Friday, December 30, 2011

BALOZI OMBENI YOHANA SEFUE ATEULIWA KUWA KATIBU MKUU KIONGOZI!!!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Balozi Ombeni Yohana Sefue kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Balozi Sefue anachukua nafasi inayoachwa wazi na Bwana Phillemon Luhanjo ambaye anahitimisha mkataba wake wa utumishi wa umma kesho, Jumamosi, Desemba 31, 2011.

Kabla ya uteuzi wake, Balozi Sefue alikuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Kabla ya hapo, Balozi Sefue alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani na kabla ya hapo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada tokea Oktoba 2005.

Balozi Sefue ataapishwa kesho, Jumamosi, Desemba 31, 2011 saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
30 Desemba, 2011

Thursday, December 29, 2011

PIGO KWA TASNIA YA HABARI TANZANIA JOHN NGAYHOMA AFARIKI DUNIA!!!


Mtangazaji wa zamani wa ITV/Radio One na Shirika la Utanagazaji la Uingereza BBC Kiswahili John Ngahyoma amefariki dunia mapema asubuhi ya leo!! Ngahyoma amefikwa na mauti akiwa Hospital ambako alikuwa anapatiwa matibabu baada ya kuugua kwa muda mrefuna hata kulazimika kupekwa nchini India kwa matibabu lakini haikusaidia!! Kifo cha Ngahyoma kimekuja wakati Tasnia ya Habari ikiwa imepata pigo kubwa la kuondokewa na mwandishi wa Tbc Halima Mchuka!! Blogu hii imepokea kwa masikitiko makubwa sana kifo hicho!! Mwenyezimungu aiweke roho yake mahali panapostahili!! Ameen!!

RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA KIFO CHA HALIMA MCHUKA!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Bwana Clement Mshana, kuomboleza kifo cha mtangazaji maarufu wa shirika hilo, Bi Halima Mohammed Mchuka ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia leo, Alhamisi, Desemba 29, 2011 kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.

“Nimepokea kwa huzuni habari za kifo cha Halima Mohammed Mchuka. Nakutumia wewe Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) salamu za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo chake. Nakuomba, kupitia kwako, uniwasilishie salamu zangu kwa wafanyakazi wenzake katika TBC ambao wamempoteza mwenzao na rafiki yao.”

Ameongeza Mheshimiwa Rais katika salamu zake, “Aidha, nataka kupitia kwako niwatumie salamu zangu za rambirambi wana-familia, ndugu na jamaa wote za marehemu. Wajulishe kuwa niko nao katika wakati huu wa maombolezo na kwamba msiba wao ni msiba wangu pia. Nawaomba wawe na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi ya Mungu. Naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amen.”

Mheshimiwa Rais pia amesema kuwa Bi. Mchuka ametoa mchango mkubwa katika nyanja ya utangazaji nchini. “Sote tutaendelea kukumbuka weledi wake, uzalendo wake na ujasiri wake katika utangazaji uliomsukuma kuwa Mwanamke wa Kwanza katika Tanzania kutangaza mechi za mpira wa miguu”.

Ameongeza Rais Kikwete: “Ni dhahiri kuwa nyanja ya utangazaji imeondokewa na mtu muhimu na namna nzuri zaidi ya kumuenzi Bi. Mchuka ni kwa watangazaji waliobakia kuendelea kuiga mfano wake katika ubora wa utangazaji nchini mwetu.”

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29 Desemba, 2011

NGOMA MPYA YA TID INAITWA HANITAKI!!

MATUKIO YALIYOTOKEA KWENYE MAHAKAMA YA ICTR-ARUSHA!!!

Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) inaweza kusherehekea mwisho wa mwaka 2011 kwa kujivuna kutokana na hukumu nzito na nyingi zilizotolewa katika mwaka huo.

Mahakama hiyo imetoa jumla ya hukumu 10 katika ngazi zote mbili za mahakama ya awali na mahakama yake ya Rufaa zenye kuhusisha watu 21, akiwemo mwanamke pekee kuwahi kushitakiwa na mahakama hiyo, Pauline Nyiramasuhuko na mtu anayesadikiwa kuwa mpangaji mkuu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994,Kanali Theoneste Bagosora.

