Friday, January 22, 2010

CUF YASHINDILIA MSUMARI MABADILIKO YA KATIBA!!

CUF – Chama cha Wananchi tunashangazwa na watu ambao wamekuwa wakionyesha msimamo wa kikatiba katika maamuzi ambayo yanaweza kuhatarisha amani kama yataendelea kuwapo pasipokupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Nchi nyingi zimepata machafuko ikiwemo jirani zetu wa Kenya, Zimbabwe na kwengineko kutokana na utekelezaji wa Katiba ambayo vifungu vyake vinautata na vinabaka demokrasia na kuwanyima wananchi imani juu ya maamuzi yanayofanywa na Tume ya Uchaguzi.

CUF Tunaendelea kusisitiza vifungu vilivyomo ndani ya katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanznaia hususani Ibara 74 (i), Ibara 74(5) na Ibara 74(12) ambazo iwapo kama Rais aliyeko madarakani pamoja na chama chake wanadhamira ya kuendelea kudumu madarakani wanaweza kuvitumia vifungu hivyo kwa maslaahi yao.

CUF – Tunawatanabaisha wapenda amani na demokrasia ya kweli ndani ya nchi, katiba siyo Msahafu wala Biblia, tumeitunga wenyewe wananchi kwa maslahi ya nchi yetu, iwapo kama vifungu vilivyomo utekelezaji wake unamashaka na kuhatarisha amani kwetu sisi wenyewe wananchi, ni vyema tukakaa chini na kurekebisha dosari hizo kuliko kuendelea kuitumia.

CUF – Tunaamini kiongozi muadilifu ni yule ambaye anawaongoza wananchi wake katika misingi ya kuleta amani ya kudumu, kwani machafuko yoyote ni chanzo cha umwagikaji damu, visasi vya kudumu na kuzorotesha maendeleo, hivyo basi mabadiliko ya Katiba yatakayopelekea kupatikana kwa Tume huru hayana ubishi, na kusogezwa mbele kwa uchaguzi wa Zanzibar ili Rais Amani Karume kuweka sawa mazingira ya Uchaguzi huru wa haki na wenye kuzingatia demokrasia ya kweli, nayo hayahitaji malumbano.

CUF – Tunawaasa Watanzania kuwa makini na viongozi ambao kwa kuchelea kuharibika kwa maslahi yao, wapo tayari kuona Watanzania tunauwana wenyewe kwa wenyewe huku wakitumia kigezo cha kuwa wanasimamia na kulinda katiba ya nchi, viongozi kama hawa tuwaogope kuliko UKIMWI.

No comments:

Post a Comment