Wednesday, May 5, 2010

MADIWANI WAGEUKA MBOGO!!!

Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wameilalamikia kamati ya idara ya mipango miji katika Manispaa hiyo kwa kushindwa kusimamia kazi zake vizuri.

Madiwani hao wametoa lawama hizo huku wakilitaka pia baraza la madiwani wa Manispaa hiyo kutoa tamko rasmi la kumuondoa mkuu wa Idara ya Mipango miji katika manispaa hiyo, Christian Mkude na kumtafuta mtu mwingine wa kushika nafasi hiyo kwa madai kuwa aliyopo sasa anashindwa kufanya kazi yake ipasavyo.

Hatua hiyo imefikiwa jana na Madiwani hao katika baraza lao la madiwani mara baada ya kumtaka Mwenyekiti wa kamati ya idara ya mipango miji, Christian Matembo kutoa maelezo ya kushindwa kusimamia vyema mpango wa ujengaji wa barabara kwa kiwango cha lami unaoendelea kufanyika mjini hapa.

Madiwani hao wamedai kuwa barabara zinazoendelea kujengwa mjini hapa kwa kiwango cha lami zipo katika kiwango duni licha ya kutumika fedha nyingi hali ambayo imepelekea kuwepo kwa malalamiko mengi ya wananchi kuhusu barabara hizo.

Golden Sanga Diwani wa Kata ya Bombambili Mjini ameishia kuishutumu kamati pamoja na idara hiyo ya mipango miji kwa kushindwa kusimamia kazi yake ipasavyo huku akiwatupia lawama moja kwa moja watalaamu kwa madai kuwa kazi wanayoifanya haikidhi mahitaji.

Amesema watalaamu wameshindwa kufanya kazi yao kwa ufanisi hali ambayo imesababisha pia barabara zingine mifereji kujengwa juu na barabara ipo chini hali ambayo inasababisha wakati wa mvua maji kupita juu ya barabara badala ya kwenye mifereji.

Akitoa hoja za kujitetea Mwenyekiti wa Kamati ya Idara ya Mipango Miji, Matembo amedai kuwa wanashindwa kufanya kazi yao vizuri kutokana na Mkuu wa Idara hiyo Bwana Mkude kutoshiriki katika mikutano ya baraza hilo la madiwani hivyo kushindwa kushauriana na kufikia muafaka.

Bwana Matembo amesema kila mkutano unapofika mkuu huyo wa idara ya mipango miji amekuwa akimtuma mwakilishi hivyo akaliomba baraza hilo kutamka rasmi kumtafuta mtu mwingine wa kushika nafasi hiyo.

Awali Mhandisi wa Manispaa ya SONGEA, Maximillian Kabairuka amekiri kuwepo kwa mapungufu katika kusimamia miradi hiyo ya barabara huku akilihakikishia baraza hilo kuwa barabara zinazojengwa ni bora na kwamba zitatumika bila kuharibika kwa muda wa zaidi ya miaka 10 hadi 15.

Akifunga baraza hilo la Madiwani, Meya wa Manispaa ya Songea, Gerald Ndimbo amesema baraza hilo linaagiza kuwa barabara hizo zifanyiwe marekebisho ya haraka hadi ifikapo Juni mwaka huu ili ziwe katika kiwango kinachotakiwa vinginevyo itamyang’anya kazi mkandarasi na kumchukulia hatua zaidi.( Habari kwa Hisani ya Emmanuel Msingwa)

No comments:

Post a Comment