Saturday, February 27, 2010

DARAJA LAVUNJWA!!!


Matajiri wa Jiji la Manchester, Klabu ya Manchester City wamefanikiwa kuvunja daraja baada ya kuipa kichapo Chelsea cha magoli 4-2. Mchezo huo uliopigwa katika dimba la Stamford Bridge ulitawaliwa na upinzani mkali lakini cha kufurahisha kila mchezaji aliyefunga ameondoka na magoli mawili. Poleni Wazee wa Darajani ndiyo Ukubwa huo!!!

Thursday, February 25, 2010

EVERTON YACHAPWA, FULHAM, LIVERPOOL ZATAMBA!!!






Mshike mshike wa Ligi ya Europa umeendelea na kushuhudia Everton akiondoshwa katika mashindano baada ya kufungwa magoli 3-0 na Sporting Lisbon. Fulham imefuzu baada ya kutoka sare ya goli 1-1 dhidi ya Shakhtar Donestk wakati ambapo Liverpool ikitoa onyo kwa Unirea kwa kuifunga magoli 3-1

MAKAMU WA RAIS NIGERIA KUENDELEA KUPETA!!!!


Serekali ya Nigeria kupitia kwa Waziri wake wa Habari Dora Akunyili imesema Makamu wa Rais wa nchi hiyo Jonathan Goodluck ataendelea kushika wadhifa wa Kukaimu nafasi ya Urais

BRIDGE ATUNDIKA DARUGA SOKA YA KIMATAIFA!!!


Beki wa Kimatifa wa England na Klabu ya Manchester City Wayne Bridge ametangaza kutundika daruga katika soka la Kimataifa. Bridge kupitia kwa mwanasheria wake ametangaza kustaafu soka ya kimataifa na kuweka bayana anaona nafasi yake ni finyu katika kikosi cha England. Wafuatiliaji wa mambo wanasema hatua hiyo yawezekana imechangiwa na hatua ya John Terry kutembea na mchumba wake.

MKUTANO WA MAAFISA WAKUU WA JESHI LA POLISI WAFUNGWA!!!

Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha linadhibiti mapema wimbi la uhalifu na kuimarisha nidhamu kwa askari kuondokana na vitendo vya rushwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Mbarak Abdulwakili ametoa rai hiyo wakati akifunga mkutano wa Maafisa Wakuu wa Jeshi la Polisi uliokuwa ukifanyika kwenye ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa, Mjini Dodoma.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali Saidi Mwema, amesema mkutano huo ambao ulikuwa ukiwashirikisha Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi, umejadili na kuweka mikakati ya kukabiliana na uhalifu ukiwemo wa vitendo vya kudai na kupokea rushwa.

Akizungumzia matarajio ya taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu, IGP Mwema amewaondolea hofu wananchi kuwa jeshi la polisi litahakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki.

Katika maazimio yao makamanda hao wamesema kuwa, watatoa elimu kwa wamiliki binafsi wa Mbwa na Farasi ili watumike kama walinzi wasaidizi.

JK AWASHUKIA VIONGOZI WA TAKUKURU!!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kujipanga kwa kazi ya kupambana na wanunuaji wa uongozi kwa kutumia sheria mpya ya matumizi ya fedha katika uchaguzi.

Rais pia amezitaka Wizara za Serikali, Idara na Mashirika ya Umma kuhakikisha kuwa zinatekeleza ipasavyo Mkakati wa Taifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (NACSAP) akisisitiza kuwa kama hilo likifanyika Tanzania itapata mafanikio makubwa katika kuzuia na kupambana na rushwa.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa dhamira yake ni kuhakikisha kuwa wakati anamaliza muda wake wa uongozi itakuwa imejengeka misingi imara ya utawala bora na maadili ya viongozi wa umma yenye kujikita katika sheria za nchi na baadaye kuwa utamaduni wa kudumu wa kuendesha shughuli za siasa nchini.

