Monday, February 13, 2012

WOLVES IMEMTIMUA KAZI KOCHA WAKE KUTOKANA NA KUPATA MATOKEO MABAYA!!!


Klabu ya Wolvehampton Wanderers ya nchini Uingereza imesitisha mkataba wake na Kocha aliyekuwa anakinoa kikosi hicho Mick McCarthy kutokana na timu hiyo kupata matokeo mabaya na hivyo kujiweka kwenye hatari ya kuweza kushuka daraja!!! Wolves imeshinda mchezo mmoja pekee kwenye michezo kumi na tatu iliyocheza na hivyo dhahiri imeanza kujichimia shimo la kushuka daraja msimu huu!!!

ZAMBIA MABINGWA WA AFRIKA WAICHAKAZA IVORY COAST!!!








Timu ya Taifa ya Zambia maarufu kama Chipolopolo imefanikiwa kutwa Ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kufanikiwa kuifunga Ivory Coast kwa mikwaju ya penalty 8-7!! Mchezo huo ulipigwa dakika 120 lakini hakuna timu ambayo iliweza kupata goli ndipo mikwaju ya penalty ikalazimika kutumika. Kolo Toure na Gervihno ndiyo walikosa penalty za Ivory Coast wakati kwa Zambia Kabala ndiye alikosa mkwaju huo. Stoppila Sunzu alifunga penalty na mwisho na kuwapa ushindi Chipolipolo!!!

Thursday, February 9, 2012

ZAMBIA NA IVORY COAST USO KWA USO FAINALI AFCON!!!



Timu ya Taifa Zambia maarufu kama Chipolopolo inatarajiwa kupambana na Ivory Coast maarufu kama Tembo baada ya timu hizo kushinda michezo yake ya Nusu Fainali!! Zambia walifanikiwa kuiondosha Ghana maarufu kama Black Stars kwa goli moja kwa nunge goli la kwake Emmanuel Mayuka!! Ivory Coast wakawaondosha Mali maarufu kama Eagles kwa goli moja la kwake Gervais Yao Kouassi Gervinho!!! Mchezo wa kusaka nafasi ya Mshindi wa Tatu ni kati ya Mali dhidi ya Ghana siku ya jumamosi!! Fainali itapigwa siku ya jumapili!!!

FABIO CAPELLO AACHIA NGAZI UKOCHA WA ENGLAND!!!


Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Uingereza Fabio Capello ametangaza kujiuzlu wadhifa wake baada ya kufanya mazungumzo na Viongozi wa Chama Cha Soka nchini humo FA baada ya kupinga hatua na Nahodha John Terry kunyang'anywa unahodha!! Capello alionekana kuchukizwa na hatua hiyo na kutoa maneno ambayo yaliikera FA na sasa Harry Redknapp anatajwa huenda akachukua jukumu hilo!! Terry alinyang'anywa Unahodha baada ya kutoa maneno ya kibaguzi dhidi ya Anton Ferdinand na kumfanya afunguliwe kesi kitu kilichowafanya FA kumpora wadhifa huo!!!

WAZIRI MKUU PINDA AKUTANA NA MADAKTARI KUWASIHI WAMALIZE MGOMO!!!


Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda anaendelea kukutana na Uongozi wa Hospital ya taifa ya Muhimbili pamoja na Madaktari Bingwa kutoka Sekta ya Umma, Binafsi na Wastaafu ili kumaliza mgomo wa madakatari uliodumu kwa zaidi ya majuma mawili.

Mkutano huo ulianza saa tatu asubuhi ambapo pia Waziri Mkuu atakutana na Madaktari Bingwa, madaktari Waliosajili na Madaktari Waliopo Kwenye Mafunzo kwa Vitendokabla ya kukutana na Wafanyakazi wa Hispotali ya Muhimbili, Moi, Ocean Road na Wawikilishi kutoka Hospital za Mkowa wa Dar Es Salaam.

WANAHARAKATI WAFUNGA BARABARA WAKISHINIKIZA SERIKALI KUMALIZA MGOMO WA MADAKTARI!!!





Wanaharakati Jijini Dar Es Aalaam wakiwa wamepiga kambi katika Barabara ya Ally Hassan Mwinyi wakishinikiza serikali kuzungumza na Madaktari ambao wapo kwenye mgomo uliodumu kwa zaidi ya majuma mawili sasa huku wagonjwa wakiendelea kupoteza maisha!! Wanaharakati hao wametaka hilo lifanyike mara moja ili kunusuru maisha ya wagonjwa!!!

Tuesday, January 31, 2012

MICHEZO YA KUNDI C KUMALIZIKA LEO!!!


Michezo ya Kundi C ya kumalizia ratiba itapigwa leo wakati huu ambapo wenyeji Gabon na Tunisia wakiwa wameshafuzu katika Robo Fainali!! Ratiba ya Mchezo ya Kundi C ni kama ifuatavyo:
Gabon v Tunisia, Franceville
Niger v Morocco, Libreville

IKULU YAKANUSHA RAIS KIKWETE KUBARIKI POSHO MPYA ZA WABUNGE!!!

Gazeti la Mwananchi la leo, Jumanne, Januari 31, 2012 limeandika habari zenye kichwa cha habari – JK abariki posho mpya za Wabunge: Kila mmoja kulipwa sh 330,000 kwa siku.



Habari hizi siyo za kweli na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais inataka kutoa ufafanuzi ufuatao:



Maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuhusu suala hili yako wazi kabisa na hakuna mahali ambako Rais Kikwete amebariki posho hizi. 

Maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhusu suala hili ni kama ifuatavyo:



Kwanza, Mheshimiwa Rais Kikwete anakubali haja ya kuangalia upya posho kwa Wabunge lakini amewataka wabunge kutumia hekima na busara katika kulitafakari suala hili.



Pili, Mheshimiwa Rais Kikwete amewataka Wabunge kutumia Kikao cha sasa cha Bunge kulizungumza upya suala hilo.



Imetolewa na:


Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.

Dar es Salaam.
31 Januari, 2012

SUDAN YAFUZU ROBO FAINAL AFCON WAKATI ANGOLA IKIONDOSHWA!!!


Timu ya Taifa ya Sudan imeweza kufuzu katika hatua ya Robo Fainali na kuvunja ukame wa miaka 42 wa kupata ushindi kwenye Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuifunga Burkina Faso kwa magoli 2-1!! Sudan ilipata tiketi ya kucheza Robo Fainali baada ya Ivory Coast kuichapa Angola ambayo ilikuwa inahitaji pointi moja pekee ili iweze kufuzu kwa hatua ya Robo Fainali!! Sudan wamefanikiwa kuitoa kimasomaso Kanda ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA baada ya kufuzu hatua ya Robo Fainali!!

TFF YATANGAZA MAPATO YA MECHI YA TWIGA STARS!!!

