Tuesday, January 12, 2010

SALAMU ZA RAMBIRAMBI PEMBA

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Januari 12, 2010, amewatembelea na kuwajulia hali majeruhi walioumia wakati wanajaribu kuingia katika Uwanja wa Michezo wa Gombani, Chake Chake, Pemba, kuhudhuria Sherehe za Miaka 46 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete amewatembelea majeruhi hao kwenye Hospitali ya Chake kabla hajaondoka Pemba kurudi Dar Es salaam baada ya kuwa amehudhuria sherehe hizo za Mapinduzi ya Zanzibar.

Watu 15 wameumia na mwingine mmoja kupoteza maisha wakati maelfu kwa maelfu ya wananchi walipokuwa wanasukumana kuingia katika Uwanja wa Gombani kwa ajili ya kuhudhuria sherehe hizo za Mapinduzi.

Kwa zaidi ya dakika 40, Rais Kikwete na Mama Salma, walimpa pole binafsi kila mmoja wa watu hao, wakiwamo wanawake tisa na wanaume sita.

Rais Kikwete na Mama Salma wamerejea mjini Dar Es Salaam jioni ya leo baada ya kuwa wamehudhuria sherehe hizo.

No comments:

Post a Comment