Sunday, May 9, 2010

SHERIA YA WALEMAVU YALILIWA!!!

Mkuu wa Kitengo Cha Walimu wenye ulemavu wa Chama Cha Walimu Tanzania CWT Peter Mlimahadala amemuomba Rais Jakaya Kikwete kusaini haraka sheria ya Walemavu iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni ili ianze kutumika na kuwanusuru walemavu wengi ambao haki zao zinapotea.

Mwalimu Peter Mlimahadala ambaye alikuwa akikabidhi Msaada Baiskeli Mbili za walemavu kwa wanafunzi Wilayani Songea Mkoani Ruvuma pia ametaka Serikali ichukue hatua za haraka kuondoa kodi na kuweka ruzuku kwa vifaa vya walemavu ambavyo kwa sasa havinunuliki kutokana na kuuzwa bei kubwa.

Pamoja na kuomba kusainiwa haraka kwa sheria ya Walemavu ya mwaka 2010, Mlimahadala pia ameomba serikali kutafuta ufumbuzi wa tatizo la vifaa vya walemavu kuuzwa kwa bei ya juu akipendekeza Serikali itoe ruzuku kwa vifaa hivyo.

Aidha Amependkeza Vifaa vya walemavu ambavyo huingizwa hapa nchini kutoka nje ya nchi visitozwe kodi, ili viwafikie walemavu kwa bei nafuu.

Akiwa Mjini Songea Mwalimu Peter Mlimahadala amekabidhi Baiskeli mbili za walemavu zenye thamani ya zaidi shilingi milioni moja zilizotolewa na CWT ambacho ni chama pekee cha wafanyakazi chenye kitengo cha Walemavu. (Habari kwa Hisani ya Gerson Msigwa)

No comments:

Post a Comment