Mechi ya marudiano ya raundi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Namibia (Brave Gladiators) imeingiza sh. 38,220,000.

Kiasi hicho ni kutokana na watazamaji 16,334 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa juzi (Januari 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Twiga Stars kuibuka na ushindi wa mabao 5-2.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 1,000 (watoto), sh. 2,000 (viti vya kijani na bluu), sh. 3,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 5,000 (VIP C na B) na sh. 10,000 kwa VIP A.

Watoto waliokata tiketi kuingia uwanja ni 634, viti vya rangi ya kijani na bluu 13,238, viti vya rangi ya chungwa 1,040, VIP B na C 1,246 na VIP A watazamaji 176.

Vilevile Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawashukuru washabiki na wadau wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha mechi hiyo kati ya Twiga Stars na Namibia.

WAMISRI KUICHEZESHA STARS FEB 29
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Misri kuchezesha mechi ya kwanza ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za 29 za Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Tanzania na Msumbiji.

Waamuzi watakaochezesha mechi hiyo namba 25 itakayochezwa Februari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni Farouk Mohamed atakayekuwa mwamuzi wa kati. Wasaidizi wake ni Ayman Degaish na B.T Abo El Sadat wakati mwamuzi wa akiba ni Ghead Grisha.

Kamishna wa mechi hiyo ni Loed Mc Ian wa Afrika Kusini. Mchezo wa marudiano kwa ajili ya fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini utafanyika jijini Maputo baadaye mwaka huu.

NAHODHA TWIGA STARS KUCHEZA UTURUKI
Nahodha wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars), Sophia Mwasikili ameondoka jana alfajiri (Januari 30 mwaka huu) kwa ndege ya Turkish Airlines kwenda Uturuki kucheza mpira wa kulipwa.

Mwasikili amekwenda kujiunga na Luleburgazgucu Spor Kulubu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya Wanawake nchini humo.

Beki huyo wa kati wa Twiga Stars aliyekuwa akichezea timu ya Sayari Women amejiunga na klabu yake hiyo mpya kwa mkataba wa miaka miwili.

Awali Mwasikili alitakiwa kujiunga mapema na timu hiyo lakini alilazimika kusubiri kwanza mechi ya marudiano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Twiga Stars na Namibia (Brave Gladiators) iliyochezwa Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tuesday, January 24, 2012

TFF YATANGAZA MABADILIKO YA RATIBA LIGI KUU NA VIINGILI VYA MCHEZO WA TWIGA STARS!!!

Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanya marekebisho madogo kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom kutokana na Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kutumika kwa sherehe za kitaifa za kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
Mechi namba 111 kati ya Toto Africans na African Lyon ambayo kwa mujibu wa ratiba ilikuwa ichezwe Februari 5 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza sasa itachezwa Aprili 18 mwaka huu.
 
Mabadiliko hayo yamefanyika baada ya wamiliki wa Uwanja wa CCM Kirumba, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kueleza kuwa watautumia kwa sherehe za kuzaliwa chama chao, hivyo hautakuwa na nafasi kwa Februari 4, 5 na 6 mwaka huu.
 
Uamuzi huo umesababisha pia mabadiliko kwa mechi nyingine mbili. Mechi namba 168 kati ya Villa Squad na African Lyon iliyokuwa ichezwe Aprili 18 mwaka huu Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, sasa itachezwa Aprili 22 mwaka huu.
 
Pia mechi namba 170 kati ya Azam na Toto Africans iliyokuwa ichezwe Aprili 29 mwaka huu jijini Dar es Salaam sasa imerudishwa nyuma hadi Aprili 26 mwaka huu ambayo ni Sikukuu ya Muungano.

 
VIINGILIO MECHI YA TWIGA STARS, NAMIBIA
Kiingilio cha chini kwa mechi ya kufuzu kwa fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Twiga Stars na Namibia itakayochezwa Jumapili (Januari 29 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa sh. 2,000.
 
Kiwango hicho ni kwa washabiki kwa viti vya bluu na kijani. Viti hivyo kwa pamoja vinachukua jumla ya watazamaji 36,693 kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua washabiki 60,000.
 
Pia kutakuwa na kiingilio cha watoto wenye umri wa chini ya miaka 10 ambacho ni sh. 1,000. Watoto watakaotumia tiketi hizo wanatakiwa kuingia uwanjani wakiwa na wazazi au walezi wao.
 
Viingilio vingine kwa mechi hiyo ni sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 5,000 kwa VIP B na C n ash. 10,000 kwa VIP A.
 
Namibia inatarajia kuwasili nchini Ijumaa (Januari 27 mwaka huu) saa 12.45 jioni kwa ndege ya South Africa Airways.

 
LIGI KUU VODACOM KUWANIA UBINGWA WA BARA
Mzunguko wa 14 wa Ligi Kuu ya Vodacom unamalizika kesho (Januari 25 mwaka huu) kwa mechi mbili zitakazochezwa kwenye viwanja tofauti jijini Dar es Salaam.
 
Simba itakuwa mwenyeji wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Viingilio vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP B na C, sh. 15,000 kwa VIP A.
 
Nayo Azam itakuwa mgeni wa African Lyon katika mechi namba 97 itakayochezwa Uwanja wa Chamazi. Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 10,000 kwa Jukwaa Kuu na sh. 3,000 mzunguko.   

 
YANGA YATAKIWA KUMLIPA NJOROGE SH. MILIONI 17
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kupitia kitengo chake cha utatuzi wa migogoro (Dispute Resolution Chamber- DRC) limeagiza klabu ya Yanga kumlipa mchezaji John Njoroge sh. 17,159,800 ikiwa ni fidia kwa kuvunja mkataba wake kinyume cha taratibu.
 
Uamuzi huo wa DRC chini ya Jaji Theo van Seggelen ambaye ni raia wa Uholanzi ulifanywa Desemba 7 mwaka jana jijini Zurich, Uswisi na kutumwa TFF kwa njia ya DHL, Januari 17 mwaka huu.
 
Njoroge ambaye ni raia wa Kenya aliwasilisha kesi yake FIFA kupinga Yanga kuvunja mkataba alioingia wa kuichezea timu yao kinyume na makubaliano. Mchezaji huyo hivi sasa anachezea timu ya Tusker ambayo ni mabingwa wa Kenya.
 
Yanga ina siku nne za kukata rufani kupinga uamuzi huo kuanzia tarehe iliyoupokea kama inataka kufanya hivyo. Klabu hiyo inatakiwa iwe imeshamlipa Njoroge ndani ya siku 30 tangu ilipopokea uamuzi huo. Ikishindwa kulipa ndani ya muda huo, itatozwa riba ya asilimia 5 kwa mwaka ya fedha hizo.
 
