Sunday, February 7, 2010

JK ZIARANI MOROGORO!!!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Morogoro kuhakikisha kuwa waathirika wa mafuriko katika Wilaya ya Kilosa wanaishi maisha ya kawaida kwa kadri inavyowezekana katika kambi zao za muda.

Aidha, Rais Kikwete ameuagiza Mkoa huo kuandaa mpango wa muda mrefu wa jinsi ya kuwarudisha wananchi hao katika maisha yao ya zamani kabla ya kuathiriwa na mafuriko.

Rais Kikwete ametoa maagizo hayo leo, Jumamosi, Februari 6, 2010, wakati alipopewa taarifa na uongozi wa mkoa huo kuhusu mafuriko hayo yaliyotokea mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu katika Wilaya ya Kilosa kufuatia mvua kubwa zilizonyesha Wilayani Mpwapwa katika mkoa jirani wa Dodoma.

Mafuriko hayo yalisababisha kubomoka kwa tuta la kuthibiti maji kwenye Mto Mkondoa, ambao unapita katikati ya Mji wa Kilosa na kusababisha maji kusambaa katika makazi ya watu kwenye eneo linalokadiriwa kufikia kilomita za mraba 541.

Rais Kikwete amewasili mjini Morogoro jioni ya leo kwa ziara ya siku mbili mkoani humo, ambako shughuli yake kuu itakuwa kutembelea na kuona uharibifu uliofanywa na mafuriko hayo pamoja na kuwapa pole wananchi walioathiriwa na mafuriko hayo.

Kiasi cha watu 25,803 ambazo ni kaya 6, 168 waliathiriwa na mafuriko hayo lakini waliokuwa kambini hadi leo ni watu 9,620 ambao ni kaya 2,464 baada ya wengine kupata hifadhi kwa ndugu, jamaa na kupanga nyumba katika maeneo ya miinuko.

Waathirika hao wanaendelea kuhudumiwa na Serikali kwa kila mahitaji ya maisha yao.

Baada ya kuwa ameambiwa hali ilivyo katika makambi hayo, Rais Kikwete ameuuliza uongozi wa Mkoa wa Morogoro: “Tunawafanyia nini watu hawa? Tunawahudumia vipi watu hawa? Je tunafanya vya kutosha ili kuwahudumia vizuri watu hawa? Tunafanya nini na miundombinu? Tunafanya nini na reli yetu kwa sababu uchumi wetu hauwezi kuhimili usafiri wa reli kusimama kwa muda mrefu?

Rais Kikwete ameongeza: “Mimi nataka tuelekeze nguvu zetu zote kwa watu walioathirika na hasa wale wanaoishi makambini. Nataka tuwashughulikie na kuhakikisha wanaishi maisha ya kawaida kabisa ya kifamilia. Waishi vizuri, wale vizuri, walale vizuri, wapate maji salama, wapate tiba ya uhakika. Tuhakikishe watoto wao wanakwenda shule vizuri bila masomo yao kuathirika.”

Rais Kikwete amesisitiza: “Baada ya kuwaweka vizuri basi tuwe na mpango wa muda mrefu wa kuhakikisha kuwa tunawasaidia kuwarudisha katika maisha ya kawaida, yaani kuwawezesha kuishi kama walivyokuwa wanaishi kabla ya kuathiriwa na mafuriko. Nitahakikisha kuwa taasisi zote za serikali zinazohusika zinashiriki katika kuandaa mpango huo.”

Mji wa Kilosa ulikabiliwa na mafuriko kwa mara ya kwanza katika bonde la Mto Mkondoa katika miaka ya 1940 wakati wa utawala wa kikoloni, na mwaka 1948 mto huo ulijengewa kingo (dykes) ili kuzuia. Mwaka 1964 yalitokea mafuriko mengine makubwa mjini Kilosa baada ya kingo za mto huo kubomoka na ndipo lilipojengwa tuta lilikomoboka majuzi.

No comments:

Post a Comment