Tuesday, May 4, 2010

MANUMBA AGEUKIA MASUALA YA MAZINGIRA!!!

Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini, Robert Manumba amesema kwamba udhibiti mkubwa wa kisheria unahitajika kutoka vyombo husika katika kupambana na vitendo vya uharibifu wa mazingira.

Kauli hiyo ilitolewa na Manumba jana wakati akizundua ripoti ya utafiti wa uharibifu wa mazingira Tanzania katika warsha ya siku moja uliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Tunahitaji udhibiti mkubwa wa sheria kutoka vyombo husika mfano polisi Takukuru katika kuhakikisha watu wanaovunja sheria za zinazodhibiti utunzaji wa mazingira kuhakikisha kuwa wanakamatwa na kuhukumiwa, ikiwemo upepelezi na uendeshaji mzuri wa kesi,” alisema Manumba.

Mkurungezi huyo amesema hayo baada ya utafiti huo kubaini kwamba vyombo vya kisheria vina upungufu wa uwezo wa kutambua, kuchunguza na kuendesha kesi zinazohusiana makosa ya mazingira.

Manumba ameongeza sekta zinazohusika kupambana na vitendo vya uharibifu wa mazingira, ambavyo ni vyombo vya kisheria,sekta binafsi na jamii zinapaswa kuweka kipaumbele utamaduni wa uratibu na ushirikiano ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo.

Ameongeza kwamba binadamu wanapaswa kuyalinda mazingira kwa kuwa ndio yanayowafanya waishi.

Akizungumzia kuhusu warsha hiyo ambayo imeshirikisha wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha DarSalaam(USDM),taasisi zisizo za kiserikali , Ushirikiano wa Polisi Duniani Tawi la Nairobi, wizara za mazingira na idara za serikali alisema itasaidia kutoa mapendekezo na mikakati ya udhibiti wa suala hilo.

Naye Dk. Wilson Kipkore kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Usalama,(ISS) alisema utafiti huo umefanyika katika nchi za Tanzania, Kenya,Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan, Ehtiopia na Schely, ambapo kila nchi ina ripoti yake, umebaini kuwa ukuaji wa idadi ya watu ni changamoto kubwa katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Amezitaja changamoto nyingine kuwa ni mabadiliko ya hali ya juu ya teknolojia mfano utumiaji wa machine zenye nguvu kubwa na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na vitendo mbalimbali vya binadamu kama vile uchomaji misitu.

Ameshauri serikali kutoa kuelekeza rasimali za kutosha,ikiwemo rasilimali watu ili kuweza kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Utafiti huo kwa sasa umefanyika kwa muda wa miaka miwili, lakini unatakiwa kukamilishwa kwa kipindi cha miaka mitatu.

No comments:

Post a Comment