Hukumu za ICTR 2011

Gatete ahukumiwa kifungo cha maisha: Machi 29, 2011, ICTR ilianza mwaka mpya kwa kutoa hukumu yake ya kwanza katika kesi inayomkabili aliyekuwa afisa mwandamizi wa serikali ya Rwanda, Jean-Baptiste Gatete ambaye alitiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi. Alipewa adhabu ya kifungo cha maisha jela na kesi hiyo sasa iko mahakama ya Rufaa.

Aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi ahukumiwa kifungo cha miaka 30: Mei 17, 2011, Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa ilitoa hukumu nyingine nzito katika kesi inayohusisha maafisa wanne wa zamani wa jeshi la Rwanda wakiwemo Afisa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi hilo , Jenerali Augustin Bizimungu na Afisa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Jenerali Augustin Ndindiliyimana.Majenerali hao walitiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.Bizimungu alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela huku mwenzake, Ndindiliyimana alipewa adhabu ya muda aliokwisha tumikia akiwa kizuizini tangu mwaka 2000.Aliachiwa huru mara moja.

Maafisa wengine waliotiwa hatiani ni pamoja na Mkuu wa Bataliani ya Usalama Jesheni, Meja Francois-Xavier Nzuwonemeye na Kapteni Innocent Sagahutu pia wa Bataliani hiyo ambao walipewa kila mmoja wao adhabu za vifungo vya miaka 20 jela baada ya kutiwa hatiani kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.Pande zote mbili za mwendesha mashitaka na utetezi zimekata rufaa.

Mwanamke pekee na wengine watano watiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari: Juni 24, 2011 ilikuwa siku ya pekee katika historia ya ICTR kwa kutoa hukumu ya kesi iliyokuwa na watuhumiwa wengi zaidi kuliko kesi yoyote katika mahakama hiyo.Kesi hiyo maarufu kwa jina la Kesi ya Butare, inajumuisha watuhumiwa sita akiwemo mwanamke pekee, Pauline Nyiramasuhuko, Waziri wa zamani wa Familia na Masuala ya Wanawake na mtoto wake wa kiume, Arsene Shalom Ntahobali. Wawili hao walihukumiwa vifungo vya maisha jela baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu ukiwemo ubakaji na kuteketeza kizazi na uhalifu wa kivita.

Wengine waliotiwa hatiani katika kesi hiyo ni pamoja na Eli Ndayambaje, aliyehukumiwa pia kifungo cha maisha jela, Alphonse Nteziryayo, alipewa adhabu ya kifungo cha miaka 30, Sylvain Nsabimana atatumikia miaka 25 jela ambapo Joseph Kanyabashi alipewa adhabu ya miaka 35 jela. Wote sita wanasubiri tarehe ya kusikilizwa kwa rufaa zao.

Mawaziri wawili waachiwa huru na wengine wawili watiwa hatiani: Septemba 30, 2011, hukumu nyingine ilitolewa katika kesi inayohusisha mawaziri wanne wa zamani wa Rwanda katika serikali ya mpito ya mwaka 1994. Mahakama iliwaachia huru mawaziri wawili ikiwa ni pamoja na Casimir Bizimungu (Afya) na Jerome Bicamumpka (Mambo ya Nje). Waliotiwa hatiani ni Justin Mugenzi (Biashara) na Prosper Mugiraneza (Utumishi wa Umma) ambao kila mmoja wao alipewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kula njama za kufanya mauaji ya kimbari na uchohezi.Kama ilivyokuwa kwa wote waliotiwa hatiani nao wamekata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Meya wa zamani ahukumiwa kifungo cha miaka 15 jela: Novemba 17, 2011 Mahakama pia ilitoa hukumu nyingine katika kesi ya meya wa zamani nchini Rwanda, Gregoire Ndahimana. Alitiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari na ukatili dhidi ya binadamu na kuhukumiwa adhabu ya kifungio cha miaka 15.Anasubiri kupangiwa tarehe ya kusikilizwa rufaa yake.

Wanasiasa vigogo wawili wa Rwanda kutumikia jela maisha: Desemba 21, 2011 ICTR ilitoa hukumu ya mwisho kwa mwaka huu katika kesi ya wanasiasa wawili wa kilichokuwa chama tawala cha MRND wakati wa mauaji ya kimbari ikiwa ni pamoja na Rais wa chama hicho Mathieu Ngirumpatse na Makamu wake, Edouard Karemera.Walitiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. Walipatikana na hatia hususa ni kwa sababu ya nafasi yao kama viongozi wa juu wa chama hicho kwa kushindwa kuwazuia wala kuwaadhibu wanamgambo wa chama chao maarufu kama Interahamwe waliokuwa wanashiriki katika mauaji ya kimbari.

