Tuesday, December 22, 2009

JAMBAZI LAKAMATWA

JESHI LA POLISI MKOANI RUVUMA LIKIWA KAZINI

Polisi Mkoani RUVUMA wamemkamata mtu mmoja aitwaye JOSEPH LUSINDE ambaye amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu kutokana na kutoroka adhabu ya kifungo cha miaka 74 Jela kutokana na kupatikana na hatia ya mashitaka manne tofauti, yanayohusiana na Uuaji, Ubakaji na Wizi.

JOSEPH LUSINDE mwenye umri wa miaka 30, MKazi wa MAKAMBAKO mkoani IRINGA amekamatwa katika kituo kidogo cha basi cha MSAMALA hapa Mjini SONGEA majira ya saa 11 alfajiri akiwa katika harakati za kusafirisha mali za wizi alizoziiba kutoka kwa wakazi wa manispaa ya SONGEA.

Mtu huyu anayehusishwa na matukio lukuki ya uhalifu, inadaiwa alishahukumiwa na mahakama ya wilaya ya Songea kutumikia miaka 14 kwa kosa la uvunjaji na wizi, kisha akahukumiwa miaka 30 Jela baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na pia alihukumiwa miaka mingine 30 Jela baada ya kupatikana na hatia ya Mauaji huko MAKAMBAKO Mkoani IRINGA.

Kwa Maelezo ya Kamanda KAMUHANDA Mtu huyu alifanikiwa kutoroka adhabu hizi kwa kuwa kwanza alikuwa nje kwa dhamana na akiwa katika dhamana alitenda makosa mengine na kuhukumiwa pasipo yeye mwenyewe kuwapo mahakamani.

Kama waswahili walivyosema za mwizi Arobaini, na Arobaini za JOSEPH LUSINDE zikamfikia Desemba 21 mwaka huu saa 11 alfajiri, alipobambwa na vifaa vya ndani kama Luninga, Deck, Radio na Nguo ambavyo aliiba kwa nyakati tofauti katika nyumba za wakazi wa hapa Mjini SONGEA.

Kamanda KAMUHANDA anasema baadhi ya vitu hivyo vimeanza kutambuliwa na walioibiwa baadhi yao wakiwa ni ABENEGO SAKAFU na DOMINICA HAULE ambao waliripoti polisi hivi karibuni baada ya kuvunjiwa nyumba zao na kuibiwa.

Katika hali ambayo sio ya kawaida Mke wa JOSEPH LUSINDE aitwaye ZARAFI ZARAMALENGA amekamatwa na Polisi wa kituo kikuu cha hapa SONGEA wakati akimpelekea mmewe Chakula aina ya Pilau.

Polisi wamemkamata ZARAFI baada ya kubaini kuwa ndani ya chakula hicho alificha Hirizi kwa lengo la kumfikishia mmewe. Alipohojiwa juu ya Hirizi hizo amejitetea kuwa ni kinga.

Nimemuuliza kamanda wa Polisi Mkoani Hapa MICHAEL KAMUHANDA kukamatwa kwa JOSEPH LUSINDE kwaweza kuwa mwisho wa Mtandao wa uvunjaji nyumba za watu na wizi Wakati Polisi wa hapa RUVUMA wakiahidi kujiimarisha hapa Mkoani katika kudhibiti uhalifu, bado taarifa zinaonesha ipo kazi kubwa ya kushugulikia mtandao wa waharifu walio nje ya Mkoa huu ambao wamekuwa wakihusiana na waharifu wa hapa ndani.

Kama itakumbukwa vyema mwezi uliopita Mtu mmoja aliyewatapeli walimu zaidi ya shilingi milioni 5 Mkazi wa Kilimanjaro alishirikiana na wenzake kadhaa wa hapa Ruvuma, na katika kipindi hicho hicho Mtu mwingine akateka motto wa miaka minne na kasha kumrejesha baada ya kutekelezewa madai ya kupewa shilingi milioni 2 (Habari kwa hisani ya Mdau Gerson Msigwa)

No comments:

Post a Comment