Thursday, December 10, 2009

JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI YAZIDI KUJIPANGA

MWENYEKITI WA JUMUIYA YA EAC AKUTANA NA BODI YA BARAZA LA BIASHARA LA EAC

Jumuiya ya Afrika Mashariki imedhamiria kuweka kipaumbele kwa watu wake na kuwawezesha wafanyibiashara ili kuimarisha na kujenga jumuiya yenye nguvu.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, amesema hayo leo katika Ikulu ya Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Bodi ya Baraza la Biashara la Afrika Mashariki.

“Mkataba wa Jumuiya hii unatoa kipaumbele kwa watu wake na kulenga katika kuiwezesha sekta binafsi, ndiyo maana tumeweka nguvu zetu nyingi katika kuweka mazingira mazuri ya kuweza kupata masoko na kurahisisha biashara baina ya nchi hizi na majirani zake” amesema na kuelezea kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki imetoa kipaumbele katika kurahisisha mawasiliano na uchukuzi ili iwe rahisi kwa wananchi wake pamoja na sekta binafsi kushika usukani katika soko hili la pamoja.

Rais amesema nchi za Afrika Mashariki kwa pamoja kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki, zimetoa kipaumbele katika kuimarisha mawasiliano ya barabara kati ya nchi hizi na pia kutoka nchi za jumuiya na zile za jirani ya nchi hizi, ili kuwezesha na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu katika nchi hizi.

Rais amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki imedhamiria kufanya hivyo hivyo katika sekta za reli, usafiri wa anga na zinginezo ili kurahisisha usafiri baina ya watu na biashara zao katika jitihada za kutafuta masoko.

Rais Kikwete amewataka wajumbe wa bodi na baraza la biashara, kumpa taarifa ya changamoto na vikwazo wanavyokutana navyo katika kufanya biashara na kutafuta masoko katika jumiya hii ili viongozi wa nchi zote tano wapate kuzitafutia ufumbuzi na hatimaye kukutana na baraza hilo mwakani kujadili na kutafuta suluhisho la vikwazo hivyo.

Mapema leo asubuhi Rais Kikwete ameongoza Baraza la Mawaziri katika kujadili mambo muhimu na yanayohitaji kutiliwa mkazo katika mkutano wa kimataifa unaofanyika huko Copenhagen, Denmark unaojadili mabadiliko ya Tabianchi.

Swala la Tabia nchi limeleta madhara makubwa duniani kutokana na ongezeko la gesi joto na kusababisha mabadiliko na athari kubwa ya hali ya hewa duniani.

No comments:

Post a Comment