Saturday, February 20, 2010

JK AUKWAA UDAKTARI HUKO UTURUKI!!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Ijumaa, Februari 19, 2010, ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Falsafa ya Udaktari katika Masuala ya Kimataifa na Chuo Kikuu cha Fatih cha Istanbul , Uturuki.

Mara baada ya kuwa ametunukiwa shahada hiyo, Rais Kikwete ametangaza kuwa naye anaitunuku shahada hiyo kwa wananchi wa Tanzania ambao wamechangia mafanikio ya utawala wake katika miaka minne iliyopita.

Akizungumza kabla ya kutunuku shahada hiyo, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Sharrif Ali, amesema kuwa uongozi wa chuo hicho kwa ushauri wa Baraza la Seneti la Chuo hicho umeamua kumtunukia Rais Kikwete shahada hiyo kwa sababu ya mchango wake mkubwa katika masuala ya kimataifa.

“Katika nafasi zako zote ulizozishikilia katika maisha yako yote, hasa ulipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ulisimamia kutatua migogoro mingi katika eneo la Maziwa Makuu ukiwamo ule wa Burundi , na zaidi uliposhika urais umeendelea kusuluhisha migogoro mingi,” Profesa Ali amemwambia Rais Kikwete.

Profesa Ali ameongeza kuwa kwa kutoa shahada hiyo ya falsafa kwa Rais Kikwete, Chuo Kikuu cha Fatih kimepata mwakilishi, mtetezi na msemaji wa chuo hicho siyo tu katika Bara la Afrika bali duniani pote.

Rais Kikwete anakuwa mtu wa tatu kutunukiwa shahada ya udaktari na chuo hicho. Wengine ambao wamewahi kutunukiwa shahada ya namna hiyo, tokea kuanzishwa kwa chuo hicho cha sayansi, mwaka 1996, ni Rais wa Azerbaijan , Mheshimiwa Ilham Heydar Aglu Aliyev na Waziri Mkuu wa Uturuki, Mheshimiwa Recep T. Edorgan.

Akizungumza baada ya kuwa ametunukiwa shahada hiyo ya falsafa, Rais Kikwete amesema kuwa naye kwa heshima kubwa anaitunuku shahada hiyo kwa “Watanzania, kwa mke wangu na kwa familia yangu” ambao kwa pamoja wamemsaidia katika kutekeleza majukumu yake.

Katika hotuba yake ya kupokea shahada hiyo, Rais Kikwete ameelezea jinsi Bara la Afrika lilivyobadilika na kuwa Bara bora zaidi katika miaka ya karibuni iwe katika kujenga demokrasia na kujenga mataifa ya Bara hilo .

“Yapo mafanikio mengi yanayojionyesha katika Afrika leo tofauti na ilivyokuwa wakati wa Uhuru miongo mitano iliyopita. Mambo mengi mazuri yametokea katika Afrika yakiwamo kuboreka kwa maisha ya wananchi wa Afrika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Afrika siyo Bara la ovyo ama Bara lililo gizani kama baadhi ya watu wanavyopenda kuliita. Badala yake, Afrika ni Bara lenye kushamiri, lililojaa matumaini, na ambako mambo yanabadilika na kuwa mazuri zaidi. Afrika inapaa kuelekea kwenye mafanikio ya kiuchumi kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. Hii inajionyesha na kujithibitisha katika Bara zima la Afrika – kutoka Cape Town hadi Cairo , kutoka Dakar hadi Dar Es Salaam .”

Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa bado Bara la Afrika linakabiliwa na changamoto nyingi. “Kuna changamoto za kisiasa, kijamii, kiusalama na kiuchumi. Lakini changamoto kubwa zaidi ni ya kiuchumi, hasa katika kuongeza kasi ya kukua kwa chumi za nchi za Afrika na kuwainua Waafrika walio wengi kutoka kwenye umasikini.”

Ameongeza: “Nchi 38 kati ya nchi 49 masikini zaidi kwenye dunia hii wanaishi katika Afrika, na wengi wao wanahemea wakiishi kwa kiasi kisichofikia dola moja ya Marekani (sawa n ash. 1,300) kwa siku.”

Rais Kikwete pia amezungumza hali ya kisiasa ya Afrika, hali ya kiuchumi katika Afrika, umuhimu wa nchi za Kiafrika kuongeza ushirikiano katika masuala ya kiuchumi na uhusiano kati ya Afrika na Uturuki.

Leo usiku, Rais Kikwete na ujumbe wake, ameandaliwa chakula cha jioni na Gavana wa Istanbul na Chama cha Wafanyabiashara wa Uturuki kwenye mgahawa wa Feriye.

No comments:

Post a Comment