Wednesday, January 13, 2010

IKULU YAISHUKIA TANZANIA DAIMA

Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari, 13, 2010, limeandika habari zilizomkariri Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party, Bwana Christopher Mtikila akidai kuwa kufutiwa kwake dhamana na kuwekwa ndani katika kesi inayomkabili, kunatokana na kukataa kwake kuingizwa katika Mtandao wa kumsaidia Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ashinde uchaguzi Mkuu ujao.

Tunapata taabu kuamini kuwa Bwana Mtikila anaweza kusema mambo hayo kwa sababu habari hizo ni za uongo na uzushi mtupu. Kama ni kweli amesema hayo, basi ni jambo la kustaajabisha na kusikitisha. Kwa nini Bwana Mtikila ajaribu kuficha ukweli kuhusu sababu za kukamatwa? Amekamatwa kwa sababu amevunja masharti yake ya dhamana aliyopewa na Mahakama na siyo sababu zozote za kisiasa.

Aidha, Bwana Mtikila amesema uongo kwa sababu hakuna mtandao unaoitwa “Saidia Jakaya Kikwete ashinde”; hivyo suala la yeye kuombwa kujiunga nalo halipo. Ataombwaje kujiunga na kitu kisichokuwepo? Tunapenda kusisitiza kuwa hata mtandao Mheshimiwa Rais Kikwete hana. Mheshimiwa Rais hana sababu ya kuwa na kitu kama hicho kwa vile CCM ipo, na huo ndiyo mtandao wake wa kumsaidia kushinda.

Vile vile, Bwana Mtikila anadai kukutana na Katibu wa Rais kuhusu suala hili. Tunapenda kueleza kuwa Katibu wa Rais Ndugu Prosper Mbena hakumbuki kukutana na Bwana Mtikila, hata mara moja. Hivyo basi suala la yeye kuitwa na kukutana na Katibu wa Rais halina ukweli wowote.

Kama ni kweli amesema hayo, tunapenda kumshauri Bwana Mtikila aache kutaja visingizio visivyokuwepo na kupotosha ukweli kuhusu kesi yake. Haitamsaidia chochote. Badala yake aelekeze nguvu zake kupambana na mashitaka yanayomkabili katika kesi yake.

Tunaomba wananchi kupuuza na kudharau madai haya ya Bwana Mtikila kwa sababu ni uongo mtupu wa kutunga tu mitaani.

No comments:

Post a Comment