Hukumu za Mahakama ya Rufaa

Luteni Kanali Muvunyi kuendelea kutumikia miaka 15 jela: Aprili 1, 2011, Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya ICTR, ilithibitisha adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela aliyopewa afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda Luteni Kanali Tharcisse Muvunyi. Afisa huyo aliyekuwa katika Chuo cha Maafisa wa Jeshi Wasiokuwa na Kamisheni (ESO) alitiwa hatiani kwa uchochezi wa mauaji ya kimbari katika hotuba yake aliyoitoa Kusini mwa Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari mwaka 1994.

Luteni Kanali Setako kuendelea kutumikia miaka 25 jela: Septemba 28, 2011 Mahakama ya Rufaa pia ilithitisha adhabu ya kifungo cha miaka 25 jela aliyopewa aliyekuwa afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Luteni Kanali Ephrem Setako baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.

Maafisa wawili waandamizi wa zamani wa jeshi wanusurika vifungo vya maisha: Desemba 14, 2011, Mahakama ya Rufaa ilipunguza hadi miaka 35 jela adhabu ya kifungo cha maisha aliyopewa mtu anayesadikiwa kuwa alikuwa mpangaji mkuu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda Kanali Theoneste Bagosora baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari,uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.Katika mahakama hiyo pia tarehe hiyohiyo ilimpunguzia afisa mwingine adhabu kama hiyo ya kifungo cha maisha jela hadi miaka 15, afisa mwingine wa jeshi, Luteni Kanali Anatole Nsengiyumva. Kwa kuzingatia muda aliokwishatumikia akiwa kizuizini tangu atiwe mbaroni, mahakama iliamuru kuachiwa huru mara moja.

Kesi ya mtuhumiwa wa ICTR kusikilizwa Rwanda kwa mara ya kwanza: Desemba 16, 2011, Mahakama ya Rufaa ilitoa uamuzi wa kihistoria kwa kuruhusu kesi ya mchungaji Jean Uwikinkindi kwenda kusikilizwa nchini Rwanda.Mahakama mapema ilitupilia mbali rufaa ya mtuhumiwa huyo kupinga uamuzi wa mahakama ya awali ulioamuru kesi hiyo kwenda kusikilizwa nchini Rwanda Juni 28, 2011. Umuazi huo unafungua njia kwa kesi nyingine za watuhumiwa wa ICTR kupelekwa kusikilizwa nchini Rwanda.

Matukio mengine muhimu ICTR

Uchaguzi wa Rais na Makamu wake ICTR: Jaji mwanamke, raia wa Pakistani, Khalida Rachid Khan alichanguliwa kuwa Rais wa ICTR,kuanzia Mei 27, 2011 kwa kipindi cha miaka miwili. Jaji Khan ambaye alikuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama namba III alikuwa Makamu wa Rais wa ICTR tangu Mei 29, 2007. Wakati hohuo, Rais huyo alitangaza Agosti 24, 2011 kwamba Jaji Vagn Joenson kutoka Denmark aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa ICTR. Jaji huyo alianza rasmi kazi hiyo Agosti 26, 2011.

Kuachiwa mapema mfungwa wa mauaji ya kimbari: Mfungwa wa mauaji ya kimbari, Michel Bagaragaza, aliachiwa toka gerezani nchini Sweden alikokuwa anatumikia adhabu ya kifungo cha miaka nane jela baada ya kutumikia tayari theluthi mbili ya adhabu hiyo iliyotolewa na ICTR kwa kula njama za kufanya mauaji ya kimbari.Hii ni mara ya kwanza kwa Mahakama hiyo ya Umoja wa Mtaifa kuruhusu mmoja wa wafungwa wake kutoka jela kabla ya muda wa adhabu uliotolewa kumalizika. Bagaragaza alikuwa Mkuu wa Mamlaka ya Chai nchini Rwanda.

