Saturday, May 1, 2010

WAKULIMA TUNDURU WALILIA SOKO!!

WAKULIMA wa Halmashauri ya wilaya ya TUNDURU, Mkoa wa RUVUMA, wameiomba serikali wilayani humo kuhakikisha inawafungulia maghulio kwa ajili ya kuuzia mazao yao ili kuepukana na wafanyabiashara matapeli ambao huwanyonya.

Wamesema kumeibuka wimbi kubwa la wafanyabiashara matapeli ambao huzunguka vijijini kuwarubuni wakulima na kisha kuununua mazao yao kwa bei ya chini tofauti na jasho wanalotumia katika kilimo chao.

Wakulima hao wamelazimika kutoa kilio chao hicho kwa mkuu wa mkoa wa RUVUMA , Bi CHRISTINE ISHENGOMA, wakati akiwakabidhi wakulima hao trekta ndogo za kulimia 62 zenye thamani ya zaidi ya milioni 360.

Bi ISHENGOMA amekabidhi trekta hizo kwa wakulima hao tayari kwa shughuli za kilimo ikiwa ni mkakati wa halmashauri hiyo kuondokana na kilimo cha jembe la mkono kutoka asilimia 0.8 sasa hadi kufikia ailimia 15 ifikapo Juni 2011 ili kuongeza tija ya uzalishaji mazao na kukuza kipato chao.

Pamoja na kuwatoa hofu wakulima hao kuondoa mashaka kuhusu uhakika wa kuuza mazao yao , Bi ISHENGOMA amewataka wakulima wilayani humo kuhakikisha wanazitumia trekta hizo katika shughuli za kilimo pekee na siyo kubebea abiria.

Amesema trekta hizo zitasaidia katika kuongeza tija ya uzalishaji mazao na kwamba mkoa huo katika kipindi cha mwaka 2009/2010 imevuna mazao ya chakula na biashara tani 983,883 sawa na asilimia 93.6 ya matarajio ya kuzalisha mazao tani 1,506,520.

Awali kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya TUNDURU, Bi MARY DING’HOI amesema gharama ya trekta moja dukani ni milioni 6.5 lakini halmashauri inamchangia mkulima asilimia 80 na hivyo mkulima anapaswa kuchangia asilimia 20 iluyobakia ambayo ni sawa na sh. milioni 1.3.

Amebainisha kuwa msimu huu wameagiza trekta 64 na kwamba zingine 75 zimeshapata mzabuni wa kuzifikisha hadi Tunduru tayari kwa kugawiwa kwa wakulima. ( Habari kwa Hisani ya Emmanuel Msigwa)

No comments:

Post a Comment