Rais Kikwete alikuwa anafungua Mkutano wa Mwaka wa TAKUKURU kwenye Chuo cha Benki Kuu (BOT) mjini Mwanza, leo, Alhamisi, Februari 25, 2010.

“Sheria hii inatuweka mahali pazuri kuanza mapambano na watu wanaotaka kupata uongozi kwa nguvu ya pesa. Pia inasaidia kuwabana watu wanaogeuza haki yao ya kupiga kura kuwa ni mradi au bidhaa ya kunufaika nayo kipesa kwa kuiuza,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Ole wao wahongaji, ole wao wahongwaji na ole wao wanaoomba kuhongwa.”

Rais Kikwete amesema kuwa TAKUKURU ndiyo inatazamiwa kufanya kazi ya kukazia utekelezaji wa sheria hiyo mpya. “Napenda kuwahakikishieni wana-TAKUKURU kwamba nitafanya kila liwekekanalo kuwawezesha ili muweze kufanikisha kazi ya kudhibiti rushwa katika chaguzi zetu nchini. Nataka tuanze na uchaguzu huu (wa mwaka huu)”

Kuhusu wizara, idara na mashirika ya umma kupambana na rushwa, Rais Kikwete amesema: “Swali ambalo sote hatuna budi kujiuliza na kuulizana ni je, mipango ya kila Wizara, Idara ya Serikali na Mashirika ya Umma iko wapi na kama kweli inazingatiwa na kutekelezwa. Mimi sina hakika, sijui nyie wenzangu. Naona mmerudia sifa yetu ya kuwa nguvu ya soda.”

“Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara za Serikali na Mashirika ya Umma kuhusu wajibu wao katika kuhakikisha kuwa Mkakati wa Taifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika maeneo yao ya uongozi uko hai na unatekelezwa kama ilivyokusudiwa.”

Rais Kikwete pia amesema kuwa kansa ya rushwa haiko katika sekta ya umma bali vile vile iko katika sekta binafsi.

“Naomba pia, hata sekta binafsi wahusishwe kwani hata na wao wanahusika katika vitendo vya rushwa. Wapo maofisa na watendaji katika makampuni binafsi wanaojihusisha na vitendo vya kutoa, kudai, na kupokea rushwa. Wanafanya hivyo katika ajira, kutafuta masoko na kutafuta zabuni. Bahati mbaya sana hata waandishi wa habari nao hawako salama katika kadhia hii. Hivyo, rushwa iko kila mahali, sote tuhusike na kuhusishwa katika mapambano hayo.”

Rais Kikwete ameisifu TAKUKURU kwa kazi nzuri katika kupambana na rushwa na kusisitiza kuwa la msingi ni kwamba taasisi hiyo isimwonee haya mtu ambaye ni mhalifu lakini vile vile isimwonee mtu ambaye hana makosa. “Tendeni haki kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni. Matunda ya kazi yetu yataonekana.”

KATIBU MKUU UWT ATIMULIWA!!!

Umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi Taifa UWT umemfukuza kazi Katibu Mkuu wa Umoja huo Hasna Mwilima kwa madai ya kutoridhishwa na utendaji wa kazi.

Taarifa iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Asha Bakari Makame imesema kuwa kuenguliwa kwa Katibu huyo kunatokana na maamuzi yaliyofikiwa na Baraza kuu la Umoja huo.

Katika maelezo yake ya awali kwa waandishi wa habari Asha Bakari Makame hakuweza kutoa sababu za msingi za maamuzi hayo na badala yake kutoa maelezo ya jumla kuwa UWT imemuondoa katika uongozi na kupitia busara za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti zilitumiika kumwandaa Hasna kupokea maamuzi ya Baraza Kuu ya kuondolewa katika uongozi.

