Thursday, January 28, 2010

KITIM TIM CHA NUSU FAINAL AFCON LEO!!!





Miamba minne ambayo iatachuana kusaka nafasi mbili za kutinga Fainal katika michezo ya Nusu Fainal ambayo itapigwa usiku wa leo.

JK AKUTANA NA CLINTON!!!!

Asante sana, Rais Kikwete
amwambia Bill Clinton

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amemshukuru Rais wa zamani wa Marekani, Rais Bill Clinton, kwa mchango wake katika maendeleo ya Tanzania, na hasa katika sekta ya afya na kupambana na maradhi.

Aidha, Rais Kikwete amemweleza Rais Clinton athari za kiuchumi ambazo zimeikumba Tanzania kutokana na msukosuko wa uchumi duniani na hatua zinachukuliwa na Serikali yake kupambana na msukosuko huo.

Rais Kikwete amemweleza hayo Rais Clinton wakati viongozi hao walipokutana na kufanya mazungumzo usiku wa leo, Jumanne, Januari 27, 2010, kwenye Jengo la Kirchner Museum, kwenye mji mdogo wa Davos ambako viongozi wote wawili watahudhuria Mkutano wa 40 wa Taasisi ya Uchumi Duniani ya World Economic Forum (WEF) unaoanza kesho, Jumatano, Januari 28, 2010.

Rais Clinton alikuwa ameomba kukutana na Rais Kikwete, hata kabla ya kiongozi huyo wa Tanzania kuwasili hapa kwa ajili ya Mkutano wa WEF wa siku tatu unaotarajiwa kuhudhuriwa na viongozi kutoka zaidi ya nchi 30 duniani.

Rais Kikwete na ujumbe wake wamewasili Davos, mji mdogo ulioko milimani nchini Uswisi usiku wa leo, wakitokea Sirte, Libya, ambako Rais Kikwete alisimama kukutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi.

Katika mkutano wake na Rais Clinton, Rais Kikwete amemshukuru kiongozi huyo wa zamani wa Marekani kwa misaada ambayo imekuwa inatolewa moja kwa moja na Taasisi za Clinton, ama kupitia taasisi nyingine, hasa katika sekta ya afya katika kupambana na magonjwa ya malaria, ukimwi na kifua kikuu.

“Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais kwa misaada yako, na napenda kukuhakishia ushirikiano wa Serikali yangu na wananchi wa Tanzania katika kuendeleza ushirikiano huo,” Rais Kikwete amemwambia Rais Clinton katika mazungumzo hayo yaliyochukua kiasi cha dakika 40.

Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Clinton alitaka kujua jinsi gani msukosuko wa uchumi duniani ulivyoathiri uchumi wa Tanzania na hatua ambazo Serikali ya Kikwete inachukua kukabiliana na athari hizo.

Rais Kikwete amemweleza athari hizo ikiwa ni pamoja na kushuka kwa bei ya mazao ya kilimo ya Tanzania kwenye soko la kimataifa, kupungua kwa mahitaji ya mazao hayo kwenye soko hilo, kupungua kwa idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania na kupungua kwa uwekezaji katika uchumi wa Tanzania.

“Tulikuwa tunatarajia kuona uwekezaji mkubwa katika uchimbaji wa madini aina ya bati na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuyenyusha bati, lakini wawekezaji katika maeneo hayo wameahirisha mipango ya uwekezaji wao hadi hali ya uchumi duniani itakaporekebika,” Rais Kikwete amemwambia Rais Clinton.

Rais Kikwete pia amemwambia Rais Clinton kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali yake kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kutangaza Mpango wa Kunusuru na Kuhami Uchumi wa Tanzania uliotangazwa na Rais Kikwete Juni, mwaka jana, 2009.

Rais Kikwete pia amesema kuwa chini ya Mpango huo, Serikali yake italinda mafanikio yaliyopatikana katika huduma za kijamii kama vile afya na elimu, na katika ujenzi wa miundombinu nchini, na hasa barabara kwa sababu ya umuhimu wa huduma hizo katika kuboresha maisha ya Watanzania.

