Saturday, July 3, 2010

MKUU WA WILAYA YA MBINGA ATAKA WANAWAKE WAWE WAKALI KWA WAUME ZAO!!!

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Kanali mstaafu Edmund Mjengwa amewataka wanawake wilayani humo kuwa wakali kwa waume zao katika kipindi cha mavuno na mauzo ya Kahawa kwa madai kuwa wengi wao wamekuwa wakithubutu kuongeza wanawake baada ya mauzo ya Kahawa.

Akiongea na wananchi wa kijiji cha Tingi, wilayani hiyo Mjengwa amesema katika wilaya hiyo wanawake ndiyo wanaoonekana kujituma zaidi katika kazi za shambani hususani katika kilimo cha zao la Kahawa lakini wanaume hujitokeza nyakati za mavuno na mauzo pekee.

Amesema tabia hiyo ya wanaume kujitokeza na kujifanya wao ndiyo wapangaji wakubwa wa mauzo nyakati hizo kumekuwa kukisababisha familia zao kuendelea kuishi maisha duni kutokana na wengi wao kutumia fedha zote za mauzo ya Kahawa kwa kuongeza wanawake na kupenda anasa zilizokithiri.

Kanali Mjengwa amesema endapo wanawake hao wakiwa wakali kwa wanaume zao juu ya suala hilo litasaidia pia katika kupunguza maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa UKIMWI katika wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na kuzifanya familia zao kuwa na maisha bora zaidi.

Ameeleza kuwa tabia hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuleta msukumo mkubwa kwa baadhi ya wanawake wenye tabia ya kuuza miili yao kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini kuja katika wilaya hiyo kuvuna fedha kwa wanaume wapenda anasa.

Baadhi ya wananchi waliiomba serikali kuwachukulia hatua kali watu wote watakaobainika kufanya hivyo kwa madai kuwa licha ya kuingilia uhuru wao binafsi lakini unawanyanyasa wanawake na watoto wasio na hatia kukosa haki zao za msingi ikiwemo kupata matibabu bora na elimu. (Habari na Emmanuel Msigwa)

No comments:

Post a Comment