Wito kwa mataifa kupokea wanaoachiwa huru ICTR: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezitaka nchi wanachama wa umoja huo kuwapokea watuhumiwa wanaoachiwa huru na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) na kuendelea kubaki chini ya uangalizi wa mahakama hiyo. Wapo watuhumiwa watano waliokwishaachiwa huru lakini bado wanatafuta nchi za kuwapokea.

TFF YATOA RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHEZAJI WA ZAMANI WA TAIFA STARS RASHID MOYO!!!

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 29, 2011

RAMBIRAMBI MSIBA WA RASHID MOYO

Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa, Rashid Moyo kilichotokea usiku wa Desemba 25 mwaka huu kwao Msambweni, Tanga.

Moyo ambaye aliichezea timu ya Taifa kwenye miaka ya 70 alizikwa Desemba 26 mwaka huu kwenye makaburi ya Mabawa mkoani Tanga. Pia alikuwa mchezaji wa timu ya Coastal Union ya mkoa wa Tanga.

Msiba huo ni pigo kwa familia ya Moyo, TFF na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango alioutoa kwa Tanzania hasa wakati akiwa mchezaji.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Moyo, Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Tanga (TRFA) na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito. Pia TFF itatoa ubani wa sh. 100,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.

Mungu aiweke roho ya marehemu Rashid Moyo mahali pema peponi. Amina

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

MTANGAZAJI WA TBC HALIMA MCHUKA AFARIKI DUNIA!!


Mtangazaji Mahiri wa Mpira katika Eneo la Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Mwanamke wa Kwanza Halima Mchuka amefariki Dunia akiwa anahudumu katika Redio Tanzania Dar es Salaam RTD na baadae Shirika la Utangazaji Tanzania (SHIUTA) amefariki Dunia.

Mchuka amefariki usiku wa kumkia leo kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi kwa muda ambapo kwa sasa inaelezwa alikuwa anaanza kupata nafuu baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mtangazaji Halima Mchuka alijiunga na Radio Tanzania Dar es Salaam mwaka 1994 ambapo alifanya kazi katika Idara ya Habari na Idara ya mipango.

Mungu ailaze Roho ya BI Halima Mchuka pahala pema peponi Amina

Wednesday, December 28, 2011

KIONGOZI WA KOREA KASKAZINI KIM JONG IL AZIKWA!!


Kiongozi wa zamani wa Korea Kaskazini Kim Jong Il amezikwa leo kwenye mazishi ambayo yameongozwa na mwanaye Kim Jong Un huku kukiwa hakuna kiongozi yoyote kutoka mataifa mengine ambaye amehudhuria maziko hayo!! Maelfu ya wananchi wa Korea Kaskazini wameshiriki kwenye shughuli hizo huku weni wao wakiomboleza kwa kilio!!

Tuesday, December 27, 2011

ARSENAL YABANWA MBAVU EMIRATES NA KUAMBULIA SARE!!



Klabu ya Arsenal maarufu kama Washika Magobole waJiji la London wamebanwa mbavu katika mchezo wa Ligi Kuu Nchini England baada ya kuambulia sare ya bao 1-1 mbele ya Wolves!! Kutokana na matokeo hayo Klabu ya Arsenal imeendelea kujiweka mbali na mbio za Ubingwa msimu huu!!

JONNY EVANS KUKAA NJE KWA MAJUMA MAWILI!!


Kocha Mkuu wa Manachester United Sir Alex Ferguson amesema watamkosa Beki wao wa kati Jonny Evans kwa majuma mawili hadi matatu na hivyo kumfanya kuwa na majeruhi kumi na moja wa kikosi chake!! Evans aliumia kwenye mchezo dhidi ya Wigan Athletic uliopigwa hiyo jana!! Wachezaji wengine ambao ni majeruhi kwa sasa ni Nemanja Vidic, Darren Fletcher, Rio Ferdinand, Michael Owen, Anderson, Tom Cleverley, Fabio Da Silva, Phil Jones, Ashley Young na Chris Smalling!!

TAHADHARI YA KUIBUKA KWA MAFURIKO TENA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM!!

Monday, December 26, 2011

MAN UTD YASHINDA HUKU LIVERPOOL, CHELSEA NA MAN CITY ZIKIBANWA MBAVU!!