Rais Kikwete anatarajiwa kuungana na viongozi wengine kutoka zaidi ya nchi 30 katika ufunguzi wa Mkutano wa 40 wa WEF unaoanza leo mjini hapa, Davos, Uswisi.

Wednesday, January 27, 2010

SERENA WILLIAMS ATINGA FAINAL AUSTRALIA OPEN!!!









Bingwa mtetezi wa Taji la Australia Open Serena Williams amefanikiwa kutinga katika hatua ya fainal baada ya kumfunga Li Na kwa seti mbili kwa nunge. Serena amepata matokeo ya 7-6 katika kila seti

MAN UTD YAIONDOA CITY CARLING CUP!!!





Mabingwa watetezi wa Kombe la Carling Manchester United wamefanikiwa kutinga hatua ya fainal baada ya kuifunga Manchester City kwa magoli 3-1 kwenye mchezo wa nusu fainal. Magoli ya Paul Scholes, Michael Carrick na Wayne Rooney yametosha kuipa ushindi Man Utd na sasa itacheza na Aston Villa tarehe 28 February.

JK ATOA SHUKURANI KWA GADAFFI!!!!

Tanzania yaishukuru Libya kwa misaada ya athari za mafuriko

Tanzania imeishukuru Libya kwa misaada yake ya kibinadamu ambayo nchi hiyo ya Afrika Kaskazini imetoa kwa Tanzania kusaidia watu walioathiriwa na athari za mvua na mafuriko ya hivi karibuni katika mikoa ya Dodoma na Morogoro.

Shukurani hizo zimetolewa usiku wa kuamkia leo, Jumatano, Januari 27, 2010, na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Libya katika mazungumzo yake na Kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi mjini Sirte, Libya.

Rais Kikwete alisimama kwa muda mjini Sirte, Libya, kwa mazungumzo na Kanali Gaddafi akiwa njiani kwenda Davos, Uswisi, kuhudhuria Mkutano wa 40 wa Taasisi ya Uchumi Duniani ya World Economic Forum unaoanza kesho, Alhamisi, Januari 29, 2010, na kushirikisha viongozi kutoka nchi zaidi ya 30 duniani.

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemwambia Kanali Gaddafi: “Nakushukuru sana kwa misaada yako ya kibinadamu ambayo Serikali yako imeipatia nchi yangu kufuatia mafuriko na athari nyingine zilizosababishwa na mvua katika Tanzania.”

Rais Kikwete amemwambia Kanali Gaddafi kuwa familia zipatazo 26,000 zilikuwa hazina mahali ya kukaa baada ya nyumba zao kubomolewa katika mafuriko hayo na kuwa zilikuwa zinaishi katika kambi za muda.

Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko hayo ni wilaya za Mpwapwa katika Mkoa wa Dodoma na hasa Wilaya ya Kilosa katika Mkoa wa Morogoro, ambayo imebeba athari kubwa zaidi za mafuriko hayo kutokana na mvua zilizonyesha kuanzia wiki ya mwisho ya Desemba, mwaka jana, hadi wiki ya kwanza ya Januari, mwaka huu.

“Tunakushukuru kwa mahema, kwa dawa, na kwa misaada mingine ambayo imetoa mchango mkubwa na kuleta tofauti kubwa katika maisha ya watu wetu walioathiriwa na mafuriko hayo. Tulikuwa na ukame wa miaka miwili mfululizo, na mvua zilipoamua kunyesha zikaja wa hasira kubwa,” Rais Kikwete amemwambia kiongozi huyo wa Libya.

Rais amesema kuwa mafuriko hayo, yaliyotokana na mito miwili, ukiwamo Mto Mkondoa kuacha njia za asili na kubomoa kingo, yameharibu mno miundombinu ya barabara na reli kiasi cha kwamba Serikali ya Tanzania inahitaji kiasi cha dola za Marekani milioni 15 kukarabati miundombinu hiyo.

