Tuesday, January 19, 2010

TANZANIA DAIMA MATATANI!!!

Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari, 13, 2010, limeandika habari zilizomkariri Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party, Bwana Christopher Mtikila akidai kuwa kufutiwa kwake dhamana na kuwekwa ndani katika kesi inayomkabili, kunatokana na kukataa kwake kuingizwa katika mtandao wa kumsaidia Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ashinde Uchaguzi Mkuu ujao.

Tunapata taabu kuamini kuwa Bwana Mtikila anaweza kusema hayo, kwa sababu habari hizo ni za uongo na ni uzushi mtupu. Kama ni kweli amesema hivyo ni jambo la kustaajabisha na kusikitisha. Kwa nini Bwana Mtikila ajaribu kuficha ukweli kuhusu sababu za kukamatwa kwake na kutafuta visingizio visivyokuwepo? Ukweli ni kwamba, amekamatwa kwa sababu amevunja masharti yake ya dhamana aliyopewa na Mahakama na siyo sababu nyingine zo zote.

Bwana Mtikila pia amesema uongo kwa sababu hakuna mtandao unaoitwa “Saidia Jakaya Kikwete ashinde” hivyo suala la yeye kuombwa kujiunga nao halipo. Ataombwaje kujiunga na kitu kisichokuwepo? Tunapenda kusisitiza kuwa Rais hana mtandao wo wote wa kumsaidia ashinde. Mheshimiwa Rais hana sababu ya kuwa na kitu kama hicho kwa vile CCM ipo. Kama kuna haja ya kuwa na mtandao wa kumsaidia ashinde hana haja ya kuhangaika kwani Chama cha Mapinduzi chenyewe ndiyo mtandao wake wa kumsaidia kushinda. Ilikuwa hivyo mwaka 2005 na itakuwa hivyo 2010. Hana haja ya kutafuta mtu yeyote nje ya CCM. Chama cha Mapinduzi kina viongozi, wanachama wa CCM na wapenzi toka Nyumba Kumi mitaani na vijijini mpaka ngazi ya taifa. Wanatosha.

Vile vile, tunapenda kueleza kuwa Katibu wa Rais ni Ndugu Prosper Mbena na yeye hakumbuki kukutana na Bwana Mtikila hata mara moja. Hivyo basi suala la yeye kuitwa na kukutana na Katibu wa Rais halina ukweli wo wote. Hata Ndugu Kassim Mtawa ambaye ni Katibu wa Rais Msaidizi hakumbuki wakati wowote kuzungumza na Bwana Mtikila kuhusu kumtaka ajiunge na mtandao huo usiokuwepo. Tunapenda kumshauri Bwana Mtikila aelekeze nguvu zake kukabiliana na mashitaka yanayomkabili katika kesi yake badala ya kusema mambo yasiyokuwepo na kupotosha ukweli kuhusu kesi yake.

Tunaomba wananchi kupuuza na kudharau madai haya ya Bwana Mtikila kwa sababu ni uongo mtupu na uzushi usiokuwa na chembe ya ukweli.

No comments:

Post a Comment