Ikiwa Yanga itashindwa kulipa ndani ya muda huo vilevile suala hilo litafikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya FIFA kwa hatua zaidi.

MAKAMANDA WA POLISI ZANZIBAR WAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WANAHABARI!!!

Makamanda wa Jeshi la Polisi Zanzibar wameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa vyombo vya Habari hapa nchini kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati muafaka ili kuwawezesha wananchi kupata haki yao ya kikatiba ya kupashwa habari.

Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, alisema kuwa ahadi hiyo imetolewa na Makamanda wa Polisi kutoka mikoa mitatu ya Unguja waliokuwa wakishiriki katika Mafunzo ya Uhusiano wa Polisi na Vyombo vya Habari yaliyokuwa yakifanyika kwenye chuo cha Polisi Zanzibar.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ACP Aziz juma Mohammed, alisema Polisi na Wanahabari ni watu wanaotegemeana kitaaluma na kwamba kazi ya Polisi isingetambulika kwa urahisi kwa raia kama sio juhudi za vyombo vya Habari.

Kamanda Azizi alisema ili kuwawezesha Waandishi wa Habari kutangasa habari kwa usahihi ni lazima Polisi nao wasiwe na kigugumizi katika kutoa taarifa zinazohitajika kwa waandishi.

Alisema kutoa taarifa sahihi na kwa wakati muafaka, kunaondoa uvumi ama minong’ono ya taarifa za kweli zilizokosa ufafanuzi kutoka kwa msemaji wa eneo husika.

Naye Kamaba wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Unguja ACP Augost Uromi, aliitaja mifano michache ya jinsi Polisi wanavyowahitaji Waandishi wa Habari kuwa ni pamoja na kusaidia kueneza mpango wa Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi jambo ambalo lingewawia Polisi vigumu kumfikia mwananchi moja mmoja kumjulisha juu ya dhana hiyo.

Alisema Vyombo vya Habari vinapotumika vizuri, huwawezesha watu wengi kupata habari moja na kwa wakati mmoja na hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa Polisi kuendelea kushirikiana kwa dhati na vyombo vya Habari na kuwaona ni wadau muhimu.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kaskazini Unguja ACP Ahmada Abdallah, aliongeza kuwa ili kuepuka waandishi kuandika taarifa zisizo sahihi ni vema kila Kamanda kuwa tayari kutoa taarifa za matukio kila yanapotokea.

Akitoa mada wakati wa mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Polisi Zanzibar SSP Ramadhan Mungi, aliwaambia walishiriki wa hao kuwa ili kuepuka upotoshwaji wa taarifa ni muhimu kila taarifa inayotolewa kwa waandishi wa Habari iwe ya maandishi.

Awali akifungua Mafunzo hayo, Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, alisema kuwa  Mafunzo hayo yameandaliwa ili kuwawezesha Maafisa wa Polisi kujua namna ya utayarishaji na usambazaji wa taarifa kwa vyombo vya Habari (Press Release) na jinsi ya kuandaa na kufanya mikutano ya moja kwa moja na waandishi wa habari. (Press Conference).

Mafunzo hayo ya siku mbili ambayo yalikuwa yakifanyika kwenye Chuo cha Polisi Zanzibar, (Zanzibar Police Academy) yamewashirikisha Kamakanda wa Polisi wa mikoa yote ya Unguja, Wakuu wa Upelelezi na Maafisa Wanadhim kutoka Mikoa ya Mjini Magharibi, Kusini na Kaskazini Unguja pamoja na Maafisa Waandamizi wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar.

RAIS KIKWETE AKUTANA NA mKURUGENZI KUTOKA CUBA!!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Januari 24, 2012, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masula ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Cuba, Bwana Alberto Velazco San Jose.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete na Bwana San Jose wamezungumzia masuala yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Cuba, masuala ya kanda ya Afrika na masuala mbalimbali ya kimataifa likiwamo lile la vikwazo ambazo Marekani iliiwekea Cuba tokea miaka ya 1960 na inaviendeleza.

“Uhusiano mzuri, wa karibu na wa miaka mingi ni kielelezo halisi cha jinsi nchi mbili ndogo na zinazoendelea zinavyoweza kushirikiana na kusaidiana kama ndugu,” Rais Kikwete amesema katika mazungumzo hayo na kuongeza, “Nipende pia kuishukuru Cuba na wananchi wa Cuba kwa kuunga mkono jitihada za maendeleo za nchi yetu miaka yote hii pamoja na kwamba mmeendelea kupambana na vikwazo vikubwa vya kila aina.”

Kwa miaka mingi, Tanzania na Cuba zimekuwa zinashirikiana katika masuala mengi na kusaidiana katika masuala ya kimataifa, na Cuba imeunga mkono jitihada za maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwamo za afya, elimu na michezo.

Bwana Alberto Valazco San Jose amemjulisha Rais Kikwete kuhusu mageuzi ya kiuchumi ambayo nchi hiyo inayafanya kwa kufungua uchumi wake kutoka uchumi wa dola na kuuelekeza kwenye uchumi wa soko ambako watu binafsi wanapata nafasi kushiriki katika uchumi wa nchi yao.

“Tunafanya mageuzi makubwa katika uchumi wetu kwa kuutoa kwenye uchumi wa dola na kuruhusu sekta binafsi kushiriki kwenye ujenzi wa uchumi huo. Tunafanya mageuzi lakini hatuna haraka kwa sababu hatutaki kufanya makosa katika jambo hili,” amesema Mkurugenzi huyo.

Naye Rais Kikwete ametumia nafasi hiyo kumjulisha Mkurugenzi huyo kuhusu jitihada za Serikali yake katika kujenga mazingira ya kuwaletea maisha bora Watanzania kwa kumweleza jitihada za Serikali kupambana na ugonjwa wa malaria, kuongeza uzalishaji wa sukari, kuongeza uzalishaji wa umeme, kupanua na kuboresha elimu na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Cuba ni moja ya mataifa yanayoongoza duniani kwa uzalishaji wa sukari, na imekuwa inajenga kiwanda cha dawa ya kuua mbu katika jitihada zake za kuisaidia Tanzania kukabiliana na ugonjwa wa malaria.

Rais Kikwete pia amemweleza mgeni huyo kuhusu jitihada za Serikali yake katika kuboresha miundombinu nchini kwa kuboresha usafiri wa reli, kukabiliana na matatizo katika usafiri wa anga, upanuzi na uboreshaji wa bandari za Tanzania na uendelezaji wa ujenzi wa barabara za lami nchini.

Bwana Alberto Valelazco San Jose yuko katika ziara za nchi za Afrika akiwa njiani kwenda Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) utakaofanyika Januari 29-30 mwaka huu.