“Ni hasara kubwa kwetu. Kiasi cha dola za Marekani milioni 15 ni nyingi kwa nchi masikini kama Tanzania lakini tumeamua kuwa ukarabati huo utakuwa umekamilika katika muda mfupi”.

Jumatatu, wiki hii, mjini Dar Es Salaam, Rais Kikwete aliitisha mkutano maalum wa viongozi na wataalam wa Wizara ya Miundombinu, taasisi na makampuni yaliyoko chini ya wizara hiyo, kujadili hali ya uharibifu kwenye miundombinu hiyo, na hatua za haraka kukarabati miundombinu hiyo.

Rais Kikwete aliamua kusimama Libya na kushauriana na Kanali Gaddafi kuhusu masuala kadhaa yanayohusu Umoja wa Afrika (AU) na Mkutano wa wiki ijayo wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa AU unaofanyika kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Kanali Gaddafi ni Mwenyekiti wa AU anayemaliza muda wake wa uongozi katika mkutano wa wiki ijayo, na alipata uenyekiti huo kutoka kwa Rais Kikwete mwaka 2009.

Tuesday, January 26, 2010

JK APAA KWENDA USWISI!!!!

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini leo tarehe 26, mchana kuelekea Davos, Uswiss kuhudhuria kikao cha kila mwaka kuhusu uchumi, World Economic Forum.

Kikao hicho kinachoanza tarehe 28 hadi 30 Januari, kinahudhuriwa na Viongozi Wakuu wa nchi, Wachumi, Viongozi wa Mashirika mbalimbali, Wanataaluma, Viongozi wa Dini na Wanaharakati mbalimbali duniani.

Mara baada ya kikao cha Davos, Rais Kikwete ataelekea Addis Ababa Ethiopia kuhudhuria Kikao cha kila mwaka cha Wakuu wa Nchi za Afrika, kitakachoanza tarehe 31Januari hadi tarehe 2, Februari mwaka huu.

Mara baada ya kikao cha Viongozi wa Afrika Rais Kikwete anatarajia kurudi Dar-es-Salaam.

MURRAY, HENIN WATINGA NUSU FAINAL AUSTRALIA OPEN!!!




Mchezaji ambaye anaorodheshwa katika nafasi ya mbili kwa ubora wa Mchezo wa Tennis Duniani upande wa wanaume Roger Federer ameondolewa katika Michuano ya Wazi ya Australia baada ya kupata kichapo kutoka kwa Andy Murray.

Federer ameondoshwa katika mashindano ya Tennis ya Australia katika hatua ya robo fainali baada ya kukubali kichapo cha seti mbili kwa bila kabla ya kupata maumivu ya goti na kushindwa kuendelea na seti ya tatu.

Katika seti ya kwanza Murray aliweza kushinda kwa sita tatu kabla ya kushinda katika seti ya pili kwa saba sita na ndipo kunako seti ya tatu wakati akiongoza kwa tatu bila ndipo Federer alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia.

Naye Andy Roddick amefungishwa virago katika hatua ya robo fainali baada ya kukubalia kichapo cha seti tatu kwa mbili huku akifanikiwa kutoka nyuma na kusawazisha seti mbili na mchezo kuwa droo kabla ya kufungwa seti ya mwisho.

Roddick amechapwa na Marin Cilic kutoka Croatia na sasa kijana huyo atakuwa na kirabua dhidi ya Andy Murray katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo inayoendelea nchini Australia.

Kwa upande wa wanawake Justine Henin ametinga hatua ya nusu fainali baada ya kuvuna ushindi wa seti mbili kwa buyu dhidi ya Nadia Petrova katika mchezo uliokuwa mkali.

Henin ameshinda seti ya kwanza kwa saba sita kabla ya kuja katika seti ya pili na kushinda kwa saba tano na hivyo kujikatia tiketi yake ya kutinga hatua ya nusu fainali ya Mixhezo hiyo ya Wazi inatimua vumbi huko Australia.

