Saturday, February 6, 2010

JK AANGAZIA BEI ZA JUU ZA VYAKULA!!!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake inatafakari hatua za kuchukua ili kupunguza bei ya vyakula ambazo zimepanda mno katika miezi ya karibuni katika maeneo ya mijini, na hasa Dar es Salaam.

Amesema kuwa baadhi ya hatua hiyo ni kuona jinsi gani akiba ya chakula kutoka Hifadhi ya Chakula cha Akiba (SGR) kinavyoweza kutumika kuthibiti bei hizo, na hata kuruhusu wafanyabiashara kuingiza chakula nchini kwa masharti nafuu.

Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Ijumaa, Februari 5, 2010, wakati hoja ya bei kubwa za vyakula, na hasa mchele na sembe, ilipoibuliwa mara mbili katika mikutano yake na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu Mkoani Dar es Salaam kukagua uhai wa chama.

Mara ya kwanza hoja ya bei kubwa za mchele na sembe imeibuliwa wakati Rais Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, alipozungumza na viongozi wa chama hicho wa Wilaya ya Temeke katika Ukumbi wa PTA, Barabara ya Kilwa, na mara ya pili wakati alipozungumza na viongozi wa chama hicho wa Wilaya ya Ilala kwenye Ukumbi wa Korean Cultural Centre.

Baada ya kuibuliwa kwa hoja hizo, Rais Kikwete amesema kuwa ni kweli kuwa bei za vyakula, hasa mchele na sembe, ziko juu na akatoa sababu za hali hiyo ambayo pia imechangia kuufanya mfumuko wa bei nchini kuwa juu kuliko ilivyokuwa katika miaka ya karibuni.

“Ni kweli bei za vyakula viko juu na ni bei hizo zilizochangia kuufanya hata mfumuko wa bei kuwa juu. Na ziko sababu mbili za hali hiyo,”amesema Rais Kikwete na kufafanua:

“Sababu ya kwanza ni ya ndani. Mikoa minane nchini ilikumbwa na ukame wa kati ya miaka miwili hadi mitatu, na hivyo kuzuia mikoa hiyo kuzalisha chakula cha kutosha kwa misimu mfululizo,” amesema Rais Kikwete.

Ameitaja baadhi ya mikoa hiyo kuwa ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Morogoro na Dodoma na kusema kuwa katika hali hiyo mikoa hiyo haikuweza kuzalisha chakula na kusababisha upungufu ambao umeilazimisha Serikali kulisha kiasi cha watu milioni 1.8 katika miezi ya karibuni.

Rais kikwete ameitaja sababu ya pili ni ukame mkubwa ambao uliikumba nchi jirani na hivyo kupelekea bei ya vyakula ilipanda kiasi cha kuwafanya wafanyabishara kununua chakula kutoka Tanzania na kukiuza nchi hiyo ya jirani kwa sababu ya bei kubwa zilizokuwa zinapatikana huko.

“Ilifikia kiasi cha mahindi kuanza kuuzwa yakiwa bado machanga mashambani, na mimi nikalazimika kuingia kati kupiga marufuku biashara ya namna hiyo. Kila siku yalikuwa yanakamatwa wastani wa malori 40 mpakani yakitorosha chakula kupeleka nchi hiyo ya jirani,” amefafanua Rais Kikwete na kuongeza kuwa Serikali inatafakari hatua zipi za kuchukua kuhakikisha bei hizo zinapungua.

Hata hivyo, Rais ameongeza kuwa ni matumaini yake kuwa bei za vyakula nchini zitaanza kushuka baada ya mikoa mingi kuanza msimu wa kuvuna kuanzia mwezi ujao wa Machi.

No comments:

Post a Comment