Saturday, December 19, 2009

JK NA RAMBIRAMBI ZA AJALI YA SAME

RAIS KIKWETE AKIWA SAME KWA AJILI YA KUTOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Ijumaa, Desemba 18, 2009, ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 19 waliopoteza maisha yao katika ajali ya gari iliyotokea wilayani Same, Mkoani Kilimanjaro, jana, Alhamisi, Desemba 17, 2009.

Katika salamu hizo ambazo pia amezipishia kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Ndugu Monica Ngenzi Mbega, Mhe. Kikwete amesema kuwa amepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za vifo vya watu hao 19.

Katika ajali hiyo, kwenye Kijiji cha Kolandoto, Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro, basi la Mohamed Trans lililokuwa linasafiri kutoka Nairobi, Kenya, kwenda Dar es Salaam, liligongana na basi dogo aina ya Coaster.

Rais Kikwete amesema katika salamu zake hizo za rambirambi: “ Kwa dhati ya moyo wangu, natoa salamu za rambirambi kwako wewe Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kutokana na ajali hiyo, iliyotokea katika eneo lako la utawala na kusababisha kupotea kwa maisha ya watu 19 wasio na hatia.”

Ameongeza Rais Kikwete katika salamu hizo: “Aidha, kupitia kwao, napenda kwa dhati kabisa kuwapa pole familia, ndugu, jamaa na marafiki wa watu wote walipoteza maisha yao katika ajali hiyo. Namwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema peponi. Nawaomba wote wawe na moyo wa usajiri na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya ndugu zao.”

Rais Kikwete vile vile amewatakia wote walioumia katika ajali hiyo baraka za Mwenyezi Mungi ili wapone haraka na kuweza kurejea haraka katika shughuli zao za maisha.

No comments:

Post a Comment