Wakati huo huo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Kundi la Makampuni ya Frontline Development Partners ya Dubai inayotaka kuwekeza katika masuala ya maji, kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari, usafirishaji wa reli na uzalishaji wa umeme.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

MTUHUMIWA WA MAUAJI YA KIMBARI KUHAMISHIWA NCHINI RWANDA!!!

Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, mchungaji Jean Uwinkindi atasafirishwa kwenda Rwanda kabla ya Februari 23, kufuatia kuthibitishwa kwa hati mpya ya mashitaka na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR).

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika vya habari hapa, Mahakama iliyokuwa inashughulikia kesi hiyo, Jumatatu (Januari 23), ilithibitisha hati mpya ya mashitaka dhidi ya Uwinkindi ikiwa ni pamoja na mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi kama uhalifu dhidi ya binadamu.

Uamuzi huo umekuja siku chache baada ya Rais wa ICTR, kuamuru utekelezaji wa kuhamishwa Uwinkindi kupelekwa Rwanda ambako kesi yake itasikilizwa, katika kipindi kisichozidi siku 30 tangu kuthibitishwa kwa hati ya mashitaka baada ya kufanywa marekebisho kama ilivyoelekezwa na mahakama.

Katika uamuzi ulitiwa saini na Kaimu Rais wa ICTR, Jaji Vagn Joensen Januari 20, 2012, alifafanua kwamba ‘’Jean Uwinkindi atahamishiwa nchini Rwanda katika kipindi cha siku 30 baada ya mahakama kupokea hati ya mashitaka iliyofanyiwa marekebisho yaliyotakiwa.’’

Wiki iliyopita Mwendesha Mashitaka wa ICTR alimshutumu Msajili wa Mahakama hiyo, kwa kujaribu kuchelewesha bila ulazima kumhamishia nchini Rwanda, mchungaji Uwinkindi kama ilivyoamriwa na mahakama hiyo akitoa hoja kadhaa ambazo alidai hazina budi kushughulikiwa kabla ya kutekelezwa amri hiyo.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kukamilisha kutiliana saini na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) itakayosimamia uendeshaji wa kesi hiyo kwa haki, kupata fedha za kugharimia tume hiyo na kufanya ukaguzi wa gereza atakaloishi mtuhumiwa huyo nchini Rwanda kama inakidhi viwango vya kimataiafa.

Hata hivyo katika uamuzi wake, Kaimu Rais alifafanua kwamba Msajili alitakiwa kuyashughulikia masuala ya kutiliana saini na ACHPR na kutafuta fedha kwa ajili ya shughuli za taasisi hiyo kuanzia Juni 28, 2011 wakati maombi ya mwendesha mashitaka yalipokubaliwa huku wakisubiri uamuzi wa mwisho wa mahakama ya Rufaa.

‘’Rais anadhani kwamba kutomhamishia nchini Rwanda mtuhumiwa huyo kwa sababu kama hizo hakuna umuhimu kwa sasa,’’ hati ya uamuzi huo inasisitiza.

Kuhusu hoja ya gereza atakaloishi Uwinkinid akiwa Rwanda, Kaimu Rais alieleza kwamba kwa kumbukumbu alizonazo, Rwanda ina magereza mawili likiwemo Gereza Kuu la Kigali na lile la Mpanga ambayo yamefikia viwango vya kimataifa na ambayo yanaweza kumhifadhi Uwinkindi.

ICTR imeamua kesi ya Mchungaji Uwinkindi wa kanisa la Pentekoste kwenda kusikilizwa nchini Rwanda ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuhitimisha kazi za mahakama hiyo.

BALOTELLI KUFUNGIWA MICHEZO MINNE KWA UTOVU WA NIDHAMU MCHEZONI!!!


Mshambuliaji wa Kimataifa wa Italia anayekipiga na Klabu ya Manchester City Mario Balotelli ameingia matatani baada ya kuonekana kwenye picha za video akimkanyaga makusudi kiungo wa Tottenham Scott Parker kwenye mchezo wao wa jumapili!! Chama Cha Soka Nchini Uingereza FA kimesema kitamfungia Balotelli lakini ana nafasi ya kukata rufaa!! FA imesema iwapo atashindwa rufaa adhabu itaongezwa!!

Monday, January 23, 2012

MANCHESTER UTD NA CITY WASHINDA NA KUENDELEA KUPAMBANA KWENYE MBIO ZA UBINGWA!!!



Manchester United imefanikiwa kupata ushindi wa magoli 2-1 mbele ya Arsenal na kufanikiwa kuendelea kuweka tofauti ya pointi dhidi ya vinara Manchester City kusalia tatu!! Magoli ya Antonio Valencia na Danny Welbeck yalitosha kuwapa ushindi Manchester United!! Mchezo wa mapema Manchester City walipata ushindi wa magoli 3-2 mbele ya Tottenham!!

Friday, January 20, 2012

RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA KIFO CHA JEREMIA SOLOMON SUMARI!!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda (Mb.,) kutokana na kifo cha Mhe. Jeremia Solomon Sumari, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CCM na aliyepata kuwa Naibu Waziri, kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 19 Januari, 2012 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Mheshimiwa Jeremia Solomon Sumari kwani alikuwa kiongozi aliyewatumikia vema wananchi wa Jimbo lake la Uchaguzi la Arumeru Mashariki na Taifa kwa ujumla katika wadhfa wake wa Waziri kwa umahiri na uhodari mkubwa”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake.

Rais Kikwete amesema kutokana na kifo chake, wananchi wa Arumeru Mashariki wamepoteza kiongozi wa kutegemewa sana huku Taifa likiachwa na pengo kubwa ambalo si rahisi kuzibika ikizingatiwa kwamba alikuwa kiongozi katika Wizara ambayo ni mhimili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.

“Kwa dhati ya moyo wangu, natuma salamu za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya Marehemu Jeremia Sumari kwa kumpoteza kiongozi na mhimili madhubuti wa familia. Ninawahakikishia kwamba nipo pamoja nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa, na namuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema aipumzishe roho ya Marehemu Jeremia Solomon Sumari mahali pema peponi, Amina”, ameongeza kusema Rais Kikwete.

Ameiomba familia ya Marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

Thursday, January 19, 2012

BECKHAM AONGEZA MKATABA KUKIPIGA LA GALAXY!!!


Kiungo wa Kimataifa wa Uingereza David Beckham ambaye anakipiga katika Klabu ya Los Angeles Galaxy ameongeza mkataba wa miaka miwili kukipia kwenye timu hiyo tangu ajiunge nayo mwaka elfu mbili na saba akitokea Real Madrid!! Beckham ambaye alikuwa anasakwa na Klabu ya Paris St Germain amesema hatua yake kuendelea kubaki LA Galaxy ni hatua muhimu zaidi!!!

MBUNGE WA ARUMERU KUPITIA CCM JEREMIA SUMARI AFARIKI DUNIA!!!


