Sunday, February 7, 2010

JK AZURU KILOSA!!!

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametumia siku nzima ya Jumapili, Februari 7, 2010, kutembelea na kuwapa pole wahanga wa mafuriko katika Wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro.

Akifuatana na Mama Salma Kikwete, Mheshimiwa Rais ametembelea kambi za wahanga za Kimamba, Kondoa na Mazulia ambako mbali na kuwapa pole amewahakikishia wahanga hao kuwa wataendelea kupata misaada ya Serikali hadi watakapokuwa wameweza kupata sehemu za kudumu za kuishi.

Katika Kambi ya Kimamba ambako Mheshimiwa Rais ameambatana pia na Mbunge wa Jimbo la Kilosa ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Uchumi, Mheshimiwa Mustafa Mkullo, Rais Kikwete amepokea shukurani kwa Serikali yake kwa misaada ambayo wahanga hao wamekuwa wanapata tokea kuhamishiwa katika mambi hiyo mwanzoni mwa mwaka huu.

Wananchi 230 wanaoishi katika kambi hiyo wamemwambia Rais Kikwete kuwa chakula wanapata, mboga wanapata, maji wanapata isipokuwa kuna uhaba wa vilalio, kwa maana ya magodoro, blanketi na shuka.

Rais Kikwete amewahakikishia kuwa Serikali yake itawapatia vilalio hivyo haraka iwezekanavyo, ili kuepusha uwezekano wa wananchi hao, na hasa watoto, kukumbwa na magonjwa kutokana na kulala chini na kwenye mazingira ya baridi.

Wananchi hao walihamia katika kambi hizo kufuatia mafuriko yaliyotokea usiku wa Desemba 31, mwaka jana, baada ya tuta kwenye Mto Mkondoa kubomoka na kusambaza maji katika mji mdogo wa Kimamba.

Kambi hiyo, kama zilivyo kambi nyingine za wahanga hao, iko kwenye uangalizi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambao wamepewa jukumu maalum na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Kikwete, kusimamia operesheni maalum ya kuokoa maisha ya wananchi walikumbwa na mafuriko hayo, na kusimamia ukarabati wa miundombinu na huduma zilizoharibiwa na mafuriko hayo.

Katika Kambi ya Kondoa, Kata ya Mabwelebwele , Rais Kikwete amewahakikishia wahanga wanaoishi katika kambi hiyo kuwa Serikali itahakikisha inawapatia mashamba ya kulima ili waweze kuzalisha chakula chao.

Rais pia amewaahidi wananchi hao kuwa Serikali itahakikisha kuwa kaya zote 242 zenye watu 948 katika kambi hiyo wanapatiwa magodoro haraka iwezekanavyo.

Wananchi wa kambi hiyo, mbali na kuomba kupatiwa huduma bora zaidi kwa ajili ya watoto wao kuendelea na masomo, pia wameomba maeneo ya kulima na magodoro. Tokea wananchi hao kuhamia katika kambi hiyo, wamepatiwa magodoro 60 tu kwa ajili ya kaya zote hizo.

Kwenye kambi kubwa zaidi ya Mazulia, Rais Kikwete amekagua baadhi ya mahema 540 ambayo yanatumiwa na wananchi wapatao 6, 704 ambao wanahudumiwa katika kambi hiyo na kuwaambia kuwa msisitizo wa sasa wa Serikali ni kutibu majeraha na athari za mafuriko kabla ya kuangalia jinsi gani ya kupata majawabu ya muda mrefu kwa ajili ya maisha ya wananchi hao.

Wengi wa wananchi hao wamehamia katika kambi hiyo kutokea maeneo ya Magomeni, Uhindini, Behewa na katikati ya mji wa Kilosa ambayo yaliathiriwa mno na mafuriko kufuatia kubomoka kwa tuta kwenye mto Mkondoa.

Rais Kikwete amewahakikishia wananchi hao kuwa litajengwa tuta jipya kwenye mto huo, kuwa Serikali itaendelea kuwahudumia kwa malazi, chakula, tiba, maji na huduma za elimu kwa watoto hao, na kuwa hatimaye Serikali itahakikisha kuwa wananchi hao wanapatiwa makazi ya kudumu.

Wananchi hao wameomba kupatiwa maeneo ya kilimo ili wasibweteke na chakula cha misaada cha Serikali, pia wameomba kupatiwa magodoro, vyandarua, mablanketi na shuka.
Rais Kikwete amewahakikisha wananchi hao kuwa maeneo ya kilimo tayari yamepatikana, mbegu za msaada zimepatikana, matrekta ya kumlimia kila mwananchi ekari moja yametikana na kuwa magodoro na vyandarua vitapatikana.

Rais pia ametumia sehemu ya ziara yake ya leo, kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo katika mji wa Kilosa ambao ameshuhudia nyumba nyingi zilibomolewa na soko moja lililoharibiwa kabisa na mafuriko hayo.

No comments:

Post a Comment