Monday, January 18, 2010

RAIS KIKWETE AKUTANA NA VIONGOZI WA MGODI WA BARRICK!!!

MTENDAJI Mkuu na Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Barrick Gold, Bwana Aaron Regent amesema kuwa sehemu kubwa ya mapato yote yanatokana na shughuli za uchimbaji dhahabu zinazofanywa na kampuni hiyo nchini, yanabakia na kutumika hapa hapa nchini.

Aidha, Bwana Regent amesema kuwa kampuni inakamilisha mipango kabambe ya upanuzi wa shughuli zake katika Afrika na Tanzania.

Bwana Regent ameyasema hayo usiku wa Jumatatu, Januari 18, 2010, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye Ikulu Ndogo mjini Mwanza.

Rais Kikwete amewasili mjini Mwanza jioni ya jumatatu akiwa njiani kwenda mkoa jirani wa Shinyanga kuanza ziara ya siku tatu mkoani humo. Rais anaanza ziara ya Shinyanga Jumanne, Januari 19, 2010.

Bwana Regent amesema sehemu kubwa ya mapato ya kampuni hiyo kutokana na uchimbaji wa dhahabu katika Tanzania inaingia tena kwenye uchumi wa Tanzania kupitia shughuli mbali mbali.

Amezitaja shughuli hizi kuwa ni pamoja na malipo ya kodi, ununuzi wa bidhaa zinazotumiwa na kampuni hiyo, miradi ya ujenzi na ununuzi wa vifaa vya ujenzi.

Kampuni ya Barrick inachimba dhahabu katika maeneo ya Bulyanhulu, Tulawaka, Buzwagi na North Mara.

Naye Rais Kikwete amemwambia mtendaji mkuu huyo kuwa ni sera ya Tanzania kuhakikisha kuwa nchi inaendeleza raslimali zake ili kukuza uchumi na kupunguza umasikini nchini.

“Uchumi wetu huu hauwezi kukua bila kuendeleza raslimali zetu, kama vile dhahabu. Hivi ndivyo vyombo vitakavyobadilisha nchi hii na uchumi wake,” Rais Kikwete amemwambia Bwana Regent na ujumbe wake.

No comments:

Post a Comment