Wednesday, January 13, 2010

JK YUPO MSUMBIJI KUHUDHURIA KUAPISHWA KWA RAIS GUEBUZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, amewasili mjini Maputo, Mozambique, Jumatano, Januari 13, 2010, kuhudhuria sherehe za kuapishwa rasmi kwa Rais Mteule wa Mozambique, Mheshimiwa Armando Emillio Guebuza, kesho, Alhamisi, Januari 14, 2010.

Msafara wa Rais Kikwete unawashirikisha pia Mama Salma Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mzee Pius Msekwa, na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Katiba na Utawala wa Bora katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Ramadhan A. Shaaban.

Mheshimiwa Guebuza wa Chama cha Frelimo ataapishwa kesho kutumikia kipindi cha pili la Urais wa Msumbiji baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwishoni mwa Novemba, mwaka jana, 2009. Chama chake cha Frelimo pia kilipata ushindi mkubwa wa viti vya ubunge katika uchaguzi huo.

Sherehe za kuapishwa kwa Rais Guebuza zitafanyika kwenye eneo la Independence Square mjini Maputo, na zimepangwa kuchukua kiasi cha saa moja unusu kuanzia saa nne kasoro robo.

Sherehe hizo za kuapishwa kwa rais huyo mteule, zitafuatiwa na hafla maalum iliyopangwa kufanyika kwenye Ikulu ya Ponta Vermelha ambayo itamalizika saa tisa mchana na kuwashirikisha viongozi mbali mbali wanaoziwakilisha nchi zao katika sherehe hizo.

Rais Kikwete na ujumbe wake anatarajiwa kuondoka mjini Maputo mara baada ya halfa hiyo kurejea nyumbani.

Tanzania na Mozambique zina uhusiano wa miaka mingi wa kindugu tokea enzi chama cha Ferlimo kilipoanzishwa mjini Dar Es Salaam mwanzoni mwa miaka ya 60 na kupigana vita ya ukombozi kutoka mjini humo.

No comments:

Post a Comment