Monday, January 25, 2010

JK AWASHUKIA MIUNDOMBINU!!!

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametaka kuchukuliwa kwa hatua za haraka kutengeneza upya miundombinu nchini, hasa reli na barabara, iliyoharibiwa kutokana na mvua na mafuriko ya wiki za karibuni katika baadhi ya mikoa nchini.

Mheshimiwa Rais pia amehimiza ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za kiraia na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kukabiliana na kazi ya kukarabati miundombinu hiyo.

“Uchumi huu utaishiwa sana nguvu kama hatukushughulikia haraka suala la kukarabati miundombuni na hasa reli,” Rais Kikwete amekiambia kikao cha dharura alichokiitisha mchana wa leo, Jumatatu, Januari 25, 2010, Ikulu, Dar es Salaam, kujadili kiwango cha uharibifu na jinsi ya kunusuru miundombinu ya reli na barabara.

Rais Kikwete aliagiza kufanyika kwa kikao hicho Ijumaa iliyopita, Januari 22, 2010, wakati alipoendesha kikao cha Baraza la Mawaziri.

Waziri wa Miundombinu, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa amewaongoza maofisa waandamizi kutoka wizara yake na kutoka baadhi ya makampuni na mashirika yaliyoko chini ya wizara yake, ikiwamo Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Wakala wa Barabara (Tanroads) katika kikao cha leo.

Katika kikao hicho, maofisa hao walimweleza Rais Kikwete uharibifu uliofanyika katika Reli ya Kati na hasa kati ya Stesheni za Gulwe na Kilosa, katika mikoa ya Dodoma na Morogoro, kutokana na mvua zilizonyesha katika wilaya za Mpwapwa na Kilosa kati ya Desemba 24, mwaka jana, 2009 na Januari 10, mwaka huu, 2010.

Katika maeneo ya Kilosa, mvua hizo na mafuriko yaliyoandamana na mvua hizo, yameng’oa kabisa sehemu ya Reli ya Kati na kusimamisha huduma za reli hiyo kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Sababu kubwa za uharibifu huo ni kufurika na kwa mito ya Mkondoa na Kinyasungwi, hali iliyosababisha kuhama kwa mito hiyo kutoka katika njia za asili na kuelekea kwenye tuta la reli.

Maofisa hao wamemweleza Rais Kikwete kuwa zipo sehemu 28 zilizoharibika kati ya stesheni hizo mbili lakini ni sehemu 26 zilizoaharibika zaidi. Pia wamemweleza kuwa madaraja tisa yamesombwa na maji na mengine matatu yako katika hatari ya kusombwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Mhandisi Omar Chambo pia amemweleza Rais Kikwete mipango ya ukarabati wa sehemu hiyo ya reli na kuahidi kuwa kazi hiyo inaweza kuwa imekamilika kati ya miezi miwili na miezi mitatu.

Kuhusu uharibifu kwenye barabara, Mhandisi Chambo amesema kuwa uharibufu kwenye barabara umefanyika katika mikoa 18 ya Tanzania Bara.

Mikoa hiyo ni Arusha, Dodoma, Iringa, Kagera, Kilimanjaro, Kigoma, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.

Mhandisi Chambo amesema kuwa kiasi cha sh bilioni 13.286 zinahitajika kuweza kukarabati barabara hizo ambazo zimeharibika kwa viwango tofauti huku uharibifu mkubwa ukiwa umetokea katika Mkoa wa Dodoma ambako barabara zake tatu hazipitiki.

MISRI, NIGERIA ZAFUZU NUSU FAINAL!!





Mabingwa Watetezi Misri na Nigeria zimekuwa timu mbili za mwisho kukamilisha idadi ya timu nne zilizotinga katika hatua ya Nusu Fainal ya Dimba la Mataifa ya Afrika.
Misri wamefuzu baada ya kuifunga Cameroon Simba Wasiofugika kwa jumla ya magoli 3-1. Nigeria wamefuzu baada ya kushinda kwa penalty 5-4 dhidi ya Zambia Chipolopolo.