Mbunge wa Arumeru kupitia Tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Jeremia Sumari amefariki Dunia asubuhi hii katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa anapatiwa matibabu!! Sumari alikuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi na anakuwa Mbunge wa Pili kufikwa na umauti baada ya Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Maendeleo na Demokrasia CHADEMA Regia Mtema!!

Wednesday, January 18, 2012

REAL MADRID YAPATA KICHAPO KUTOKA KWA BARCELONA!!!




Magoli mawili ya Carles Puyol na Eric Abidal yalitosha kuwazima Real Madrid kwenye mchezo wa kwanza wa Kombe la Copa Del Rey uliopigwa kwenye Dimba la Santiago Bernabeu!! Barcelona wamejiweka katika mazingira mazuri kufuzu hatua ya nusu fainal baada ya kutokea nyuma kwa goli la Cristiano Ronaldo na kupata ushindi huo!! Mchezo wa marudiano utapigwa juma lijalo kwenye Uwanja wa Camp Nou!!!

ASAMOAH GYAN TAYARI KWA MATAIFA YA AFRIKA!!!


Kikosi cha Timu ya Taifa ya Ghana maarufu kama Black Stars kimepata nguvu baada ya Mshambuliaji wake Asamoah Gyan kufanikiwa kurejea kwenye kikosi hicho kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Platinum Stars!! Kwenye mchezo huo Gyan alifanikiwa kufunga goli moja kati ya mawili huku jingine likifungwa na Andrew Ayew!!

Monday, January 16, 2012

MAN CITY YAONGEZA TOFAUTI YA POINTI KUFIKIA TATU MBELE YA MAN UTD!!!



Goli la pekee la kwake Edin Dzeko lilitosha kuwapa ushindi Manchester City mbele ya Wigan Athletics katika mchezo uliokuwa mgumu!! Dzeko alifunga kwa kichwa kiunganisha mpira uliopigwa na Davis Silva na hivyo kuongeza tofauti ya pointi kufikia tatu dhidi ya mahasimu wao Manchester United!!

KALOU AIPA USHINDI IVORY COAST DHIDI YA LIBYA!!!


Timu ya Taifa ya Ivory Coast imeendelea vyema katika michezo yake ya kirafiki baada ya kufanikiwa kuifunga Libya kwa goli 1-0!! Goli la pekee lilifungwa na Mshambuliaji anayekipiga na Chelsea Solomon Kalou!! Ivory Coast ilishuhudia mchezi Bora wa Afrika Yaya Toure naye akirejea baada ya kuwa maheruhi!! Mashindano ya Mataifa ya Afrika yanatarajia kuanza kutimua vumbi siku ya Jumamosi!!

Sunday, January 15, 2012

INTER MILAN WAWALAZA MAPEMA AC MILAN BAADA YA KUWAPA KICHAPO!!!


Goli pekee la Mshambuliaji wa Kimataifa wa Argentina Diego Milito lilitosha kuwanyamazisha AC Milan ambayo ilikuwa na rekodi mwanana ya kushinda katika michezo yake kumi na miwili!! Licha ya AC Milan kupata nafasi nyingi walishindwa kuzitumia na hivyo kushuhudia jahazi lao likizama!!

SWANSEA CITY YASHUSHA KILIO KWA ARSENAL!!!




Klabu ya Swensea ilipeleka kilio huko Emirates baada ya kufanikiwa kuwachakaza Washika Bunduki Arsenal kwa magoli 3-2 na hivyo kuifanya timu hiyo kukwamisha kwenye mipango yake ya kusaka nafasi nne za juu!! Kocha Mkuu wa Arsenal ameangusha lawama zake kwa Mabeki wa Timu hiyo na kuwataka kuwa makini kwenye michezo inayofuata!!

Tuesday, January 10, 2012

ZITTO KABWE ATOA WITO MZITO KWA SERIKALI!!

Mwezi Disemba mwaka 2011 Waziri wa Fedha na Uchumi alimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) kumwahidi mambo yepi Serikali ya Tanzania itafanya ili kurekebisha Bajeti yake. Utaratibu huu hufanyika kila mwaka kupitia mpango unaoitwa ‘Policy Support Instrument (PSI). Katika barua hiyo Waziri wa Fedha wa Tanzania ameahidi kwamba Serikali itafanya juhudi kupunguza matumizi ili kuweza kupunguza uwiano wa nakisi ya Bajeti na Pato la Taifa (fiscal deficit to GDP ratio) kutoka asilimia 7.2 mpaka asilimia 6.6 ya Pato la Taifa.

Waziri wa Fedha na Uchumi ameiambia IMF kwamba ifikapo mwisho wa Mwezi Disemba mwaka 2011 (wiki mbili zilizopita) Baraza la Mawaziri la Tanzania limefikia maamuzi ya kupunguza nakisi ya Bajeti kwa kiwango kilichotajwa. Maeneo yanayotajwa ni Pamoja na Miradi ya Maendeleo ambapo jumla ya miradi yenye thamani ya Tshs 157bn itakatwa. Waziriwa Fedha ametaja miradi hiyo katika Ukarabati na Ujenzi wa Miundombinu.

Kambi ya Upinzani Bungeni inapinga kuondolewa kwa miradi ya maendeleo ili kupunguza matumizi ya Serikali. Kimsingi wakati kama huu ambapo hali ya uchumi ni mbaya na vijana wengi vijijini na mijini hawana ajira tunasisitiza umuhimu wa kutumia zaidi kwenye miradi ya maendeleo.

*Punguza matumizi ya kawaida

Kambi ya Upinzani Bungeni inarejea wito wake kwa Serikali kupunguza matumizi ya kawaida ili kupata fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo. Haiwezekani kamwe tukawa Taifa huru iwapo miradi yetu yote ya maendeleo inafadhiliwa na wahisani. Kiwango kidogo tulichokiweka katika Bajeti ya mwaka huu ndicho hicho sasa kinakatwa na hivyo miradi yote ya maendeleo kubakia kwa wahisani ama kwa mikopo au misaada.

Kiwango cha Tshs 203bn sawa na 0.5% ya Pato la Taifa ambacho Serikali imeahidi kupunguza ni kidogo mno na kinalenga kuumiza watumishi wa kada ya chini ya Serikali na sio viongozi wakubwa. Bajeti ya Mafunzo inayoenda kukatwa itaumiza Manesi na Walimu au watumishi wanaoongeza ujuzi ili kuboresha kazi zao. Serikali ikate matumizi yote yasiyo ya lazima na hasa posho (360bn), ipunguze matumizi ya magari na yale yasiyo na uhitaji yapigwe mnada na viongozi wote isipokuwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika na Jaji Mkuu washushwe madaraja ya kusafiria kwenye ndege. Safari zote ambazo hazina mahusiano na miradi ya maendeleo zipigwe marufuku kwa muda wote wa miezi sita ya Bajeti iliyobakia.

