Thursday, January 28, 2010

JK AKUTANA NA CLINTON!!!!

Asante sana, Rais Kikwete
amwambia Bill Clinton

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amemshukuru Rais wa zamani wa Marekani, Rais Bill Clinton, kwa mchango wake katika maendeleo ya Tanzania, na hasa katika sekta ya afya na kupambana na maradhi.

Aidha, Rais Kikwete amemweleza Rais Clinton athari za kiuchumi ambazo zimeikumba Tanzania kutokana na msukosuko wa uchumi duniani na hatua zinachukuliwa na Serikali yake kupambana na msukosuko huo.

Rais Kikwete amemweleza hayo Rais Clinton wakati viongozi hao walipokutana na kufanya mazungumzo usiku wa leo, Jumanne, Januari 27, 2010, kwenye Jengo la Kirchner Museum, kwenye mji mdogo wa Davos ambako viongozi wote wawili watahudhuria Mkutano wa 40 wa Taasisi ya Uchumi Duniani ya World Economic Forum (WEF) unaoanza kesho, Jumatano, Januari 28, 2010.

Rais Clinton alikuwa ameomba kukutana na Rais Kikwete, hata kabla ya kiongozi huyo wa Tanzania kuwasili hapa kwa ajili ya Mkutano wa WEF wa siku tatu unaotarajiwa kuhudhuriwa na viongozi kutoka zaidi ya nchi 30 duniani.

Rais Kikwete na ujumbe wake wamewasili Davos, mji mdogo ulioko milimani nchini Uswisi usiku wa leo, wakitokea Sirte, Libya, ambako Rais Kikwete alisimama kukutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi.

Katika mkutano wake na Rais Clinton, Rais Kikwete amemshukuru kiongozi huyo wa zamani wa Marekani kwa misaada ambayo imekuwa inatolewa moja kwa moja na Taasisi za Clinton, ama kupitia taasisi nyingine, hasa katika sekta ya afya katika kupambana na magonjwa ya malaria, ukimwi na kifua kikuu.

“Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais kwa misaada yako, na napenda kukuhakishia ushirikiano wa Serikali yangu na wananchi wa Tanzania katika kuendeleza ushirikiano huo,” Rais Kikwete amemwambia Rais Clinton katika mazungumzo hayo yaliyochukua kiasi cha dakika 40.

Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Clinton alitaka kujua jinsi gani msukosuko wa uchumi duniani ulivyoathiri uchumi wa Tanzania na hatua ambazo Serikali ya Kikwete inachukua kukabiliana na athari hizo.

Rais Kikwete amemweleza athari hizo ikiwa ni pamoja na kushuka kwa bei ya mazao ya kilimo ya Tanzania kwenye soko la kimataifa, kupungua kwa mahitaji ya mazao hayo kwenye soko hilo, kupungua kwa idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania na kupungua kwa uwekezaji katika uchumi wa Tanzania.

“Tulikuwa tunatarajia kuona uwekezaji mkubwa katika uchimbaji wa madini aina ya bati na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuyenyusha bati, lakini wawekezaji katika maeneo hayo wameahirisha mipango ya uwekezaji wao hadi hali ya uchumi duniani itakaporekebika,” Rais Kikwete amemwambia Rais Clinton.

Rais Kikwete pia amemwambia Rais Clinton kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali yake kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kutangaza Mpango wa Kunusuru na Kuhami Uchumi wa Tanzania uliotangazwa na Rais Kikwete Juni, mwaka jana, 2009.

Rais Kikwete pia amesema kuwa chini ya Mpango huo, Serikali yake italinda mafanikio yaliyopatikana katika huduma za kijamii kama vile afya na elimu, na katika ujenzi wa miundombinu nchini, na hasa barabara kwa sababu ya umuhimu wa huduma hizo katika kuboresha maisha ya Watanzania.

Rais Kikwete anatarajiwa kuungana na viongozi wengine kutoka zaidi ya nchi 30 katika ufunguzi wa Mkutano wa 40 wa WEF unaoanza leo mjini hapa, Davos, Uswisi.

No comments:

Post a Comment