Thursday, February 25, 2010

KATIBU MKUU UWT ATIMULIWA!!!

Umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi Taifa UWT umemfukuza kazi Katibu Mkuu wa Umoja huo Hasna Mwilima kwa madai ya kutoridhishwa na utendaji wa kazi.

Taarifa iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Asha Bakari Makame imesema kuwa kuenguliwa kwa Katibu huyo kunatokana na maamuzi yaliyofikiwa na Baraza kuu la Umoja huo.

Katika maelezo yake ya awali kwa waandishi wa habari Asha Bakari Makame hakuweza kutoa sababu za msingi za maamuzi hayo na badala yake kutoa maelezo ya jumla kuwa UWT imemuondoa katika uongozi na kupitia busara za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti zilitumiika kumwandaa Hasna kupokea maamuzi ya Baraza Kuu ya kuondolewa katika uongozi.

Kuondolewa madarakani kwa Hasna kunafutia fununu za muda mrefu kupitia vyombo vya habari kwamba hali ya mambo ndani ya Jumuiya hiyo si shwari kutokana na kuwepo kwa mvutano wa kiuongozi.

Bi Hasna Sudi Mwilima ni mmoja wa wanawake ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambaye nyota yake ya uongozi ilianza kung’ara katika nyadhifa ya ukuu wa wilaya na aliondolewa kuwa mkuu wa wilaya ya Same na kupewa nafasi kabla ya Baraza Kuu la UWT kuamua kumuondoa katika nafasi ya ukatibu mkuu.

Hasna anakuwa katibu mkuu wa pili wa UWT kutimuliwa katika uongozi akimfuata Katibu Mkuu wa zamani Halima Mamuya ambaye naye aliondolewa katika nafasi hiyo na kwa mantiki hiyo Hasna amepoteza nafasi ya kuwa mbunge wa viti maalum katika bunge jipya lijalo kwani kwa mujibu wa katiba ya UWT Katibu Mkuu ana nafasi ya moja kwa moja kushika nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment