Thursday, December 24, 2009

SALAMA ZA X-MASS KUTOKA KWA RAIS KIKWETE

MUENDELEZO WA SALAMU ZA X-MASS KATIKA MAADHIMISHO YAKE
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mama Salma Kikwete, wanatoa Salamu za Heri na Fanaka za Sikukuu ya Krismas kwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Rais pamoja na Mama Kikwete wanawatakia Watanzania wote sikukuu salama, yenye furaha, amani na utulivu. Aidha, anawaomba madereva, hususani wa magari ya abiria kuwa waangalifu zaidi wanapokuwa kazini barabara katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Krismas na ile ya Mwaka Mpya.

Na katika kuadhimisha Sikukuu hiyo, Rais Kikwete, kama ilivyo jadi, ametoa mkono maalum wa heri kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapa zawadi ya kuwawezesha nao kusherehekea sikukuu hiyo kwa furaha, kama walivyo watoto wengine wa Tanzania.

Mbali na kutoa zawadi kwa watoto hao yatima, Mheshimiwa Rais pia ametoa zawadi ya namna hiyo kwa Wazee, waliopo katika nyumba maalum za wazee.

Watakaonufaika na zawadi hiyo ya Mheshimiwa Rais, ambayo ni vyakula ni walioko katika vituo 28 vya mikoa minane ya Tanzania Bara.

Vituo hivyo ni saba vya Mkoa wa Dar es Salaam, vyote vilivyoandikishwa rasmi katika Mikoa ya Dodoma, Kigoma, Mwanza, Tabora na Tanga, na kituo kimoja kimoja katika mikoa ya Iringa na Arusha.

Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, vitanufaika vituo vine: Nyumba ya Wazee ya Sebleni iliyoko Unguja, na Nyumba ya Wazee ya Limbani, Pemba na vituo viwili vya watoto yatima vya Mabaoni na Istikama vilivyoko Pemba.

Kwa mara nyingine, Mheshimiwa Rais Kikwete, na mkewe Mama Salma Kikwete wanawatakia Watanzania wote Sikukuu yenye Heri ya Krismas.

No comments:

Post a Comment