CHEMICAL ALI AJIUA!!!!



Ali Hassan al-Majid maarufu kama Chemical Ali ambaye ni Kiongozi wa zamani wa Serikali ya Rais Saddam Hussein pia ni binamu ya Kiongozi huyo ameamua kujiua kwa kujinyonga siku kadhaa baada ya Mahakama ya nchi hiyo kumuhukumu adhabu ya kifo cha kunyongwa hadi kufa. Chemical Ali anatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya Wakurdi zaidi ya Laki Tano mnamo mwaka 1988.

MANCINI ATAKA ROBINHO ABAKI!!!!


Kocha wa Klabu ya Manchester City, Roberto Mancini ametangaza naye ya kutaka kumbakiza mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil ambaye kwa sasa hana namba ya kudumu katika kikosi chake Robinho. Mshambuliaji huyo ametangaza nia yake ya kutaka kuongoza Eastlands kutokana na kukosa namba ya kudumu

INTER MILAN, REAL MADRID ZASHINDA!!!!




Klabu ya Inter Milan imevuna ushindi wa magoli 2-0 mbele ya AC Milan katika mchezo wa Ligi ya Serie A. Magoli ya Diego Milito na lile la Goran Pandev yalitosha kuip ushidni Inter Milan. Nchini Spain Real Madrid imeshinda magoli 2-0 kwa magoli ya Cristiano Ronaldo.

GHANA, ALGERIA WATINGA NUSU FAINAL AFCON!!!



Wawakilishi wawili wa Bara la Afrika kwenye Kombe la Dunia Ghana na Algeria wamefanikiwa kufuzu katika hatua ya nusu fainali ya Michuano ya Dimba la Mataifa ya Afrika. Ghana wamefuzu baada ya kuwafunga wenyeji Angola goli 1-0. Algeria wamewaondosha Ivory Coast kwa kuwachabanga magoli 3-2.

ETHIOPIAN AIRLINE YAANGUKA BEIRUT!!!!



Ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia ambayo ilikuwa inatoka Nchini Lebanon katika mji wa Beirut imeanguka mapema asubuhi kilometa 3.5 tangu iruke kutoka Kiwanja cha ndege. Ndege hiyo ambayo ilikuwa na abiria 83 na wafanyakazi 7 imeanguka baada ya kupotea katika radar dakika chache tangu iruke. Taarifa zinaeleeza kuwa Rubani akaielekeza kwenye Bahari ya Mediteranean na mpaka sasa watu saba wameshaokolewa wakiwa hai.

Friday, January 22, 2010

NEVILLE NA TEVEZ KUTOPEWA ADHABU!!!


Chama Cha Soka Nchini England FA kimetangaza kutowachukulia hatua wachezaji Gary Neville wa Manchester United na Carlos Tevez wa Manchester City baada ya kuoneshana ishara ambazo si za kiungwana. Licha ya wacheazaji hao kukwepa rungu la adhabu lakini FA imewaonya wachezaji hao kwa tabia hiyo

RIOBA AREJEA KWENYE KURUNZI LA MLIMANI!!!









Hatimaye Ayub Rioba arejea tena kwenye Kurunzi la Mlimani baada ya kukabiliwa na majukumu mengi ya Kitaifa. Rioba ambaye ni Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC). Huyu ni mwanahabari ambaye amebobea na pia ndiye mwanzilishi wa Kurunzi la Mlimani. Karibu Rioba tuendeleza jahazi la Mlimani Tv Elimu Kwanza.

WANANCHI HAITI WAANZA KUHAMISHWA!!!


Siku kumi baada ya nchi ya Haiti kupigwa na tetemeko la ardhi mamia ya wananchi wameanza kuhamishwa kutoka katika maeneo ambayo yameathirika. Wengi wa wakazi kutoka Mji Mkuu Porto-au-Prince ambao hawana makazi wameanza kuhama. Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu laki nne hawana makazi nchini Haiti

WAPINZANI WASHINIKIZA RAIS YAR'ADUA AACHIE MADARAKA!!!