Serikali ihakikishe matumizi katika Sekta ya Elimu na Afya hayakatwi kabisa ili kuhakikisha tunalinda mafanikio kiduchu ya upanuzi wa sekta hizi na kuongeza uwezo wa Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi hasa wa vijijini.

*Matumizi ya Maendeleo yasiguswe, yaongezwe

Tayari imeonekana kwamba katika kipindi chote cha nusu ya Bajeti Halmashauri za Wilaya hazijapata fedha za maendeleo. Mfano Halmashauri ya Wilaya Kigoma imepata asilimia 0.3 tu ya Bajeti ya Maendeleo ilhali Halmashauri ya Mji wa Mpanda imepata asilimia 4 tu. Ni dhahiri miradi ya maendeleo kwa maeneo mengi ya vijijini itakwama kwani ni wazi kabisa kwamba Halmashauri hazipati fedha zote za Bajeti ya Maendeleo.

Serikali itambue kwamba miradi ya maendeleo sio anasa bali ndio vyanzo vya baadaye vya mapato ya serikali. Miradi ya maendeleo hutoa ajira kwa wananchi na hivyo kuwapunguzia umasikini wa kipato. Jumla ya Tshs 157bn zinazotakiwa kukatwa zisikatwe bali ziongezwe ili kupata fedha za kurekebisha miundombinu kama Reli ya Kati.Kwa mfano Reli ya Kati inahitaji Tshs 200bn katika kipindi cha miaka 3 ili iweze kusafirisha mizigo tani 1.5m kwa mwaka kila siku na kuzalisha faida.

*Ongeza Mapato ya Ndani

Inashangaza kwamba katika mpango wa Serikali kupunguza nakisi ya Bajeti mkazo umewekwa kwenye kuondoa miradi ya maendeleo badala ya kuongeza mapato. Nakisi hupunguzwa ama kwa kupunguza matumizi au kwa kuongeza Mapato. Serikali katika Taarifa yake kwa IMF imeibua njia moja tu ya kuongeza mapato, kodi ya mapato kutoka Kampuni ya Geita Goldmine. Huu ni uvivu wa kufikiri.

Serikali imeambiwa mara kadhaa suala la kuanza kutumika kwa sheria mpya ya madini kwa Kampuni za Madini zilizokuwapo. Makusanyo ya Mrahaba peke yake kwa sheria mpya, kiwango kipya na kanuni mpya ya kukokotoa ingeongeza mrahaba mpaka Tshs 203bn kutoka Tshs 99bn za sasa. Kwanini Serikali ianvuta miguu katika kutekeleza hili? Waziri wa Nishati na Madini aliahidi Bungeni kwamba mazungumzo na Kampuni za Madini yanaisha Mwezi Septemba. Mbona Serikali imekuwa BUBU katika hili?

Serikali iliahidi kuangalia suala la mauzo ya mali za makampuni zilizoko Tanzania na kodi ambayo tunapaswa kukusanya, Serikali imekuwa kimya kabisa katika suala hili. Marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kuondoa msamaha kwenye ‘deemed capital goods yangeongeza mapato ya Serikali kwa kiwango kikubwa na kupunguza mzigo wa misamaha ya Kodi.

*Uwajibikaji kwa Bunge

Inashangaza zaidi kwamba sasa imekuwa ni mtindo kwa Serikali kutoa ‘commitments’ muhimu za kibajeti kwa Shirika la IMF badala ya wananchi kupitia Bunge. Bunge limepitisha Bajeti, mapitio yeyote ya Bajeti yanapaswa kuidhinishwa na Bunge. Bila kufanya hivyo maana ya Bunge kupitisha Bajeti inakuwa haina mantiki na uhuru wa Taifa letu unakuwa haupo kwetu.

Umuhimu wa Bunge kutunga haraka Sheria ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge (Parliamentary Budget Act) sasa unaonekana waziwazi. Muswada umewasilishwa Bungeni na Wabunge binafsi kutaka kuundwa kwa mfumo wa kuisimamia Serikali katika Bajeti. Ofisi ya Spika wa Bunge ihakikishe muswada huu unachapishwa katika Gazeti la Serikali mara moja ili usomwe kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Sita wa Bunge na kutungwa kuwa sheria katika mkutano wa Saba.

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ilete mpango wa kupunguza matumizi Bungeni ili ujadiliwe na kuidhinishwa na Bunge kabla ya kuanza kutumika. Vinginevyo Mpango wa Serikali kwa IMF utakuwa ni kudharau wananchi na kuuza uhuru wetu kwa Shirika la Fedha la Kimataifa. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mwishoni mwa miaka ya Sabini ‘toka lini Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limekuwa Wizara ya Fedha ya Kimataifa (International Ministry of Finance)?’

Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Waziri Kivuli Fedha na Uchumi
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni (NKUB)
Dar es Salaam, 10 Januari 2012.

Thursday, January 5, 2012

YAYA NA KOLO TOURE WATAKIWA KUJIUNGA NA KAMBI YA TIMU YA TAIFA!!


Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Ivory Coast Francois Zahoui ametaka wachezaji wawili wa timu hiyo wanaocheka katika Klabu ya Manchester City kujiunga mara moja na kikosi hicho kwa ajili ya maandailizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika!! Yaya Toure na kakake Kolo Toure wanatakiwa wawe wamejiunga na kambi siku ya jumamosi huko Paris kabla ya kuelekea Abu Dhabi kwa Kambi!! Kocha wa Man City Roberto Mancini alikuwa anataka kuwatumia wacheza hao kwenye mchezo wa Kombe la FA siku ya jumapili dhidi ya Manchester United!!

ZITTO KABWE ATOA WARAKA KWA JUSSA RADU BAADA YA KUFUKUZWA KWA HAMAD RASHID!!!


Ndugu Jussa, Kama rafiki yako mkubwa na unajua ninavyomheshimu Maalim Seif Kama kiongozi thabiti. Leo nakwambia usilolipenda. Sio sahihi katika demokrasia Kama yetu kumfukuza Mbunge Hamad Rashid au hata wanachama wengine wa chama chenu cha CUF.

Kama Maalim aliweza kumsamehe Salmin, aliweza kumsamehe Karume, aliweza kukubali kutangazwa kushindwa ilhali hata wewe unajua alishinda Urais wa Zanzibar iweje iwe muhali kumaliza tatizo hili dogo la Hamad Rashid? Hamad ana makosa lukuki. Nimefanya naye kazi Bungeni.

Hamad pia ana mazuri mengi kafanya. Hamad amejitoa muhanga. Uamuzi wa Baraza Kuu la CUF kumfukuza uanachama ufikiriwe upya. That is my appeal to you as a friend and a fine politician.

