Friday, May 21, 2010

CUF WATOA KAULI MAUAJI YA KATIBU CCM MWANZA!!

CUF – Chama cha Wananchi tunawasihi Wagombea na Viongozi wa Vyama vya Siasa vya upinzani kwa ngazi zote kuwa makini juu ya usalama wao kuelekea uchaguzi mkuu ujao kutokana na dalili mbaya ya mauaji ya Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Isamilo mkoani Mwanza, Bahati Stephano yaliyofanyika wiki iliyopita,.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari mauaji hayo yanahusishwa na tetesi za kisiasa na tayari watu wanne wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo wamekamatwa akiwemo Meya wa Jiji la Mwanza ambaye pia ni Diwani wa Kata hiyohiyo ya Isamilo, Bandiho Bihondo (64).

CUF – Chama cha Wananchi tumeshitushwa na mauaji hayo kufanyika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, na hasa ikizingatiwa kuwa aliyeuliwa alikuwa ni kiongozi wa chama cha siasa kilichoko madarakani na wanaotuhumiwa wanahusika kwa njia moja au nyingine ni wanachama wa chama hicho.

CUF – Kutokana na mazingira ya kifo hicho tunazidi kusisitiza na kuwaasa Wagombea na Viongozi wa vyama vya Siasa vya upinzani kwa ngazi zote kuwa macho na maisha yao, na waichukulie kuwa hii ni dalili ya hali ya hatari, kwa wale wagombea wa upinzani wanaokubalika katika maeneo yao, na viongozi waliomstari wa mbele katika ujenzi wa chama kiasi cha kuwa tishio katika maeneo yatakayogombewa hususani kwa wanaotaka kutetea nafasi zao.

CUF – Tunawasihi Wananchi wa Tanzania hususani wapiga kura wote kuwa makini na wagombea ambao wanaona nafasi walizonazo wanahati miliki nazo, kutoa fundisho kwa wagombea hao na chama chao cha CCM ili watambue kuwa nchi hii ni yetu sote na wananchi (wapiga kura) ndio wenye hati miliki ya nani ndie mstahiki wa kuongoza nchi kwa kipindi husika.

No comments:

Post a Comment