Sunday, June 27, 2010

MV SONGEA YASITISHA SAFARI ZA MALAWI!!

MELI ya Mv Songea inayofanya safari zake katika nchi ya Tanzania na Malawi kupitia Ziwa Nyasa, imeshindwa kuendelea na safari zake kutokana na abiria wa meli hiyo kusitisha safari zao kwenda Malawi kwa madai kuwa wananyanyaswa na askari wa nchi hiyo.

Habari zilizothibishwa jana na baadhi ya wafanyabiashara katika Bandari ya Mbambabay, wilaya ya Ziwa Nyasa ambao hufanya safari zao nchini Malawi kwa ajili ya kununua mahitaji mbalimbali, zimesema kuwa meli hiyo imesitisha safari zake kutokana na kukosa abiria tangu Juni 22 mwaka huu.

Wafanyabiashara hao wamesema meli hiyo imelazimika kusimama safari zake kutokana na kukosa abiria na mizigo ya kutoka Malawi kutokana na unyanyasaji mkubwa unaofanywa na askari wa nchi hiyo huku wengi wao wakidai kuwa wamekuwa wakichapwa viboko.

Bw. John Nindi ambaye ni mmoja wa abiria wa meli hiyo amedai kuwa wamechoshwa kunyanyaswa hivyo wameamua kuchukua hatua za kupumzike ili mamlaka husika kama zipo zichukue hatua na kuona namna ya kuwasaidia.

Naye Bw. Peter Ndunguru amesema masharti yote ya kwenda Malawi yanazingatiwa lakini cha kushangaza wakifika huko askari huwalazimisha kutoa fedha zingine na wanaoshindwa kufanya hivyo huchapwa viboko.

Mmoja wa Maofisa wa Bandari hiyo ya Mbambabay iliyopo katika wilaya mpya ya Ziwa Nyasa ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa madai kuwa yeye siyo msemaji wa bandari hiyo, alikiri meli hiyo kusitisha safari zake kati ya Tanzania na Malawi na kudai kuwa meli hiyo imesitisha safari zake kutokana na kuharibika mfumo wa gia boksi.

Amedai kuwa si kweli kwamba meli hiyo imesitisha safari kutokana na kukosa abiria na mizigo ya kwenda Malawi isipokuwa imeharibika mfumo wa gia boksi ambapo tayari wameshapeleka oda katika kampuni ya Sub-Scania Dar es Salaam zinakotengenezwa kwani meli hiyo inatumia injini ya Scania.

Kusitishwa kwa safari ya meli hiyo kumeleta manung’uniko makubwa kwa vijana wanaofanya shughuili za kubeba mizigo na kudai kuwa hali hiyo imewasababishia kukosa kipato cha kuendeshea maisha yao. (Habari kwa Hisani ya Emmanuel Msigwa)

No comments:

Post a Comment