Thursday, February 4, 2010

JK ATOA RMBIRAMBI KWA MKUU WA MKOA WA TANGA!!!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Saidi S. Kalembo kutokana na vifo vya watu 25 vilivyotokea tarehe 02 Februari, 2010.

Katika ajali hiyo, basi kubwa la abiria la Kampuni ya Chatco liligongana uso kwa uso na basi lingine dogo liitwalo Nzuri. Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Kitumbi Kwamgolo, Wilayani Handeni katika Mkoa wa Tanga kwenye Barabara Kuu ya Chalinze – Segera. Ajali ya basi la Chatco na Nzuri imesababisha watu wengine 53 kujeruhiwa.

“Kwa dhati za moyo wangu, kupitia kwako wewe Mkuu wa Mkoa, natuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu wote waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo. Ninamuomba Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aziweke mahali pema peponi roho za marehemu wote”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake.

Rais Kikwete pia amewataka wafiwa wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya wapendwa wao. Amewatakia nafuu na kupona haraka watu wote waliojeruhiwa katika ajali hiyo, ili waweze tena kurejea katika hali zao za kawaida na kuungana na ndugu na jamaa zao katika ujenzi wa Taifa.

Pamoja na salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete amewataka viongozi katika ngazi zote kuanzia Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Viongozi wengine katika ngazi za chini, kuchukua hatua za makusudi na kuweka malengo mahsusi ya kupunguza au kuondoa kabisa ajali za barabarani na kuyafanyia tathmini malengo hayo, ili mwenendo wa matukio ya ajali za barabarani ubadilike kabisa katika mwaka huu mpya wa 2010.

“Sote tunaelewa jinsi ajali za barabarani zinavyoligharimu Taifa letu. Watu wetu wengi ambao ni rasilimali na nguvu kazi muhimu katika ujenzi wa nchi yetu wamekuwa wakipoteza maisha. Wengi wa watu wetu pia wamekuwa wanapata ulemavu wa kudumu na hivyo kuzorotesha au kuwaondolea uwezo wao wa kuendelea na uzalishaji. Hivyo ni vema mwaka huu 2010 tuonyeshe mabadiliko katika kukabiliana na ajali za barabarani”, amemalizia salamu zake Rais Kikwete.

No comments:

Post a Comment