Monday, May 24, 2010

WANANCHI SONGEA WATAKIWA KUCHANGAMKIA NAFASI ZA MASOMO!!!

Askofu mkuu wa Jimbo Katoliki la Songea, Mkoa wa Ruvuma , Mhashamu Norbert Mtega, amewataka wananchi wa mkoa huo kuchangamkia fursa za masomo zinazojitokeza humo.

Askofu Mtega amewataka wazazi kuhakikisha wanakuwa na mwamko wa elimu kwa kuwapeleka watoto wao shule badala ya fedha zao kuishia katika pombe na michango ya harusi.

Askofu Mtega ametoa mwito huo wakati akitoa ekaristi takatifu ya Kipaimara kwa waumini 100 wa kanisa hilo katika kanisa la Mtakatifu Agness lililopo Chipole Songea vijijini.

Amesema kumekuwa na fursa nyingi za masomo zinazojitokeza lakini mwamko wa wananchi wa wana-Ruvuma kujitokeza kwa ajili ya kujiendeleza kimasomo ni mdogo mno.

Ametoa mfano na kusema kuwa Songea imebahatika kupata chuo cha Computer Science cha Mtakatifu Joseph ambacho kinasimamiwa na Mabinti wa Maria Imakulata (DMI) kutoka India lakini watu waliojiunga na chuo hicho wengi wao wanatoka Arusha, Moshi, Mbeya na kwingineko.

Anasema yeye ni Mwenyekiti wa bodi ya shule ya St. Joseph ambayo kwa bahati nzuri inachukua hata wanafunzi wa kidato cha Nne waliopata daraja la Tatu na Nne na kisha kuwaendeleza kwa miezi sita katika somo la Hesabu na Kiingereza ambapo wakifaulu wanaendelea na masomo hadi kupata Diploma na Digrii kwa gharama za serikali. (Habari kwa hisani ya Emmanuel Msingwa)

Amesema katika hali ya kushangaza akiwa Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo ameshuhudia kuona wanafunzi wengi wanaokuja kujiunga na shule hiyo wanatokea katika mikoa mingine bila kuelewa sababu inayochangia hali hiyo.

No comments:

Post a Comment