Monday, July 12, 2010

JUMUIYA YA WAZAZI SONGEA YALIVALIA NJUGA SUALA LA MIMBA!!!

JUMUIYA ya wazazi nchini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), imejipanga kufufua jumuiya hiyo inayodaiwa kuanza kufa kwa kuhakikisha kuwa inajenga mabweni ya wanafunzi katika shule zote za sekondari za kata ili kutokomeza mimba kwa watoto wa kike.

Aidha, Jumuiya hiyo imejipanga kuzunguka nchi nzima kuelezea na kuweka wazi shughuli zake kwa wananchi ili waitambue na kuweza kujiunga kwa wingi zaidi ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanachama.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Taifa, Bw. Athumani Mhina wakati alipokuwa akizungumza na wajumbe wa kamati maalumu ya wazazi mkoani Ruvuma pamoja na wananchi wa kata ya Lizaboni mjini Songea.

Amesema kasi ya wanafunzi kupata ujauzito Tanzania kwa sasa ni kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma hali ambayo inatishia kuwa na kizazi kisicho na elimu na kwamba wazazi wenyewe ndiyo wenye jukumu la kwanza kutokomeza hali hiyo kwa kujenga mabweni ya wanafunzi hao katika shule zote za kata.

Ameeleza kuwa kitendo kuwaachia watoto hao kutembea umbali mrefu kwenda shule kila siku ni kuwapa nafasi kubwa mafataki kuwaingiza katika vishawishi mbalimbali na hatimaye kuwajaza mimba na kisha kuwatelekeza na kuwaacha wakihangaika peke yao.

Mhina pia ameoneshwa kusikitishwa na baadhi ya tabia ya wazazi ambao wameshindwa kuheshimu watoto wa wenzao na kuamua kufanya nao mapenzi na kuwaingiza katika matatizo makubwa badala ya wao kuwa walimu na walinzi wa watoto hao.

Mbali na hayo, pia Mhina amewaomba wazazi nchini kuhakikisha ujenzi wa mabweni hayo ya wanafunzi yaende sambamba na ujenzi wa nyumba za walimu ili kuwafanya walimu hao kudumu na kuipenda kazi yao.

Amesema walimu wengi wanashindwa kufanya kazi yao na kulazimika kuacha kazi hiyo ama kuhamia maeneo mengine yenye unafuu kutokana na kufanya kazi katika mazingira mabovu yasiyovumilika. (Habari kwa hisani ya Emmanuel Msigwa)

No comments:

Post a Comment