Wednesday, June 30, 2010

KAMPENI ZAZIDI KUSHIKA KASI KWA WABUNGE!!!

Mbunge wa Mbinga Magharibi, mkoa wa Ruvuma, Kapteni John Komba amewaomba wananchi wa jimbo lake kumfilisi fedha zote kwa ajili kutatua matatizo yao na kwamba hateteleki na wagombea wanaojitokeza kuwania nafasi hiyo katika jimbo hilo.

Kapteni Komba ameyasema hayo huku akijihakikishia kwa asilimia 100 kwamba amefanikiwa kutatua matatizo mbalimbali ya wananchi kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu, maji, afya, miundombinu ya barabara na mengineyo.

Akizungumza na wananchi wa vijiji mbalimbali katika jimbo hilo hivi karibuni ambalo kwa sasa limepewa jina la wilaya ya Ziwa Nyasa, Kepten Komba amewaambia wananchi hao kuwa bado ana kiu ya kutaka kuendelea kuwasaidia.

Amesema kuwa mafanikio makubwa waliyoyapata hadi sasa yanatokana na jitihada zake binafsi na kwamba ana kiu ya kuendelea kuwasaidia huku akijinadi kuwa Mungu hakukosea kuwapa chaguo lake.

Hata hivyo amesema wanasiasa wanaojitokeza kugombea nafasi hiyo katika jimbo la Mbinga Magharibi hawana nguvu ya kushindana naye kwani wananchi bado wana imani naye kutokana na kufanikiwa kuleta mabadiliko makubwa katika kipindi kifupi cha miaka mitano.

Aidha, amewaasa wapiga kura wake kuwaogopa kama ukoma wanasiasa wanaotaka madaraka kwa kigezo cha kutumia ukabila kwani wamepitwa na wakati hivyo wametakiwa kuchagua kiongozi makini ambaye ana uwezo wa kuleta maendeleo mbalimbali pamoja na kupiga vita umaskini.

Amewataka wananchi wakati wa kupiga kura utakapofika wamchague tena ili aweze kumalizia kazi ambazo alikuwa amezianzisha katika harakati za kuwasaidia kuondokana na kero zilizokuwa zikiwakabili kwa muda mrefu.

Jumla ya wagombea Wanne ndiyo waliojitokeza kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo la Mbinga magharibi hadi sasa akiwemo Bw. Stanley Vumu, Bw. Alex Shauri na wengine waliotambulika kwa majina ya Bw. Haule na Bw. Mangwea. (Habari na Mdau Emmanuel Msigwa)

No comments:

Post a Comment