EWURA YATANGAZA ONGEZEKO LA BEI YA PETROLI NA MAFUTA YA TAA!!


Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji EWURA imependisha bei ya mafuta ya Petroli kwa shilingi 72 zaidi ya ile ya awali. Mbali na Petroli EWURA imepandisha bei ya mafuta ya Taa kwa shilingi 5 huku bei ya Dizali ikibaki kama ilivyo.

Awali bei ya Petroli iliuzwa shilingi 1882 na kuanzia leo inatarajiwa kuuzwa kwa shilingi 195 kwa lita, mafuta ya Taa yaliyokuwa yanauzwa kwa shilingi 1958 yatauzwa 1963 lakini Dizali itaendelea kuuzwa shilingi 1976 kwa lita.

Bei hiyo mpya inayotarajiwa kuanza kutumika leo kote nchini imekwenda sambamba na kuanza upya kwa matumizi ya kanuni ya ukokotoaji wa bei za mafuta.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EWURA kwa vyombo vya habari kanuni hiyo mpya inakwenda sambamba na kuanza kutumika kwa kanuni mpya za mfumo wa ukokotoaji wa bei ya mafuta.

“Kanuni hii itaanza kutumika Jumatano ya January 4 mwaka huu kwa Tanzania Bara na itakuwa ikirekebishwa kila baada ya mwezi mmoja” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa ilifafanua kuwa gharama za mafuta zinatokana na ongezeko la tozo inayotozwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania ambayo imeongezeka kutoka dola 8.30 za Marekani kwa ujazo wa tani moja hadi dola 10 za Marekani. Kiasi hicho ni kwa ujazo wa tani moja, pamoja na ongezeko la thamani VAT.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa ongezeko hilo limelenga kuiwezesha TPA kuendeleza miradi mbalimbali inayohusu biashara ya mafuta, ikiwamo ujenzi wa gati mpya ya kupakua mafuta SPM na Ukarabati wa mifumo ya miundombinu ya Kurasini Oil Jetty KOJ.

Ilitaja miradi mingine inayotekelezwa na TPA kuwa ni ujenzi wa maghala mapya na eneo la upokeaji mafuta na kwamba miradi itakapokamilika itaboresha kazi ya kupokea mafuta na pia itapunguza gharama za mafuta kumalizika kwa miradi hiyo.

Kutokana na bei hiyo mpya Petroli kwa Jiji la Dar Es Salaam itauzwa 1956, Dizeli shilingi 1977 na Mafuta ya Taa ni shilingi 1963. Mwanza Petroli itauzwa shilingi 2106, Dizali ni shilingi 2127 na Mafuta ya Taa ni shilingi 2112.

Katika Jiji la Arusha Petroli itauzwa kwa shilingi 2040, Dizeli itakuwa shilingi 2061 na Mafuta ya Taa yatakuwa shilingi 2047. Mbeya Petroli itauzwa shilingi 2063, Dizeli itakuwa shilingi 2084 na Mafuta ya Taa yatauzwa 2069.

Wednesday, January 4, 2012

MASHAHIDI 3,200 WAHOJIWA NA MAHAKAMA YA ICTR!!

Zaidi ya mashahidi 3,200 wameshatoa ushahidi katika kesi mbalimbali mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) tangu mahakama hiyo ianze rasmi kusikiliza kesi za mauaji ya kimbari mwaka 1997.

Rais wa Mahakama hiyo Jaji Khalida Rachid Khan alieleza katika ripoti yake kwamba usikilizaji wa ushahidi wa mashahidi hao ulichukukua jumla ya masaa 26,000.

Chombo Maalum kitakachorithi kazi zitakazoachwa na ICTR kitaanza kazi rasmi Julai mosi, mwaka huu, na kitakuwa pamoja na mambo mengine na jukumu la kuhifadhi nyaraka lukuki ikiwa ni pamoja na kurasa 900,000 za kumbukumbu za maandishi za mahakama na rekodi za kaseti na video za zaidi ya siku za kusikiliza kesi 6,000. Chombo hicho pia kitatunza maamuzi na hukumu zaidi ya 10,000.

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Desemba 7, 2011, juu ya maendeleo ya mkakati wa kuhitimisha kazi za ICTR, Jaji Khan aliahidi kwamba kesi katika ngazi ya mahakama ya awali yaani ICTR zitakamilika ifikapo Juni, 2012 ambapo kesi katika ngazi ya Mahakama ya Rufaa zitakamilika mwishoni mwa 2014.

NEWCASTLE UNITED YAIDHALILISHA MAN UTD KWA KIPIGO!!!





Klabu ya Manchester United imekubali kipigo cha magoli 3-0 kutoka kwa Newcastle United na hivyo kusalia pointi tatu nyuma ya vinara Manchester City!! Magoli yake Demba Ba, Yohan Cabaye na lile la kujifunga la Phil Jones yalitosha kuwapa ushindi Newcastle na kuwa kipigo cha pili mfululizo kwa Man Utd!!

CUF YAMTIMUA UANACHAMA MBUNGE WA WAWI HAMAD RASHID MOHAMMED!!


Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi CUF limemvua uanachama Mbunge wa Jimbo la Wawi na Mjumbe wa Baraza Kuu la Chama hicho Hamad Rashid Mohamed na wenzake watatu kwa madai ya kukiuka utaratibu wa chama hivyo na hivyo wamepoteza sifa za kuwa wanachama.

Uamuzi huo ulitangazwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara Julius Mtatiro kwenye Hotel ya Manson Mji Mkongwe baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Baraza Kuu la CUF ambalo liliwajadili Hamad na wenzake watatu ambao nao wamevuliwa uanachama.

Hamad ambaye alitangaza nia yake ya kuwania Ukatibu Mkuu wa CUF kwenye uchaguzi ujao akitaka kujenga heshima ya Chama hicho iliyopotea amethibitisha kutimuliwa kwake uanachama na ameahidi ataendelea kupigania haki yake Mahakama ili arejeshewe uanachama.

Mbunge huyo wa Wawi amesema iwapo watagonga mwamba kupata haki yao Mahakamani basi watafikiri uamuzi wa kuanzisha Chama chao na si kujiunga na chama kingine chochote hapa nchini Tanzania.

Hamad amekuwa akimkosoa vilivyo Katibu Mkuu wa CUF Seif Sharif Hamad kutokana na kuwa chanzo cha kukidhoofisha chama hicho huko Tanzania Bara kutokana na muda wake mwingi kuutumia kwenye masuala ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo yeye ni Makamu wa Rais wa Kwanza!!

Tuesday, January 3, 2012

RATIBA YA SHEREHE ZA MAPINDUZI YA ZANZIBAR YATOLEWA!!