Ligi Kuu nchini Uingereza imeendelea na kushuhudia Manchester United ikifanikiwa kuibuka na ushindi wa magoli 5-0 na kuikaribia Manchester City kilele baada ya timu hiyo kulazimishwa sare ya bila kufungana na Wes Bromwich Albion!! Chelsea walikwenda sare ya goli 1-1 mbele ya Fulham wakati Liverpool walibanwa mbavu na Blackburn Rovers baada ya kutoka sare ya goli 1-1!!

Wednesday, December 21, 2011

MANCHESTER UNITED NA CITY WAKABANA KOO LIGI KUU NCHINI UINGEREZA!!





Manchester Unite imevuna ushidni wa magoli 5-0 mbele ya Fulham wakati Manchester City wakiisambaratisha Stoke City kwa magoli 3-0!! Arsenal nayo iliendelea kuvuna ushindi baada ya kuifunga Aston Villa kwa magoli 2-1!! Newcastle United imeendelea na wakati mgumu baada ya kufunga magoli 3-2 na West Bromwich Albion!! Everton ilishinda kwa goli 1-0 mbele ya Swansea huku Wigan wakitoka sare tasa na Liverpool huku QPR wakipata kichapo cha nyumbani mbele ya Sunderland!!

RAIS KIKWETE ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA WALIOFIKWA NA VIFO KUTOKANA NA MAFURIKO DSM!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Said Meck Sadiq kuomboleza vifo vya watu 13 ambao wamepoteza maisha katika mafuriko makubwa yaliyotokana na mvua ambazo zimekuwa zinanyesha tokea Jumanne, Desemba 20, 2011.

Aidha, Rais Kikwete amempa pole Mkuu huyo wa Mkoa kutokana na uharibifu mkubwa wa nyumba, makazi na mali nyingine za wananchi uliosababishwa na mvua hizo ambazo pia zimesababisha uharibifu wa miundombinu.

Rais Kikwete pia ameuelekeza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kusaidiana na taasisi na vyombo vyenye uzoefu wa maafa kushirikiana katika kuendelea kuokoa maisha ya watu, kusaidia waliozingirwa na mafuriko na kuwahifadhi na kuwasaidia wale wote waliopoteza nyumba na makazi kutokana na mafuriko hayo.

Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Sadiq: “Nimepokea kwa masikitiko habari za vifo vya wenzetu 13 vilivyotokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa ambayo sote tumeishuhudia katika Mkoa wa Dar es Salaam tokea jana. Nakutumia wewe rambirambi zangu kutokana na vifo hivyo, na kupitia kwako kwa familia, ndugu na jamaa waliopoteza wapendwa wao katika balaa hili la mafuriko. Wajulishe kuwa msiba wao ni msiba wangu, naelewa machungu yao na niko nao katika hali ya sasa ya maombolezo. Mungu aziweke pema peponi roho za marehemu wote.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Napenda pia kupitia kwako kutoa pole zangu nyingi kwa wote walioumia ama kupoteza mali zao katika mafuriko haya. Wajulishe kuwa moyo wangu uko nao wakati huu wa mazingira magumu.”

“Chini ya usimamizi wako, ningependa kuona uongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na taasisi na vyombo vyenye ujuzi na uzoefu wa kupambana na majanga na dharura za namna hii, kuhakikisha kuwa tunaendelea kuokoa watu ambao bado wamezingirwa na mafuriko, tunawapa matibabu wale walioumia katika mafuriko hayo, na tunawahifadhi na kuwapa huduma za kibinadamu wote waliopoteza nyumba na makazi yao katika mafurikio hayo.”

WATU 13 WAPOTEZA MAISHA JIJINI DAR ES SALAAM KUTOKANA NA MVUA!!



Boti zikitumika kuwaokoa wananchi ambao walikumbwa na mafuriko katika Jiji la Dar Es Salaam. Boti hiyo ilitumika kuwaokoa wakazi wa Jangwani na hata Kigogo ambao walikuwa wamechukuliwa na mafuriko hayo. Mamia ya wananchi hawana makazi kutokana na mvua hizo zilizochangia kuzuka kwa mafuriko huku watu 13 wakipoteza maisha na uharibifu mwingine wa miundombinu ukishuhudiwa!!

MAFURIKO YAENDELEA KUTESA WAKAZI WA DAR ES SALAAM KWA SIKU YA PILI SASA!!