Kambi ya Upinzani nchini Nigeria imeetisha maandamano ya kushinikiza Rais wa nchi hiyo Umar Yar'Adua aachie ngazi kutokana na kuendelea kukabiliwa na maradhi ya moyo. Rais Yar'Adua amekuwa nchini Saudi Arabia kwa muda sasa akipatiwa matibabu

CUF YASHINDILIA MSUMARI MABADILIKO YA KATIBA!!

CUF – Chama cha Wananchi tunashangazwa na watu ambao wamekuwa wakionyesha msimamo wa kikatiba katika maamuzi ambayo yanaweza kuhatarisha amani kama yataendelea kuwapo pasipokupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Nchi nyingi zimepata machafuko ikiwemo jirani zetu wa Kenya, Zimbabwe na kwengineko kutokana na utekelezaji wa Katiba ambayo vifungu vyake vinautata na vinabaka demokrasia na kuwanyima wananchi imani juu ya maamuzi yanayofanywa na Tume ya Uchaguzi.

CUF Tunaendelea kusisitiza vifungu vilivyomo ndani ya katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanznaia hususani Ibara 74 (i), Ibara 74(5) na Ibara 74(12) ambazo iwapo kama Rais aliyeko madarakani pamoja na chama chake wanadhamira ya kuendelea kudumu madarakani wanaweza kuvitumia vifungu hivyo kwa maslaahi yao.

CUF – Tunawatanabaisha wapenda amani na demokrasia ya kweli ndani ya nchi, katiba siyo Msahafu wala Biblia, tumeitunga wenyewe wananchi kwa maslahi ya nchi yetu, iwapo kama vifungu vilivyomo utekelezaji wake unamashaka na kuhatarisha amani kwetu sisi wenyewe wananchi, ni vyema tukakaa chini na kurekebisha dosari hizo kuliko kuendelea kuitumia.

CUF – Tunaamini kiongozi muadilifu ni yule ambaye anawaongoza wananchi wake katika misingi ya kuleta amani ya kudumu, kwani machafuko yoyote ni chanzo cha umwagikaji damu, visasi vya kudumu na kuzorotesha maendeleo, hivyo basi mabadiliko ya Katiba yatakayopelekea kupatikana kwa Tume huru hayana ubishi, na kusogezwa mbele kwa uchaguzi wa Zanzibar ili Rais Amani Karume kuweka sawa mazingira ya Uchaguzi huru wa haki na wenye kuzingatia demokrasia ya kweli, nayo hayahitaji malumbano.

CUF – Tunawaasa Watanzania kuwa makini na viongozi ambao kwa kuchelea kuharibika kwa maslahi yao, wapo tayari kuona Watanzania tunauwana wenyewe kwa wenyewe huku wakitumia kigezo cha kuwa wanasimamia na kulinda katiba ya nchi, viongozi kama hawa tuwaogope kuliko UKIMWI.

ZAMBIA NA CAMEROON ZATINGA ROBO FAINAL!!!



Timu za Taifa za Zambia na Cameroon zimekamilisha orodha ya Mataifa nane ambayo yamefanikiwa kufuzu katika hatua ya Robo Fainal ya AFCON. Zambia wamefanikiwa kumaliza wakiwa vinara wa Kundi D huku Cameroon wakiwa washindi wapili.

Tuesday, January 19, 2010

TANZANIA DAIMA MATATANI!!!

Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari, 13, 2010, limeandika habari zilizomkariri Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party, Bwana Christopher Mtikila akidai kuwa kufutiwa kwake dhamana na kuwekwa ndani katika kesi inayomkabili, kunatokana na kukataa kwake kuingizwa katika mtandao wa kumsaidia Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ashinde Uchaguzi Mkuu ujao.