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa ratiba ya sherehe za kuadhimisha miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambazo zinaanza rasmi kesho katika majimbo yote 50 ya Unguja na Pemba

Katibu wa Kamati ya Sherehe hizo Dk. Khalid Mohamed amesema kuanzia kesho kutakuwa na kazi ya usafishaji mazingira katika majimbo yote 50 ya Zanzibar ambapo wasimamizi wa zoezi hilo ni Halimashauri za Wilaya, Baraza la Manispaa,Mabaraza ya Miji na Masheha.

Kwa mujibu wa Ratiba hiyo inaonesha kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein atazindua Jengo la Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) huko Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi

Aidha Rais Shein anatarajiwa pia kuzindua Barabara ya Dunga-Amani katika hafala itakayofanyika huko Dunga Mkoa wa Kusini Unguja ambapo Januari 9 atafungua barabara mbili (2) za Wilaya ya Chake Chake Pemba ambazo ni Chanjamjawiri-Tundaua na Chanjamjawiri-Pujini.

Katika hatua nyingine Rais Shein anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Nyumba ya Madaktari kutoka Norway katika Chuo cha Afya cha Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi

Halikakadhalika Rais Shein atafungua Barabara nne (4) za Wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba ikiwemo Mtambile-Kengeja, Mtambile-Kangani, Mizingani-Wambaa na Kenya-Chambani

Shughuli nyengine atakazofanya Dk.Shein ni Ufunguzi wa Jengo la Ofisi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi huko Weni Mkoa wa Kaskazini Pemba na ataendesha zoezi la kuchangia Mfuko wa Fedha za Mikopo (Fund Rising) katika Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar

Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim seif Sharif Hamad anatarajiwa kuzindua Jengo la Ofisi ya Makao Makuu ya Mfuko wa Barabara Zanzibar ambapo jioni yake atafungua Jengo la Idara ya Uvuvi liliopo Maruhubi katika Mkoa wa Mjini Magharibi

Aidha Maalim seif Sharif Hamad atafungua Tangi la Maji Gongoni Wilaya ya Micheweni Pemba ikiwa ni shamra sharma za kutimiza mika 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Naye Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya Ufunguzi wa Skuli ya Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba ambapo pia atafungua Soko la Jumapili (Sunday Market) kwa wajasiriamali liliopo Michenzani Mkoa wa Mjini Magharibi

Viongozi wengine watakaofungua miradi mbalimbali ya maendeleo kwa nyakati tofauti ni pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mama Salma Kikwete na Marais Wastaafu wa Zanzibar

Wengine ni pamoja na Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao watahusika na ufunguzi wa miradi mbali mbali ya maedeleo

Shamra sharma za Sherehe za kutimiza miaka 48 ya Mapinduzi Zanzibar zimenza jana na ziaendelea katika mikoa yote ya Zanzibar ambapo kilele chake kitafikiwa Januari 12 katika kiwanja cha Aman Mjini Zanibar

TFF YATOLEA UFAFANUZI SAKATA LA MALIPO YA KUUZWA KWA MBWANA SAMATTA!!


FIDIA YA KIMBANGULILE KWA SAMATA
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya uenyekiti wa Alex Mgongolwa ilikutana Desemba 30 mwaka jana kupitia masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake ikiwemo taarifa ya uamuzi wa timu ya Kimbangulile kukata rufani Kamati ya Rufani kupinga uamuzi wake juu ya mchezaji Mbwana Samata.
 
Ikumbukwe kuwa Kimbangulile iliwasilisha malalamiko TFF ikieleza kuwa inastahili malipo baada ya Simba kumuuza Samata kwa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
 
Kimbangulile ilitaka ilipwe fidia ya mazoezi (training compensation) na mchango maalumu (solidarity contribution) kwa mujibu wa Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
 
Uamuzi wa Kamati ya Mgongolwa ulikuwa Kimbangulile imeshindwa kutoa vielelezo kuonesha kuwa iliingia gharama za mazoezi kwa mchezaji husika wakati akiichezea timu hiyo.
 
Kwa upande wa solidarity contribution ambayo ni asilimia 5 ya mauzo ya mchezaji huyo TP Mazembe, fedha hizo zinatakiwa kulipwa na klabu yake hiyo mpya ambayo TFF itaitaka kufanya hivyo wakati Samata atakapoombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC). Hivyo Kamati itatengeneza utetezi wake na kuuwasilisha kwenye Kamati ya Rufani itakaposikiliza rufani ya Kimbangulile.

RAIS KIKWETE AFANYA UTEUZI WA MABALOZI WAPYA!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewateua mabalozi wawili kuanzia Oktoba 12, mwaka jana, 2011, Katibu Mkuu Kiongozi, Bwana Ombeni Yohana Sefue ametangaza leo, Jumanne, Januari 3, 2012.

Katika taarifa yake, Katibu Mkuu Kiongozi Sefue amesema kuwa Rais Kikwete amemteua Dkt. James Alex Msekela kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia. Kabla ya hapo Mheshimiwa Msekela alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Aidha, taarifa hiyo ya Bwana Sefue imesema kuwa Rais Kikwete amemteua Bwana Ramadhani Muombwa Mwinyi kuwa Naibu Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York. Kabla ya hapo, Bwana Mwinyi alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Katibu Mkuu kiongozi amesema katika taarifa yake kuwa wateuliwa hao wawili wataapishwa keshokutwa, Alhamisi, Januari 5, 2012.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

MAN CITY YAIZIMA LIVERPOOL WAKATI TOTTENHAM IKIPAA!!





Magoli ya kwao Sergio Kun Aguero, Yaya Toure na James Milner yalitosha kuwapa ushindi Manchester City iliyomaliza ikiwa na wachezaji kumi kupata ushindi wa magoli 3-0 mbele ya Liverpool!! Man City ilimpoteza Gareth barry baada ya kuzawadiwa kadi nyekundu lakini haikuwa kikwazo kuibuka na ushindi!! Tottenham nao wameendelea kuchupa baada ya kuifunga West Bromwich Albion kwa goli 1-0 huku Sunderland ikishusha ghadhabu zake kwa Wigan Athletic na kuifunga magoli 4-1!!

Monday, January 2, 2012

ARSENAL YACHAPWA NA FULHAM WAKATI CHELSEA IKIPATA USHINDI MBELE YA WOLVES!!





Klabu ya Arsenal imekumbana na kichapo kutoka kwa Fulham cha magoli 2-1!! Washika Bunduki hao ndiyo walikuwa wa kwanza kupata goli kabla ya magoli ya Steve Sidwell na Bobby Zamora kulizamisha jahazi la timu hiyo!! Katika mchezo mwingine Chelsea wakaibuka na ushindi wa magoli 2-1 mbele ya Wolves!!
Matokeo mengine ni:
Aston Villa 0-2 Swansea
Blackburn 1-2 Stoke City
QPR 2-1 Norwich City