Thursday, June 3, 2010

CUF YAZUNGUMZIA UCHOMWAJI WA VITUO VYA POLISI!!!

CUF – Chama cha Wananchi tunalitaka jeshi la Polisi lisitafute mchawi katika sakata la wananchi kuchoma moto magari na kituo cha Polisi cha Hedaru mkoani Kilimanjaro, mwanzoni mwa wiki hii, wanatakiwa wajichunguze sababu zakupelekea wananchi kukosa imani na chombo chao cha Dola.

Tukio hilo ambalo lilifanywa na wananchi zaidi ya mia 300 wenye hasira, ambao walivamia kituo hicho cha Polisi cha Hedaru kinachokadiriwa kuwa na askari 10 wasio na silaha za moto waliojisalimisha kwa kumbia pamoja na watuhumiwa wanane ambao ndio chanzo cha wananchi hao kukivamia kituo hicho ili kuwaadhibu.

Watuhumiwa hao ambao walikamatwa na wananchi na kuletwa kituoni hapo baada ya askari kutolipa uzito unaostahili tuhuma za watu hao kudaiwa kumtorosha mtoto kwa ajili ya kumtumia kwa imani za kishirikina za kumtoa kafara kwenye machimbo ya madini yaliyo msitu wa Shengena.

CUF – Pamoja na kulaani vitendo vya wananchi kuvamia vituo vya polisi, matukio ambayo yanazidi kushika kasi hapa nchini, lakini ni wajibu wa jeshi la Polisi kujichunguza chanzo kilichopelekea wananchi kukosa imani na chombo chao cha dola, wasiishie kuwakamata na kuwatia hatiani, vitisho sio sulihisho la kujenga imani ya wananchi kwao.

CUF – Chama cha Wananchi tunamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani Lawrance Masha, awajibike kwa kujiuzulu nafasi hiyo, kwani tumechoshwa kusikia kila wakati wananchi kukosa imani na jeshi hilo ambalo limekosa uadilifu katika majukumu yake ya kulinda raia na mali zake.

CUF – Tunawatanabaisha Watanzania kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi imelitengeza jeshi la Polisi kuwa chombo cha kuhakikisha kinawalinda viongozi walioko madarakani wasiondolewe kwa hali yoyote hata kama hawatakiwi na wananchi, ndio sababu vituo vya kulinda raia na mali zao havina silaha, lakini silaha hupatikana kwa wingi wakati wa uchaguzi hadi zile za kijeshi ili kutisha wananchi kutumia haki yao ya kidemokrasia, hivyo ni lazima wafanye mabadiliko ya kuhakikisha CCM hairudi madarakani katika uchaguzi ujao.

No comments:

Post a Comment