Kuondolewa madarakani kwa Hasna kunafutia fununu za muda mrefu kupitia vyombo vya habari kwamba hali ya mambo ndani ya Jumuiya hiyo si shwari kutokana na kuwepo kwa mvutano wa kiuongozi.

Bi Hasna Sudi Mwilima ni mmoja wa wanawake ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambaye nyota yake ya uongozi ilianza kung’ara katika nyadhifa ya ukuu wa wilaya na aliondolewa kuwa mkuu wa wilaya ya Same na kupewa nafasi kabla ya Baraza Kuu la UWT kuamua kumuondoa katika nafasi ya ukatibu mkuu.

Hasna anakuwa katibu mkuu wa pili wa UWT kutimuliwa katika uongozi akimfuata Katibu Mkuu wa zamani Halima Mamuya ambaye naye aliondolewa katika nafasi hiyo na kwa mantiki hiyo Hasna amepoteza nafasi ya kuwa mbunge wa viti maalum katika bunge jipya lijalo kwani kwa mujibu wa katiba ya UWT Katibu Mkuu ana nafasi ya moja kwa moja kushika nafasi hiyo.

ANDERSON WA MAN UTD NJE MSIMU MZIMA!!!



Kiungo wa Kimatifa wa Brazil ambaye anakipiga katika Klabu ya Manchester United Anderson anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi chote cha msimu kilichosalia kutokana na maumivu ya mguu aliyoyapata. Kocha wa Man Utd Sir Alex Ferguson amesema maumivu aliyoyapata Anderson katika mchezo dhidi ya West Ham United ni makubwa na inawezekana akakosa Mchuano wa Kombe la Dunia baadaye mwaka huu.

Wednesday, February 24, 2010

WABONGO WAKISAKA RIZIKI!!








Hawa ni vijana wa Kitanzania ambao wanasaka riziki yao ya kila siku na kuwa na matumaini siku moja watafurahia maisha bora ambayo yaliahidiwa na Mkuu wa nchi! Hapa kila mmoja anaumiza kichwa kuhakikisha mambo yake yanamnyookea licha ya vizingiti wanavyovikumbana navyo!!

MADAI YA PENSHENI KWA WAZEE WA MBINGA!!!

Wazee wa Wilaya ya MBINGA Mkoani RUVUMA wameanza harakati za kuishinikiza serikali kutoa Pensheni kwa wazee wote wa Tanzania bila kujali kama waliajiriwa katika sekta ya umma ama hawakuajiriwa.

Katika harakati hizo wazee hao wameunda kikundi kazi ambacho kitawatembelea wazee wote wa wilaya hiyo, na baadaye kuunda Mtandao wa Mkoa Mzima wa RUVUMA ambao pamoja na kuwaunganisha wazee wote, utatoa shinikizo kwa serikali ili wazee wote wapate Pensheni.

Akizungumza na Baadaya ya warsha ya siku mbili iliyofanyika katika wilaya ya MBINGA Mkoani RUVUMA, Meneja miradi wa shirika la Help Age International Bw SMART DANIEL amesema pensheni ni haki ya msingi ya kila mzee, ambaye amelitumikia taifa la Tanzania bila kujali kama ameajiriwa ama hajaajiriwa.

Amesema zaidi ya wazee milioni waliopo hapa nchini ni asilimia 4 ndio wanaopata Pensheni, huku wengine wote wakitapatapa kwa maisha ya taabu na fedheha kutokana na kukosa kipato.

Nae Mzee Maarufu wa Mkoani RUVUMA Mzee MUSTAFA SONGAMBELE amesema Serikali ikitekeleza mpango huo wa kutoa Pensheni kwa wazee wote wa Tanzania itakuwa imewasaidia watoto na wajukuu wao, yakiwemo makundi maalumu kama vile watoto yatima ambao tafiti zimeonesha kwa asilimia 50 wanalelewa na wazee.(Habari kwa hisani ya Gerson Msigwa)

INTER MILAN YAIUA CHELSEA SAN SIRO!!!









