Wednesday, January 27, 2010

JK ATOA SHUKURANI KWA GADAFFI!!!!

Tanzania yaishukuru Libya kwa misaada ya athari za mafuriko

Tanzania imeishukuru Libya kwa misaada yake ya kibinadamu ambayo nchi hiyo ya Afrika Kaskazini imetoa kwa Tanzania kusaidia watu walioathiriwa na athari za mvua na mafuriko ya hivi karibuni katika mikoa ya Dodoma na Morogoro.

Shukurani hizo zimetolewa usiku wa kuamkia leo, Jumatano, Januari 27, 2010, na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Libya katika mazungumzo yake na Kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi mjini Sirte, Libya.

Rais Kikwete alisimama kwa muda mjini Sirte, Libya, kwa mazungumzo na Kanali Gaddafi akiwa njiani kwenda Davos, Uswisi, kuhudhuria Mkutano wa 40 wa Taasisi ya Uchumi Duniani ya World Economic Forum unaoanza kesho, Alhamisi, Januari 29, 2010, na kushirikisha viongozi kutoka nchi zaidi ya 30 duniani.

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemwambia Kanali Gaddafi: “Nakushukuru sana kwa misaada yako ya kibinadamu ambayo Serikali yako imeipatia nchi yangu kufuatia mafuriko na athari nyingine zilizosababishwa na mvua katika Tanzania.”

Rais Kikwete amemwambia Kanali Gaddafi kuwa familia zipatazo 26,000 zilikuwa hazina mahali ya kukaa baada ya nyumba zao kubomolewa katika mafuriko hayo na kuwa zilikuwa zinaishi katika kambi za muda.

Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko hayo ni wilaya za Mpwapwa katika Mkoa wa Dodoma na hasa Wilaya ya Kilosa katika Mkoa wa Morogoro, ambayo imebeba athari kubwa zaidi za mafuriko hayo kutokana na mvua zilizonyesha kuanzia wiki ya mwisho ya Desemba, mwaka jana, hadi wiki ya kwanza ya Januari, mwaka huu.

“Tunakushukuru kwa mahema, kwa dawa, na kwa misaada mingine ambayo imetoa mchango mkubwa na kuleta tofauti kubwa katika maisha ya watu wetu walioathiriwa na mafuriko hayo. Tulikuwa na ukame wa miaka miwili mfululizo, na mvua zilipoamua kunyesha zikaja wa hasira kubwa,” Rais Kikwete amemwambia kiongozi huyo wa Libya.

Rais amesema kuwa mafuriko hayo, yaliyotokana na mito miwili, ukiwamo Mto Mkondoa kuacha njia za asili na kubomoa kingo, yameharibu mno miundombinu ya barabara na reli kiasi cha kwamba Serikali ya Tanzania inahitaji kiasi cha dola za Marekani milioni 15 kukarabati miundombinu hiyo.

“Ni hasara kubwa kwetu. Kiasi cha dola za Marekani milioni 15 ni nyingi kwa nchi masikini kama Tanzania lakini tumeamua kuwa ukarabati huo utakuwa umekamilika katika muda mfupi”.

Jumatatu, wiki hii, mjini Dar Es Salaam, Rais Kikwete aliitisha mkutano maalum wa viongozi na wataalam wa Wizara ya Miundombinu, taasisi na makampuni yaliyoko chini ya wizara hiyo, kujadili hali ya uharibifu kwenye miundombinu hiyo, na hatua za haraka kukarabati miundombinu hiyo.

Rais Kikwete aliamua kusimama Libya na kushauriana na Kanali Gaddafi kuhusu masuala kadhaa yanayohusu Umoja wa Afrika (AU) na Mkutano wa wiki ijayo wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU unaofanyika kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Kanali Gaddafi ni Mwenyekiti wa AU anayemaliza muda wake wa uongozi katika mkutano wa wiki ijayo, na alipata uenyekiti huo kutoka kwa Rais Kikwete mwaka 2009.

No comments:

Post a Comment