Tuesday, January 24, 2012

MTUHUMIWA WA MAUAJI YA KIMBARI KUHAMISHIWA NCHINI RWANDA!!!

Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, mchungaji Jean Uwinkindi atasafirishwa kwenda Rwanda kabla ya Februari 23, kufuatia kuthibitishwa kwa hati mpya ya mashitaka na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR).

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika vya habari hapa, Mahakama iliyokuwa inashughulikia kesi hiyo, Jumatatu (Januari 23), ilithibitisha hati mpya ya mashitaka dhidi ya Uwinkindi ikiwa ni pamoja na mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi kama uhalifu dhidi ya binadamu.

Uamuzi huo umekuja siku chache baada ya Rais wa ICTR, kuamuru utekelezaji wa kuhamishwa Uwinkindi kupelekwa Rwanda ambako kesi yake itasikilizwa, katika kipindi kisichozidi siku 30 tangu kuthibitishwa kwa hati ya mashitaka baada ya kufanywa marekebisho kama ilivyoelekezwa na mahakama.

Katika uamuzi ulitiwa saini na Kaimu Rais wa ICTR, Jaji Vagn Joensen Januari 20, 2012, alifafanua kwamba ‘’Jean Uwinkindi atahamishiwa nchini Rwanda katika kipindi cha siku 30 baada ya mahakama kupokea hati ya mashitaka iliyofanyiwa marekebisho yaliyotakiwa.’’

Wiki iliyopita Mwendesha Mashitaka wa ICTR alimshutumu Msajili wa Mahakama hiyo, kwa kujaribu kuchelewesha bila ulazima kumhamishia nchini Rwanda, mchungaji Uwinkindi kama ilivyoamriwa na mahakama hiyo akitoa hoja kadhaa ambazo alidai hazina budi kushughulikiwa kabla ya kutekelezwa amri hiyo.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kukamilisha kutiliana saini na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) itakayosimamia uendeshaji wa kesi hiyo kwa haki, kupata fedha za kugharimia tume hiyo na kufanya ukaguzi wa gereza atakaloishi mtuhumiwa huyo nchini Rwanda kama inakidhi viwango vya kimataiafa.

Hata hivyo katika uamuzi wake, Kaimu Rais alifafanua kwamba Msajili alitakiwa kuyashughulikia masuala ya kutiliana saini na ACHPR na kutafuta fedha kwa ajili ya shughuli za taasisi hiyo kuanzia Juni 28, 2011 wakati maombi ya mwendesha mashitaka yalipokubaliwa huku wakisubiri uamuzi wa mwisho wa mahakama ya Rufaa.

‘’Rais anadhani kwamba kutomhamishia nchini Rwanda mtuhumiwa huyo kwa sababu kama hizo hakuna umuhimu kwa sasa,’’ hati ya uamuzi huo inasisitiza.

Kuhusu hoja ya gereza atakaloishi Uwinkinid akiwa Rwanda, Kaimu Rais alieleza kwamba kwa kumbukumbu alizonazo, Rwanda ina magereza mawili likiwemo Gereza Kuu la Kigali na lile la Mpanga ambayo yamefikia viwango vya kimataifa na ambayo yanaweza kumhifadhi Uwinkindi.

ICTR imeamua kesi ya Mchungaji Uwinkindi wa kanisa la Pentekoste kwenda kusikilizwa nchini Rwanda ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuhitimisha kazi za mahakama hiyo.

No comments:

Post a Comment