Michezo ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya imeendelea na kushuhudia Inter Milan ambayo inanolewa na Jose Mourinho ikivuna ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya timu yake ya zamani Chelsea. Katika mchezo huo magoli ya Inter Milan yamefungwa na Diego Milito na Estabian Cambiasso wakati lile la Chelsea limefungwa na Solomon Kalou! Cha kufurahisha Mourinho hakuthubutu kushangilia hata goli moja na sasa marejeano ni majuma matatu yajayo katika Dimba la Stamford Bridge!!

MANCHESTER UNITED YATAMBA!!!








Manchester United ikiiadhibu West Ham United katika mchezo wa Ligi. Mashetani hao Wekundu wamefanikiwa kuwachabanga vilivyo Wagonga Nyundo wa Jiji la London kwa magoli 3-1!!!

MICHEZO YA CHAMPIONS LEAGUE KATIKA PICTURE!!





Mshike mshike wa Michezo ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya ambayo inaendelea wiki hii. Kitimu timu hicho kilianza juma lililopita.

RAIS YAR'ADUA AREJEA NYUMBANI!!!


Rais wa Nigeria Umar Yar'Adua amerejea nyumbani baada ya kuwa nchini Saudi Arabia kwa matibabu yaliyodumu kwa kipindi cha miezi mitatu!! Hakuna taarifa zaidi iwapo Rais huyo ataendelea na majukumu yake ya kikazi au la!!!

Monday, February 22, 2010

KIPAWA HIVI SASA KWEUPE!!!




Kama ndiyo mara yako ya kwanza kukanyaga katika Jiji hili na ukaletwa katika sehemu ya Kipawa huwezi ukaamini ukiambiwa kama hapa palijaa majumba. Lakini kwa sasa eneo hili lote ni jeupe kabisa baada ya serikali kuvunja kupisha upanuzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere. Maendeleo huwa yanakuja na athari zake!!!!

Sunday, February 21, 2010

MAN UTD YACHAPWA HUKU SIR FERGUSON AKITETEA UCHOVU NDIYO CHANZO!!!







Kocha Mkuu wa Manchester United Sir Alex Ferguson ametetea kichapo alichokipata kutoka kwa Everton kimechangiwa na wachezaji wake kuchoka. Lakini amesema ana imani watafanya vizuri kwenye mchezo wao dhidi ya West Ham United.

Matokeo mengine ya Ligi hiyo ni kama ifuatavyo:
Barclays Premier League
Arsenal 2-0 Sunderland
Everton 3-1 Man Utd
Portsmouth 1-2 Stoke
West Ham 3-0 Hull
Wolverhampton 0-2 Chelsea

Saturday, February 20, 2010

JK AUKWAA UDAKTARI HUKO UTURUKI!!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Ijumaa, Februari 19, 2010, ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Falsafa ya Udaktari katika Masuala ya Kimataifa na Chuo Kikuu cha Fatih cha Istanbul , Uturuki.

Mara baada ya kuwa ametunukiwa shahada hiyo, Rais Kikwete ametangaza kuwa naye anaitunuku shahada hiyo kwa wananchi wa Tanzania ambao wamechangia mafanikio ya utawala wake katika miaka minne iliyopita.

Akizungumza kabla ya kutunuku shahada hiyo, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Sharrif Ali, amesema kuwa uongozi wa chuo hicho kwa ushauri wa Baraza la Seneti la Chuo hicho umeamua kumtunukia Rais Kikwete shahada hiyo kwa sababu ya mchango wake mkubwa katika masuala ya kimataifa.

“Katika nafasi zako zote ulizozishikilia katika maisha yako yote, hasa ulipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ulisimamia kutatua migogoro mingi katika eneo la Maziwa Makuu ukiwamo ule wa Burundi , na zaidi uliposhika urais umeendelea kusuluhisha migogoro mingi,” Profesa Ali amemwambia Rais Kikwete.

