Thursday, January 5, 2012

EWURA YATANGAZA ONGEZEKO LA BEI YA PETROLI NA MAFUTA YA TAA!!


Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji EWURA imependisha bei ya mafuta ya Petroli kwa shilingi 72 zaidi ya ile ya awali. Mbali na Petroli EWURA imepandisha bei ya mafuta ya Taa kwa shilingi 5 huku bei ya Dizali ikibaki kama ilivyo.

Awali bei ya Petroli iliuzwa shilingi 1882 na kuanzia leo inatarajiwa kuuzwa kwa shilingi 195 kwa lita, mafuta ya Taa yaliyokuwa yanauzwa kwa shilingi 1958 yatauzwa 1963 lakini Dizali itaendelea kuuzwa shilingi 1976 kwa lita.

Bei hiyo mpya inayotarajiwa kuanza kutumika leo kote nchini imekwenda sambamba na kuanza upya kwa matumizi ya kanuni ya ukokotoaji wa bei za mafuta.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EWURA kwa vyombo vya habari kanuni hiyo mpya inakwenda sambamba na kuanza kutumika kwa kanuni mpya za mfumo wa ukokotoaji wa bei ya mafuta.

“Kanuni hii itaanza kutumika Jumatano ya January 4 mwaka huu kwa Tanzania Bara na itakuwa ikirekebishwa kila baada ya mwezi mmoja” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa ilifafanua kuwa gharama za mafuta zinatokana na ongezeko la tozo inayotozwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania ambayo imeongezeka kutoka dola 8.30 za Marekani kwa ujazo wa tani moja hadi dola 10 za Marekani. Kiasi hicho ni kwa ujazo wa tani moja, pamoja na ongezeko la thamani VAT.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa ongezeko hilo limelenga kuiwezesha TPA kuendeleza miradi mbalimbali inayohusu biashara ya mafuta, ikiwamo ujenzi wa gati mpya ya kupakua mafuta SPM na Ukarabati wa mifumo ya miundombinu ya Kurasini Oil Jetty KOJ.

Ilitaja miradi mingine inayotekelezwa na TPA kuwa ni ujenzi wa maghala mapya na eneo la upokeaji mafuta na kwamba miradi itakapokamilika itaboresha kazi ya kupokea mafuta na pia itapunguza gharama za mafuta kumalizika kwa miradi hiyo.

Kutokana na bei hiyo mpya Petroli kwa Jiji la Dar Es Salaam itauzwa 1956, Dizeli shilingi 1977 na Mafuta ya Taa ni shilingi 1963. Mwanza Petroli itauzwa shilingi 2106, Dizali ni shilingi 2127 na Mafuta ya Taa ni shilingi 2112.

Katika Jiji la Arusha Petroli itauzwa kwa shilingi 2040, Dizeli itakuwa shilingi 2061 na Mafuta ya Taa yatakuwa shilingi 2047. Mbeya Petroli itauzwa shilingi 2063, Dizeli itakuwa shilingi 2084 na Mafuta ya Taa yatauzwa 2069.

No comments:

Post a Comment