Monday, February 8, 2010

CUF NA KUFELI KWA KINA KAYUMBA!!!

CUF – Chama Cha Wananchi hakikushangazwa na matokeo ya kidato cha nne ya Sekondari za Kata, Mkoani Dar es Salaam kwa kufanya vibaya katika matokeo ya mitihani iliyofanyika mwaka jana.

Haya ni matokeo ya mipango mibovu ya sera ya CCM na Serikali yake ya awamu ya nne ambayo imerejesha tena mfumo wa elimu ya UPE ( Ualimu pasipo Elimu) katika awamu hii ni kwa ngazi ya Sekondari.

Pamoja na wadau wengi kupigia kelele kuhusu madhara ya shule za sekondari za Kata, lakini serikali ya CCM imekaidi na kuzidi kujenga na kudai kuwa ni mchakato, lakini hawajui kuwa wanafunzi hao hawasimami kusoma wanaenda sambamba na shule nyingine zenye ubora wa waalimu na vifaa vya kisasa, watunga mitihani hawajali kuwa shule za kata hazina maabara, maktaba na upungufu wa waalimu waliopata mafunzo ya chap chap ya wiki 3, ambapo waliopewa mafunzo hayo hawakufanya vizuri katika mitihani yao ya kumaliza kidato cha sita.

CUF Chama Cha Wananchi kinatambua kuwa elimu hii ni kiini macho kwa wapiga kura na haya ndio malengo ya Serikali ya CCM ya kujenga matabaka ya watoto wanaokosa elimu bora ambao wengi wao ni watoto wa kimaskini na watoto wanaopata elimu bora ambao wengi wao ni watoto wa vigogo.

CUF Chama Cha wananchi kinaitaka Serikali ya CCM kuacha kuwahadaa watanzania katika Sekta ya elimu ili kutimiza malengo yao ya kupigiwa kura katika chaguzi mbali mbali kwa kuwajengea shule za kata ambazo hazina muelekeo wa kutoa elimu bora kwa Wanafunzi wa watoto wa kimasikini nchini.

No comments:

Post a Comment