Tunapata taabu kuamini kuwa Bwana Mtikila anaweza kusema hayo, kwa sababu habari hizo ni za uongo na ni uzushi mtupu. Kama ni kweli amesema hivyo ni jambo la kustaajabisha na kusikitisha. Kwa nini Bwana Mtikila ajaribu kuficha ukweli kuhusu sababu za kukamatwa kwake na kutafuta visingizio visivyokuwepo? Ukweli ni kwamba, amekamatwa kwa sababu amevunja masharti yake ya dhamana aliyopewa na Mahakama na siyo sababu nyingine zo zote.

Bwana Mtikila pia amesema uongo kwa sababu hakuna mtandao unaoitwa “Saidia Jakaya Kikwete ashinde” hivyo suala la yeye kuombwa kujiunga nao halipo. Ataombwaje kujiunga na kitu kisichokuwepo? Tunapenda kusisitiza kuwa Rais hana mtandao wo wote wa kumsaidia ashinde. Mheshimiwa Rais hana sababu ya kuwa na kitu kama hicho kwa vile CCM ipo. Kama kuna haja ya kuwa na mtandao wa kumsaidia ashinde hana haja ya kuhangaika kwani Chama cha Mapinduzi chenyewe ndiyo mtandao wake wa kumsaidia kushinda. Ilikuwa hivyo mwaka 2005 na itakuwa hivyo 2010. Hana haja ya kutafuta mtu yeyote nje ya CCM. Chama cha Mapinduzi kina viongozi, wanachama wa CCM na wapenzi toka Nyumba Kumi mitaani na vijijini mpaka ngazi ya taifa. Wanatosha.

Vile vile, tunapenda kueleza kuwa Katibu wa Rais ni Ndugu Prosper Mbena na yeye hakumbuki kukutana na Bwana Mtikila hata mara moja. Hivyo basi suala la yeye kuitwa na kukutana na Katibu wa Rais halina ukweli wo wote. Hata Ndugu Kassim Mtawa ambaye ni Katibu wa Rais Msaidizi hakumbuki wakati wowote kuzungumza na Bwana Mtikila kuhusu kumtaka ajiunge na mtandao huo usiokuwepo. Tunapenda kumshauri Bwana Mtikila aelekeze nguvu zake kukabiliana na mashitaka yanayomkabili katika kesi yake badala ya kusema mambo yasiyokuwepo na kupotosha ukweli kuhusu kesi yake.

Tunaomba wananchi kupuuza na kudharau madai haya ya Bwana Mtikila kwa sababu ni uongo mtupu na uzushi usiokuwa na chembe ya ukweli.

Monday, January 18, 2010

MISAADA YAANZA KUWAFIKIA WAATHIRIKA HAITI!!!



Juma moja tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi baya kuwahi kupiga nchi ya Haiti katika kipindi cha zaidi ya miaka mia mbili hatimaye misaada imeanza kuwafika baadhi ya wananchi. Licha ya baadhi ya maeneo kupata misaada hiyo lakini kuna wale ambao mpaka sasa hawajapata msaada wa aina yoyote. Mji wa Port0-au-Prince umezingirwa na harufu kali iliyosababishwa na maiti ambazo zimezagaa na kushindwa kuzikwa kutokana na nguvu kubwa kuelekezwa kwa manusura.

RAIS KIKWETE AKUTANA NA VIONGOZI WA MGODI WA BARRICK!!!

MTENDAJI Mkuu na Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Barrick Gold, Bwana Aaron Regent amesema kuwa sehemu kubwa ya mapato yote yanatokana na shughuli za uchimbaji dhahabu zinazofanywa na kampuni hiyo nchini, yanabakia na kutumika hapa hapa nchini.

Aidha, Bwana Regent amesema kuwa kampuni inakamilisha mipango kabambe ya upanuzi wa shughuli zake katika Afrika na Tanzania.

Bwana Regent ameyasema hayo usiku wa Jumatatu, Januari 18, 2010, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye Ikulu Ndogo mjini Mwanza.

Rais Kikwete amewasili mjini Mwanza jioni ya jumatatu akiwa njiani kwenda mkoa jirani wa Shinyanga kuanza ziara ya siku tatu mkoani humo. Rais anaanza ziara ya Shinyanga Jumanne, Januari 19, 2010.

