo la kusikitisha,” amesemaRais katika salamu hizo.

Ameongeza Mheshimiwa Kikwete: “Napenda uwajulishe wafiwa kuwa mawazo yangu yote yako kwao katika kipindi hiki kigumu cha kupotelewa na wapendwa wao, tena ghafla, na kwa njia ya kikatili kiasi hiki. Nawatakia subira katika wakati huu wa msiba, na napenda kuwahakikishia kuwa msiba wao ni msiba wetu.”

Rais Kikwete amewatakia wale wote waliojeruhiwa katika tukio hilo haraka ya kupona na kurejea katika shughuli zao za maisha.

“Kwa wale waliojeruhiwa katika tukio hilo, nawatakia wapone haraka na kurudisha afya zao, ili waendelee kushiriki katika shughuli za maisha yao.” Amesema Rais Kikwete katika salamu hizo.

No comments:

Post a Comment