Profesa Ali ameongeza kuwa kwa kutoa shahada hiyo ya falsafa kwa Rais Kikwete, Chuo Kikuu cha Fatih kimepata mwakilishi, mtetezi na msemaji wa chuo hicho siyo tu katika Bara la Afrika bali duniani pote.

Rais Kikwete anakuwa mtu wa tatu kutunukiwa shahada ya udaktari na chuo hicho. Wengine ambao wamewahi kutunukiwa shahada ya namna hiyo, tokea kuanzishwa kwa chuo hicho cha sayansi, mwaka 1996, ni Rais wa Azerbaijan , Mheshimiwa Ilham Heydar Aglu Aliyev na Waziri Mkuu wa Uturuki, Mheshimiwa Recep T. Edorgan.

Akizungumza baada ya kuwa ametunukiwa shahada hiyo ya falsafa, Rais Kikwete amesema kuwa naye kwa heshima kubwa anaitunuku shahada hiyo kwa “Watanzania, kwa mke wangu na kwa familia yangu” ambao kwa pamoja wamemsaidia katika kutekeleza majukumu yake.

Katika hotuba yake ya kupokea shahada hiyo, Rais Kikwete ameelezea jinsi Bara la Afrika lilivyobadilika na kuwa Bara bora zaidi katika miaka ya karibuni iwe katika kujenga demokrasia na kujenga mataifa ya Bara hilo .

“Yapo mafanikio mengi yanayojionyesha katika Afrika leo tofauti na ilivyokuwa wakati wa Uhuru miongo mitano iliyopita. Mambo mengi mazuri yametokea katika Afrika yakiwamo kuboreka kwa maisha ya wananchi wa Afrika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Afrika siyo Bara la ovyo ama Bara lililo gizani kama baadhi ya watu wanavyopenda kuliita. Badala yake, Afrika ni Bara lenye kushamiri, lililojaa matumaini, na ambako mambo yanabadilika na kuwa mazuri zaidi. Afrika inapaa kuelekea kwenye mafanikio ya kiuchumi kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. Hii inajionyesha na kujithibitisha katika Bara zima la Afrika – kutoka Cape Town hadi Cairo , kutoka Dakar hadi Dar Es Salaam .”

Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa bado Bara la Afrika linakabiliwa na changamoto nyingi. “Kuna changamoto za kisiasa, kijamii, kiusalama na kiuchumi. Lakini changamoto kubwa zaidi ni ya kiuchumi, hasa katika kuongeza kasi ya kukua kwa chumi za nchi za Afrika na kuwainua Waafrika walio wengi kutoka kwenye umasikini.”

Ameongeza: “Nchi 38 kati ya nchi 49 masikini zaidi kwenye dunia hii wanaishi katika Afrika, na wengi wao wanahemea wakiishi kwa kiasi kisichofikia dola moja ya Marekani (sawa n ash. 1,300) kwa siku.”

Rais Kikwete pia amezungumza hali ya kisiasa ya Afrika, hali ya kiuchumi katika Afrika, umuhimu wa nchi za Kiafrika kuongeza ushirikiano katika masuala ya kiuchumi na uhusiano kati ya Afrika na Uturuki.

Leo usiku, Rais Kikwete na ujumbe wake, ameandaliwa chakula cha jioni na Gavana wa Istanbul na Chama cha Wafanyabiashara wa Uturuki kwenye mgahawa wa Feriye.

Friday, February 19, 2010

KILIMO CHA MPUNGA MOSHI!!!







Mashamba haya ukiyaangalia unaweza kuhisi ni Mbeya au Shinyanga lakini hapana. Hapa ni Moshi ambapo kilimo cha mpunga kimechukua mashiko kwa kiasi kikubwa. Mradi huu ambao unasaidiwa kwa kiasi kikubwa na serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Japan (JICA)!!