Hali ilivyo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam baada ya mvua kali ikiambatana na radi kuendelea kutikisa Jiji hilo. Mvua hiyo imenyesha kwa saa zaidi ya nne sasa huku mawasiliano ya barabara yakikatizwa na kuchangia watu kushindwa kufika maeneo wanayokwenda!! Jeshi la Polisi nalo linaendelea na zoez la uokozi kwa wale ambao wamekwama kwenye maeneo ya mabondeni!!

Monday, December 19, 2011

RAIS KIKWETE AWAAPISHA MABALOZI WAPYA IKULU LEO!!


Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewaapisha Mabalozi wapya ambao amewateua kwenda kuiwakilisha nchi kwenye mataifa ya ughaibuni. Miongoni wa walioapishwa ni pamoja na Philip Marmo ambaye anakwenda nchini China, Daktari Batlida Salha Burian ambaye anakwenda nchini Kenya. Dokta Deodorus Kamala yeye anachukua nafasi ya kuwa Balozi nchini Ubelgiji. naye Dokta Ladislaus Komba anakwenda kuhudumu nchini Uganda. Mabalozi wengine ni pamoja na Bi Shamim Nyanguga ambaye amepelekwa nchini Msumbiji, Bi Grace J.E. Mujuma ambaye anakwenda nchini Zambia, Mohamed Hamza ambaye anakwenda kuiwakilisha nchi huko Misri na Ali Saleh ambaye amepelekwa Omani.

MBUNGE WA KIGOMA KUSINI DAVID KAFULILA AVULIWA UANACHAMA NCCR-MAGEUZI!!


Halmashauri Kuu ya Chama Cha NCCR-Mageuzi imemtimua uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila kwa madai ya kutaka kukiharibu chama hicho huku wanachama wengine sita wakiingia kwenye mkumbo huo.

Mgombea wa Urais kwenye uchaguzi uliopita Hashim Rungwe ni miongoni mwa waliotimuliwa kwa kosa linalofanana na Kafulila wakitajwa kutaka kukivuruga Chama.

Wanachama hao wanasiku kumi na nne za kukataa rufaa kupinga adhabu ambayo imetolewa na iwapo watashindwa kwenye rufaa yao ni wazi Kafulila atakuwa amepoteza uhalali wa kuwa Mbunge na hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi kulazimika kuitisha Uchaguzi Mdogo.

MAN CITY YAREJEA KILELENI WAKATI MAN UTD IKISHINDA DHIDI YA QPR!!




Klabu ya Manchester City imefanikiwa kurudi kileleni mwa Ligi Kuu Nchini Uingereza baada ya kuifunga Arsenal kwa goli moja kwa nunge!! Goli la David Silva ndiyo lilipeleka kilio kwa Washika Bunduki wa Jiji la London!! Manchester United ilifanikiwa kupata ushindi wa magoli 2-0 mbele ya Queens Park Rangers!!

BARCELONA YATWAA UBINGWA WA KLABU BINGWA DUNIANI!!


Klabu ya FC Barcelona imefanikiwa kutetea Ubingwa wake wa Klabu Bingwa ya Dunia baada ya kuifunga Santos kwa magoli 4-0!! Katika mchezo wa fainal uliopigwa nchini Japan katika Jiji la Yokohama ulishuhudia Lionel Messi akifanikiwa kufunga magoli mawili huku mengine yakifungwa na Xavi Hanandez na Cesc Fabregas!!

KIONGOZI WA KOREA KASKAZINI KIM JONG IL AFARIKI DUNIA!!


Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Il amefariki Dunia akiwa na umri wa miaka 69 baada kuugua ugonjwa wa moyo. Kiongozi huyo ambaye aliingia madarakani mwaka 1994 baada ya kifo cha Baba yake Kim Jong Sung. Nafasi yake itachukuliwa na mwanae Kim Jong Un!! Mazishi yake yatafanyika tarehe 28 December 2011!!

Monday, May 23, 2011

CARLO ANCELOTTI ATUPIWA VIRAGO CHELSEA!!



Kocha wa Chelsea Carlo Ancelotti ametupiwa virago na Chelsea baada ya kile kinachotajwa kuwa ni kushindwa kwake kutimiza malengo ambayo yalikuwa yamewekwa na tajiri wake!! Ancelotii anaondoka na sasa kibarua kinabaki kwa Chelsea kusaka Kocha mwingine!!

