Friday, June 25, 2010

IKULU YAISHUKIA TENA MWANA HALISI!!!

Gazeti la Mwananchi la Jana, Alhamisi, Juni 24, 2010 lilichapisha habari kwenye ukurasa wake wa kwanza chini ya kichwa cha habari “Mgombea mwenza sasa aipasua CCM”. Kichwa hicho cha habari kilinogeshwa na kichwa cha habari kidogo kisemacho “Kamati Kuu yaondoa Mahakama ya Kadhi kwenye Ilani”.

Katika habari hiyo, miongoni mwa mambo mengine, gazeti hili lilisema “Hadi sasa, vyanzo mbalimbali vya habari vinasema Meghji ni chaguo la Rais Kikwete ambaye katika uongozi wake amewapa wanawake nafasi nyingi ikiwemo ya wizara nyeti ya fedha iliyoenda kwa Meghji katika baraza lake la kwanza”. Liliongeza Mwananchi katika habari hiyo, “Kwa mujibu wa vyanzo hivyo ndani na nje ya CCM, msimamo wa Rais Kikwete bado unampendekeza Meghji kuwa mgombea mwenza.”

Tunapenda kufafanua kuwa habari kwamba Mheshimiwa Meghji ni chaguo la Mheshimiwa Rais Kikwete kwa nafasi ya Mgombea Mwenza siyo habari ya kweli. Hayo ni mawazo na matakwa binafsi ya waandishi wa habari hiyo na katu si msimamo wa Rais Kikwete. Si jambo ambalo amelizungumza na mtu yeyote hivyo hakuna chanzo chochote cha ndani na nje ya CCM cha kuzungumzia msimamo wa Rais kwa jambo hili. Kwa sasa Rais anashukuru suala la mgombea mwenza hajaanza kulishughulikia kwani wakati wake bado. Hivyo maneno hayo hayana chembe ya ukweli.

Siyo sawa kabisa kwa waandishi hao wa habari kusema uongo kuhusu mawazo na uamuzi wa Mheshimwia Rais ambao haupo na kujifanya kuwa ni kweli. Kufanya hivyo ni kufanya kazi ya uandishi bila kujali wajibu wa kusema ukweli na weledi. Ni kupotosha jamii kwa kiasi cha kusikitisha.

Kusingekuwa na tatizo kama habari hiyo ingeandikwa kama ubashiri au uchambuzi wa sifa za mtu ambae waandishi wanamuona anafaa kuwa Mgombea Mwenza wa Mheshimiwa Rais Kikwete. Lakini, kufanya maoni na mapenzi yao kuwa mawazo na uamuzi wa Rais ni kutomtendea haki Kiongozi Mkuu wa nchi yetu.

Kwa mara nyingine tena napenda kusema kuwa Serikali inaheshimu na itaendelea kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari lakini waandishi wautumie uhuru huo kutoa habari zilizokuwa za kweli. Wajiepushe na kutoa habari zisizokuwa za kweli. Kugushi habari au kupotosha ukweli ni utovu wa hali ya juu wa maadili ya uandishi wa habari.

“Habari ya gazeti la Mwananchi kudai kuthibitisha kuwa Mheshimiwa Rais tayari amemchagua Mgombea Mwenza na kudai kwamba kuwa mgongano wa mawazo ndani ya Chama kuhusu chaguo hilo, siyo ya kweli na siyo ya haki kwa waandishi wa habari kumsingizia Mheshimiwa Rais kwa jambo ambalo hajalifanya. Mchakato wake ndani ya Chama haujaanza”.

Tunapenda kumalizia kwa kurudia kuwashauri waandishi wa habari, kujiepusha kuandika habari za ubashiri wao kama vile ni habari ya kweli au kuandika habari za uongo, habari za kufitinisha na kugonganisha watu na kupotosha watu na jamii. Hii ni hatari kwa utulivu wa nchi na siyo mifano ya heshima ya taaluma ya uandishi wa habari nchini Tanzania.

No comments:

Post a Comment