Wednesday, June 30, 2010

WAFANYABIASHARA WALIA NA TRA SONGEA!!!

WAFANYABIASHARA mbalimbali katika Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, wamesema watamwandikia barua Rais Jakaya Kikwete kulalamikia kitendo cha serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuwalazimisha kulipa kodi kubwa inayosababisha biashara zao kufa.

Aidha, wamesema watamwandikia Rais Kikwete kuikataa sheria mpya ya ukusanyaji kodi kupitia mfumo mpya wa kudhibiti mapato kwa kutumia mashine maalumu ya Electronics kwa madai hauna manufaa kwa wananchi na umelenga kushibisha matumbo ya wachache.

Wafanyabiashara hao wameyasema hayo jana wakati wa mkutano ulioandaliwa na TRA mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kuwafahamisha wafanyabiashara juu ya mfumo mpya wa kudhibiti mapato kwa kutumia mashine hizo.

Wamesema wamechoshwa na vitendo vya serikali kupitia mamlaka hiyo kwa kuwachezea rafu mara kwa mara katika kutimiza malengo yao ya kukusanya kodi kwani wamekuwa wakiwakadiria kodi kubwa bila kuangalia hali ya biashara zao ina nguvu kiasi gani.

Wamesema wamefikia hatua hiyo kutokana na TRA mkoani humo kudai kuwa wanatekeleza sheria na maagizo yaliyotolewa na serikali hivyo hata kama mkoa umepangiwa kodi kubwa ni lazima ipigane kufa na kupona ili kutimiza lengo lao.

John Rupia amesema amesena kama serikali ndiyo inayotumika kuwanyonya wananchi wake basi watamwamndikia barua Rais Kikwete kulalamikia suala hilo wakidai kuwa unasababisha biashara zao kufa kutokana na kulipa kodi kubwa.

Aidha, kwa upande wa mashine hizo Bw. Rupia amesema zimeletwa kwa ajili ya kushibisha matumbo ya wachache kwa madai kuwa upo uwezekano wa kuuziwa bei kubwa hata kama bei yake ni ndogo.

Ameeleza kuwa wana wasiwasi na mtiririko wa kuuziwa mashine hizo kwani unaonesha wazi kuwa una mianya ya kuwanufaisha baadhi ya watu huku wakitilia mashaka makampuni yaliyopewa kazi ya kusambaza mashine hizo kwa wafanyabiashara.

Kwa mujibu wa Ofisa wa TRA mkoa wa Ruvuma kitengo cha utoaji elimu kwa mlipa kodi, Msetti Jackson, mashine hizo zinauzwa kuanzia milioni Moja hadi Tano na kwamba makampuni yaliyopewa tenda ya kusambaza mashine hizo yapo Sita tu.

Amesema makampuni hayo yatasambaza na kutoa elimu kwa wauzaji wa maduka yaliyosajiriwa na VAT namna ya kuzitumia huku akitaja sifa lukuki za mashine hizo katika kudhibiti mapato ikiwemo ya utunzaji wa kumbukumbu kwa miaka Mitano na kwamba imeunganishwa mtandao moja kwa moja na TRA. (Habari na Emmanuel Msigwa)

No comments:

Post a Comment