Bwana Regent amesema sehemu kubwa ya mapato ya kampuni hiyo kutokana na uchimbaji wa dhahabu katika Tanzania inaingia tena kwenye uchumi wa Tanzania kupitia shughuli mbali mbali.

Amezitaja shughuli hizi kuwa ni pamoja na malipo ya kodi, ununuzi wa bidhaa zinazotumiwa na kampuni hiyo, miradi ya ujenzi na ununuzi wa vifaa vya ujenzi.

Kampuni ya Barrick inachimba dhahabu katika maeneo ya Bulyanhulu, Tulawaka, Buzwagi na North Mara.

Naye Rais Kikwete amemwambia mtendaji mkuu huyo kuwa ni sera ya Tanzania kuhakikisha kuwa nchi inaendeleza raslimali zake ili kukuza uchumi na kupunguza umasikini nchini.

“Uchumi wetu huu hauwezi kukua bila kuendeleza raslimali zetu, kama vile dhahabu. Hivi ndivyo vyombo vitakavyobadilisha nchi hii na uchumi wake,” Rais Kikwete amemwambia Bwana Regent na ujumbe wake.

JK ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA WALIOUAWA UKEREWE!!!

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, kufuatia mauaji ya watu 12 katika Kisiwa cha Izinga, Wilaya ya Ukerewe, yaliyofanywa na majambazi, ambao pia wamejeruhi watu 15 katika shambulio hilo.

Rais Kikwete amesema kuwa mauaji hayo yaliyofanyika usiku wa kuamkia jana, Jumapili, ni kitendo cha kikatili na cha kulaaniwa kwa kila hali kwa sababu kimekatisha maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi habari za mauaji ya watu 12 katika Kisiwa cha Izinga. Napenda kutuma salamu za rambirambi zangu kwako wewe Mkuu wa Mkoa. Aidha, kupitia kwako, napenda kutoa pole kwa familia zote zilizopotolewa na wapendwa wao katika tukio hilo la kusikitisha,” amesemaRais katika salamu hizo.

Ameongeza Mheshimiwa Kikwete: “Napenda uwajulishe wafiwa kuwa mawazo yangu yote yako kwao katika kipindi hiki kigumu cha kupotelewa na wapendwa wao, tena ghafla, na kwa njia ya kikatili kiasi hiki. Nawatakia subira katika wakati huu wa msiba, na napenda kuwahakikishia kuwa msiba wao ni msiba wetu.”

Rais Kikwete amewatakia wale wote waliojeruhiwa katika tukio hilo haraka ya kupona na kurejea katika shughuli zao za maisha.

“Kwa wale waliojeruhiwa katika tukio hilo, nawatakia wapone haraka na kurudisha afya zao, ili waendelee kushiriki katika shughuli za maisha yao.” Amesema Rais Kikwete katika salamu hizo.

HENRY AKWEPA RUNGU LA FIFA!!!!


Mshambuliaji wa Kimataifa wa France na Klabu ya Barcelona Thierry Henry amekwepa rungu la adhabu la FIFA kutokana na kuunawa mpira kwa maksudi katika mchezo wa kutafuta tiketi ya Kombe la Dunia dhidi ya Jamhuri ya Ireland. Henry amekutwa hana hatia ya kufanya kitendo hicho makusudi na kamati ya nidhamu ya FIFA.

MALI YATUPWA NJE AFCON LICHA YA KUSHINDA!!!!



Timu ya Taifa ya Mali imeondolewa katika michuano ya Dimba la Mataifa ya Afrika licha ya kupata ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya Malawi. Magoli ya Mali yamefungwa na Fredrick Kanoute, Seydou Keita na Mamadou Bagayoko. Angola na Algeria wamefanikiwa kufuzu kutoka Kundi A. Huku Algeria yeye ikifuzu kutokana na sheria za mashindano hayo kumbebe.