Monday, December 14, 2009

JK AKUTANA NA WANAMAFIA

RAIS KIKWETE AMEKUTANA NA WANANCHI WA MAFIA AMBAO WANAISHI UGHAIBUNI LAKINI WANACHANGIA HAPA NCHINI.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amekutana na viongozi na wanachama wa vikundi viwili visivyo vya kiserikali vinavyofanya shughuli za maendeleo katika jamii na kufanya nao mazungumzo.

Viongozi hao wa Kikundi cha Maendeleo cha Mafia (Mafia Development Foundation) na kikundi cha Kiislamu kinachotoa misaada katika Jamii (Islamic Help) chenye makao yake nchini Uingereza wakiongozwa na Mbunge wa Mafia, Mheshimiwa Abdulkarim Esmail Hassan Shah.

Mheshimiwa Shah amemueleza Rais Kikwete kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na kikundi cha Islamic Help cha Uingereza ambazo ni pamoja na kusaidia katika shughuli za jamii na kuwa tayari kikundi hicho kimeshachimba visima virefu vya maji.

Lengo la kikundi hicho ni kuchimba visima vipatavyo sabini (70) katika vijiji mbalimbali katika mji wa Mafia, kutoa vyandarua 5000 (Elfu tano) kwa wananchi wa Mafia na kutoa madawati kwa ajili ya shule kadhaa.

Rais amewashukuru kwa mchango wao mkubwa na kuwaomba waendelee na moyo huo huo wa kujitolea kwani zinasaidia na kuunga mkono juhudi zake za kuwapatia wananchi maisha bora.

“Lengo letu katika serikali ni kuhakikisha kuwa asilimia 90 ya wananchi wetu mijini wanapata maji safi na salama ifikapo mwaka 2010 na asilimia 65 ya wakazi wa vijijini, hivyo tukipata marafiki na watu wema katika kuchangia juhudi hizi ni jambo la kufurahisha sana”. Amesema na kuongeza kuwa juhudi kama hizi za kikundi cha Islamic Help kinasaidia pia katika kuwaondolea wakina mama mzigo wa kutafua maji kwa masaa mengi na pia kuwaepushia wananchi na magonjwa yanayotokana na maji yasiyo safi na salama.

Rais pia amewapongeza vijana hao kwa kutoa msaada wa vyandarua 5000 (Elfu tano) kwa wananchi wa Mafia na kusisitiza azma ya serikali kuwa juhudi kama hizi ni mchango mkubwa kwa wananchi na serikali yao.

Hata hivyo amesema lengo kubwa la serikali ni hatimaye kutokomeza vyanzo vyote vya malaria ambavyo ni mbu na mazalia yake kwa kuwa ugonjwa huu ni hatari na unaongoza kwa idadi ya vifo.

No comments:

Post a Comment