Wednesday, December 23, 2009

CUF WATAKA VITENDO NA SI MANENO MATUPU

JAJI LEWIS MAKAME TUNATAKA TUONE MKITEMBEA KWENYE KAULI ZENU NA SIYO PROPAGANDA.
CUF – Chama cha Wananchi tumepokea kwa tahadhari kubwa maonyo aliyoyatoa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame kwa Maafisa wa Polisi nchini juu ya Uchaguzi Mkuu ujao Oktoba 2010.

Jaji Lewis makame aliwaonya Maafisa hao wa Polisi kuwa ni makosa kujihusisha na Siasa kwani watakuwa wanakiuka Katiba ya Nchi lakini pia wao kama askari wajibu wao mkubwa ni kutetea, kulinda na kudumisha amani na wanapaswa kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ujao hivyo wahakikishe uchaguzi unakuwa wa haki na amani.

CUF – Tumeipokea kwa tahadhari kubwa kauli hii na tena inatutia mashaka kwani Jaji Lewis Makame akiwa ni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa alitakiwa kuwa mkweli kwa kukemea yale yote yaliyofanywa na askari Polisi hapa nchini katika vipindi vya uchaguzi vilivyopita.

Jeshi la Polisi limekuwa likijihusisha kikamilifu na siasa na uchaguzi kwa kuegemea upande wa Chama cha Mapinduzi hasa katika maeneo ambayo yamekusudiwa Chama hicho kushinda kwa hali yoyote, ambapo imebidi askari kukimbia na masanduku ya kupigia kura yakiwa na kura ndani.


Hali hiyo ilijitokeza katika chaguzi za Serikali za mitaa zilizoranyika Oktoba mwaka huu katika mtaa wa Zombokoni Manispaa ya Temeke, Mtaa wa Muungano na Kagera katika Manispaa ya Kinondoni..

Hivyo kama haitoshi matukio kama hayo yalijitokeza katika chaguzi za 2005 na 2000 katika uchaguzi wa Zanzibar, lakini pia jeshi la Polisi limediriki kuwatisha wapiga kura siku moja kabla ya siku ya upigaji kura ambapo mwaka 2005 aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo nchini Omari Mahita akionyeshwa katika televisheni mbalimbali nchini akiwa ameshikilia visu vyenye mipini ya rangi ya bendera za CUF alidai wamekamata kontena nzima ya visu na majamvia yaliyotarajiwa kutumiwa na Chama chetu katika uchaguzi huo.

Tukio jengine la kusikitisha ni lile lilofanyika siku moja kabla ya uchaguzi wa 2000 katika mkutano wa hadhara wa kufunga kampeni kwa chama cha CUF pale Jangwani Dar es Salaam ambapo kwa makusudi jeshi la Polisi liliamua kuwapiga mabomu ya machozi na kutishia kwa riasi za moto wananchi waliokuwa wanatoka mkutanoni.


CUF – Chama cha Wananchi tunasisitiza kuwa tunaipokea kwa tahadhari kubwa kauli za Mwenyekiti wa Tume ya taifa ya Uchaguzi Jaji Lewis Makame, halikadhalika tunamtahadharisha Mkuu wa jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema kutofuata nyayo za Mkuu wa jeshi hilo aliyemtangulia ambaye aliligeuza jina jeshi hilo na kuliita ngunguri ili kukabiliana na kauli mbiu ya Chama cha Siasa cha CUF cha kuwataka wanachama wake kuwa ngangari.

No comments:

Post a Comment