Thursday, December 17, 2009

RAMBIRAMBI ZA KIFO CHA LAWRENCE GAMA

RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA FAMILIA NA NDUGU WA MAREHEMU LAWRENCE GAMA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Alhamisi, Desemba 17, 2009, ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Marehemu Mzee Lawrence Gama, kufuatia kifo cha mzee huyo, aliyepata kuwa mwanasiasa na mtumishi mwandamizi wa umma, kilichotokea mjini Dar es Salaam jana, Jumatano, Desemba 16, 2009.

“Nimeshtushwa na kuhuzunishwa sana na habari za kifo cha Mzee Lawrence Gama, Mtanzania mwenzetu aliyepata kuwa mtumishi hodari wa umma na mwakilishi mwenye uwezo mkubwa wa wananchi wa Jimbo la Songea mjini, kilichotokea jana katika Hospitali ya Aga Khan mjini Dar es Salaam,” amesema Rais Kikwete katika salamu hizo za rambirambi.

Rais Kikwete amesema kuwa Mzee Gama alikuwa kiongozi mfano wa uaminifu na uadilifu katika nafasi zote ambazo alipata kuzishikilia katika maisha yake.

“Iwe katika utumishi wa Serikali ambako alipata kuwa Mkuu wa Mkoa, iwe katika utumishi wa Jeshi ambako alipata kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT), iwe utumishi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambako alipata kuwa Katibu Mkuu, ama kwenye nafasi ya uwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Songea Mjini ambako alipata kuwa Mbunge, Mzee Gama alikuwa mfano wa uongozi bora, na Taifa letu litakosa sana busara zake na mchango wake mkubwa katika jitihada za kujitafutia maendeleo,” amesema Rais Kikwete.

Rais Kikwete amesema kuwa kwa wakati huu wa msiba mawazo yake yako kwa familia ya Mzee Gama ambayo imepotelewa na babu, baba, mzazi, mlezi na kiongozi wa kuaminika.

“Naungana nanyi – familia nzima, ndugu, jamaa na marafiki wa Mzee Gama- katika kuomboleza msiba huu mkubwa. Nawatakieni subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo,” amesema Rais Kikwete katika salamu hizo za rambirambi.

“Naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu ailaze pema roho ya Marehemu Lawrence Gama,” Rais Kikwete anamalizia salamu zake za ramnbirambi.

No comments:

Post a Comment