Monday, May 9, 2011

HOTUBA YA RAIS KIKWETE KWENYE MAFUNZO ELEKEZI!!!

HOTUBA YA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA AKIFUNGUA MAFUNZO ELEKEZI KWA
VIONGOZI NA WATENDAJI WAKUU WA SERIKALI
TAREHE 9 MEI, 2011

Mheshimiwa Waziri Mkuu;
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Wazee Wetu, Mzee Cleopa Msuya na Mzee Pius Msekwa;
Ndugu Mawaziri;
Ndugu Naibu Mawaziri;
Ndugu Makatibu Wakuu;
Ndugu Naibu Makatibu Wakuu;
Wakuu wa Vyombo vya Dola;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Ukaribisho
Nianze kwa kuwakaribisha nyote kwenye Semina Elekezi inayojumuisha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu. Kama lilivyo jina lake, Semina hii ni ya kuelekezana juu ya namna tutakavyotimiza majukumu yetu katika Serikali. Tulikuwa na Semina kama hii mwaka 2006. Imetusaidia kupata mafanikio tuliyoyapata miaka mitano iliyopita. Naamini na Semina hii itatusaidia kupata ufanisi tunaoutarajia na ambao wananchi wanautarajia kutoka kwetu.
Ndugu Viongozi na Watendaji wa Serikali;
Niruhusuni niombe radhi kwa niaba ya Viongozi Wakuu wawili kutokuwa nasi siku ya leo. Wa kwanza ni Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal na wa pili ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein. Makamu wa Rais yuko Uturuki kuniwakilisha katika LDC Summit. Mwanzoni nilikubali kushiriki kwenye LDC Summit, lakini baada ya tarehe za Semina yetu kubadilika na kuangukia kwenye tarehe za Mkutano huo nikawa sina namna ila kutuma mwakilishi.
Kwa uzito wa mkutano wenyewe na matumaini ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na wenyeji wetu kuhusu ushiriki wa Tanzania nikaona Makamu wa Rais atuwakilishe. Makamu wa Rais amefuatana na Mheshimiwa Prof. Anna Tibaijuka, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim. Najua watakosa uhondo, lakini tutawapatia DVD ya Semina wataona na kusikia tuliyozungumza. Mheshimiwa Rais wa Zanzibar amebanwa na vikao vya maandalizi ya bajeti.
Madhumuni ya Semina
Ndugu Viongozi,
Katika Semina hii majukumu ya msingi ya Serikali ya utawala, maendeleo na ulinzi na usalama yatafafanuliwa. Pia itaelezwa jinsi kila mmoja wetu anavyohusika nayo na anavyotegemewa kutimiza wajibu wake. Katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge nilitaja malengo 13 ambayo yamejumuisha mambo makuu tutakayoyapa kipaumbele katika Serikali katika miaka mitano hii. Lakini nilikumbusha kuwa yale mambo 13 ni muhtasari wa maelekezo yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Ndugu Mawaziri;
Mtakumbuka kuwa katika mkutano wangu wa kwanza nanyi niliwasisitizia umuhimu wa Ilani ya Uchaguzi kwa kila mmoja wenu na kwa Serikali yetu kwa jumla. Niliwaambia kuwa Ilani ndiyo mkataba mkuu baina ya Chama cha Mapinduzi na wananchi. Utekelezaji wake ndicho kipimo kikuu cha uwezo wetu wa kuongoza, mwaka 2015. Niliwataka kila mmoja wenu atambue ukweli huo na kutengeneza mkakati wa kutekekeleza Ilani kwa yale mambo yanayohusu Wizara yake. Sina shaka kuwa takriban miezi mitano baadae kila mmoja wetu atakuwa amekamilisha kazi hiyo na kuingiza katika mipango ya kazi ya Wizara itakayotekelezwa kuanzia bajeti itakayowasilishwa Bungeni mwezi ujao.
Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;
Siku ile pia nilisisitiza jambo kwa Mawaziri ambalo napenda kulirudia tena leo kwani linawahusu na Makatibu Wakuu. Ninyi kwa pamoja, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu ndiyo timu moja ya uongozi na utawala katika Wizara. Kama viongozi mnategemewa kuonyesha njia kuhusu nini cha kufanya kutekeleza majukumu ya Wizara nilizowakabidhi kuziongoza.
