Wednesday, January 4, 2012

CUF YAMTIMUA UANACHAMA MBUNGE WA WAWI HAMAD RASHID MOHAMMED!!


Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi CUF limemvua uanachama Mbunge wa Jimbo la Wawi na Mjumbe wa Baraza Kuu la Chama hicho Hamad Rashid Mohamed na wenzake watatu kwa madai ya kukiuka utaratibu wa chama hivyo na hivyo wamepoteza sifa za kuwa wanachama.

Uamuzi huo ulitangazwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara Julius Mtatiro kwenye Hotel ya Manson Mji Mkongwe baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Baraza Kuu la CUF ambalo liliwajadili Hamad na wenzake watatu ambao nao wamevuliwa uanachama.

Hamad ambaye alitangaza nia yake ya kuwania Ukatibu Mkuu wa CUF kwenye uchaguzi ujao akitaka kujenga heshima ya Chama hicho iliyopotea amethibitisha kutimuliwa kwake uanachama na ameahidi ataendelea kupigania haki yake Mahakama ili arejeshewe uanachama.

Mbunge huyo wa Wawi amesema iwapo watagonga mwamba kupata haki yao Mahakamani basi watafikiri uamuzi wa kuanzisha Chama chao na si kujiunga na chama kingine chochote hapa nchini Tanzania.

Hamad amekuwa akimkosoa vilivyo Katibu Mkuu wa CUF Seif Sharif Hamad kutokana na kuwa chanzo cha kukidhoofisha chama hicho huko Tanzania Bara kutokana na muda wake mwingi kuutumia kwenye masuala ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo yeye ni Makamu wa Rais wa Kwanza!!

No comments:

Post a Comment