Tuesday, June 22, 2010

RAIS KIKWETE AKUTANA NA BILL CLINTON!!!

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo katika Ikulu ya Dar-Es-Salaam amefanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Marekani Mh. Bill Clinton ambaye amekuja Tanzania kutembelea na kuangalia shughuli zinavyoendelea katika mfuko wake unajishughulisha na shughuli za upatikanaji wa huduma za afya duniani, Clinton Health Acess Initiative (CHAI)

Katika mazungumzo yao, pamoja na Rais Kikwete kumshukuru Bw. Clinton kwa mchango wake hapa nchini katika sekta ya afya, viongozi hao wamezungumzia hali ya kisiasa na maendeleo ya Tanzania.

Mchango huo wa Bw. Clinton hapa nchini ni katika maswala ya HIV/AIDS ambapo mfuko wa Bill Clinton unasaidi kutoa dawa za kupunguza makali na athari za Ukimwi (ARVs).

Bw. Clinton amekua mstari wa mbele katika kuchagia makampuni mengi kupewa nafasi ya kutengeneza dawa za ARV na hivyo kuweza kushuka kwa bei na hatimaye watu wengi hasa katika nchi maskini kuweza kumudu bei ya dawa hizo.

Kutokana na jitihada hizo serikali imeweza kuanzisha mpango wa kitaifa wa huduma na matibabu wa mwaka 2003 (National HIV/AIDS Care and Treatment Plan 2003), mpango ambao umeandaliwa kwa pamoja baina ya serikali na CHAI.

Mpango huu unalenga katika kuhakikisha kuwa watu waishio na virusi vya UKIMWI wanapata huduma na dawa bila kujali hali zao za kiuchumi au uwezo.

Mfano wa Juhudi za CHAI za kuhakikisha huduma za afya zinapatikana , ni katika Mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo waathirika wanapata huduma za awali ikiwemo vipimo na dawa katika vituo vya maabara ya kisasa huko huko vijijini, wilayani na Mikoani. Pamoja na dawa, CHAI pia inatoa mafunzo kwa maafisa wa afya wanaotoa huduma.

Leo mchana Bw. Clinton ametembelea kituo cha Afya cha Kitere kilichoko Mtwara Vijijini na kurejea jijini jioni. Bw Clinton ataondoka nchini Kesho kuelekea Afrika Kusini.

Mapema leo asubuhi, Rais pia ameapisha Majaji 10 wa Mahakama, Majaji hao ni Jaji John Harold Utamwa, Jaji Samwel VICTOR Karua, Jaji Beatrice Rodah Mutungi na Jaji Richard Malima Kibela.

Wengine ni Jaji Grace Kalongwe Mwakipesile, Jaji Ama-Isario Ataulwa Munisi, Jaji Agnes Enos Bukuku, Jaji Mwendwa Judith Malecela, Jaji Haruna Twaibu Songoro na Jaji Dkt. Fauz Abdallah Twaib.

No comments:

Post a Comment