Tuesday, January 24, 2012

MAKAMANDA WA POLISI ZANZIBAR WAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WANAHABARI!!!

Makamanda wa Jeshi la Polisi Zanzibar wameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa vyombo vya Habari hapa nchini kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati muafaka ili kuwawezesha wananchi kupata haki yao ya kikatiba ya kupashwa habari.

Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, alisema kuwa ahadi hiyo imetolewa na Makamanda wa Polisi kutoka mikoa mitatu ya Unguja waliokuwa wakishiriki katika Mafunzo ya Uhusiano wa Polisi na Vyombo vya Habari yaliyokuwa yakifanyika kwenye chuo cha Polisi Zanzibar.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ACP Aziz juma Mohammed, alisema Polisi na Wanahabari ni watu wanaotegemeana kitaaluma na kwamba kazi ya Polisi isingetambulika kwa urahisi kwa raia kama sio juhudi za vyombo vya Habari.

Kamanda Azizi alisema ili kuwawezesha Waandishi wa Habari kutangasa habari kwa usahihi ni lazima Polisi nao wasiwe na kigugumizi katika kutoa taarifa zinazohitajika kwa waandishi.

Alisema kutoa taarifa sahihi na kwa wakati muafaka, kunaondoa uvumi ama minong’ono ya taarifa za kweli zilizokosa ufafanuzi kutoka kwa msemaji wa eneo husika.

Naye Kamaba wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Unguja ACP Augost Uromi, aliitaja mifano michache ya jinsi Polisi wanavyowahitaji Waandishi wa Habari kuwa ni pamoja na kusaidia kueneza mpango wa Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi jambo ambalo lingewawia Polisi vigumu kumfikia mwananchi moja mmoja kumjulisha juu ya dhana hiyo.

Alisema Vyombo vya Habari vinapotumika vizuri, huwawezesha watu wengi kupata habari moja na kwa wakati mmoja na hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa Polisi kuendelea kushirikiana kwa dhati na vyombo vya Habari na kuwaona ni wadau muhimu.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kaskazini Unguja ACP Ahmada Abdallah, aliongeza kuwa ili kuepuka waandishi kuandika taarifa zisizo sahihi ni vema kila Kamanda kuwa tayari kutoa taarifa za matukio kila yanapotokea.

Akitoa mada wakati wa mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Polisi Zanzibar SSP Ramadhan Mungi, aliwaambia walishiriki wa hao kuwa ili kuepuka upotoshwaji wa taarifa ni muhimu kila taarifa inayotolewa kwa waandishi wa Habari iwe ya maandishi.

Awali akifungua Mafunzo hayo, Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, alisema kuwa  Mafunzo hayo yameandaliwa ili kuwawezesha Maafisa wa Polisi kujua namna ya utayarishaji na usambazaji wa taarifa kwa vyombo vya Habari (Press Release) na jinsi ya kuandaa na kufanya mikutano ya moja kwa moja na waandishi wa habari. (Press Conference).

Mafunzo hayo ya siku mbili ambayo yalikuwa yakifanyika kwenye Chuo cha Polisi Zanzibar, (Zanzibar Police Academy) yamewashirikisha Kamakanda wa Polisi wa mikoa yote ya Unguja, Wakuu wa Upelelezi na Maafisa Wanadhim kutoka Mikoa ya Mjini Magharibi, Kusini na Kaskazini Unguja pamoja na Maafisa Waandamizi wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar.

No comments:

Post a Comment