Katika jukumu lenu la utawala mnategemewa kuwa makini na mahiri katika kutumia rasilimali watu, vifaa na fedha za umma mlizokabidhiwa katika kutekeleza majukumu yenu. Mnategemewa kuwa na mipango na mikakati thabiti ya kutekeleza majukumu hayo.
Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;
Katika Wizara kila kitu huanzia na kuishia kwenu. Hakuna mwingine tena kuliko nyie isipokuwa mamlaka zilizo juu yenu; yaani Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais. Kwa sababu hiyo, ili muweze kutimiza kwa ukamilifu wajibu wenu huo hamna budi kwanza kabisa kutambua vyema majukumu yenu na jinsi ya kuyatekeleza. Semina hii ina shabaha ya kusaidia katika hilo. Lakini, njia kubwa zaidi ni ile niliyowaambia siku ile, yaani ninyi wenyewe kufanya bidii ya kujua kwa kusoma, kuona na kufanya shughuli za Wizara zenu kwa makini.
Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu mnatakiwa kuyajua kwa kina mambo yote yanayohusu Wizara mnazoziongoza. Vinginevyo hamtaongoza vizuri. Mtakuwa wababaishaji. Mtashindwa kutoa malengo maana mtakuwa hamjui nini cha kuekeleza, mtashindwa kusimamia mambo, kwa vile hamjui cha kusimamia, mtakuwa hamuonekani mkifanya chochote cha maana kwa sababu hamna jambo la kufanya zaidi ya mambo ya kawaida – routine issues. Mawaziri na Makatibu Wakuu lazima mtoke. Hiyo ndiyo njia bora zaidi ya kujua mambo yahusuyo Wizara yenu na ndiyo njia bora ya kuongoza: kuona wenyewe na kutenda. Itawafanya mjiamini kuelekeza na pia mnaposimama mbele za watu na kusema. Msiwe mangimeza. Tokeni, tembeeni kuona shughuli zenu. Tembeleeni wananchi muwafahamu, wawafahamu, mjue shida zao muwatatulie.
Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;
Ili mjue mambo ya Wizara zenu vizuri lazima mtengeneze utaratibu mzuri wa kupashana habari kuhusu mambo yanayotokea Wizarani. Utaratibu utakaomwezesha kila mmoja kujua kinachoendelea Wizarani. Msipofanya hivyo kuna hatari ya ninyi wenyewe viongozi wakuu mkawa hamjiamini na hata kuwa na kauli tofauti kwa jambo hilo hilo. Mmoja anasema hivi na mwingine anasema vile. Kuna hatari ya kuzuka kutokuelewana miongoni mwenu.
Hii pia ni muhimu sana hasa kwa sababu barua huandikwa kwa Waziri au Katibu Mkuu. Msipotengeneza utaratibu wa kupashana habari Waziri anaweza asijue anachojua Katibu Mkuu na kinyume chake. Na, baya zaidi Naibu Waziri na Naibu Katibu Mkuu wanaweza kuwa gizani kabisa. Naibu Waziri hushikilia Wizara anaposafiri Waziri na ndiye msemaji wa Wizara katika Bunge asipoyajua vyema yanayotokea au mambo yanayohusu Wizara hatakuwa msemaji mzuri na wa kujiamini wa Wizara. Naibu Katibu Mkuu hushikilia ofisi ya Katibu Mkuu anapokuwa hayupo. Hatafanya kazi kwa kujiamini na atashindwa kuamua mambo kwa sababu hana habari ya mambo yanayohusu Wizara. Mambo yatakawia na mengine kukwama kwa sababu hiyo.
Pamoja na kutoa fursa kwa kila mmoja wenu kuona na kujua kinachotokea Wizarani, jengeni utaratibu wa kukutana mara kwa mara kuzungumzia shughuli za Wizara zenu. Itasaidia sana. Ndiyo maana Jeshini kuna Officers Mess kutoa fursa ya maofisa kufahamiana na kuzungumza masuala yahusuyo shughuli zao. Mnaweza kuwa na vikao vya mara kwa mara au hata kunywa chai pamoja. Hata nyie mnaweza kuwa na utaratibu kama huo.
Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;
Narudia kuwakumbusha kwamba msingi wa utendaji Serikalini ni katiba, sheria, kanuni na taratibu. Ni muhimu kwenu kama viongozi mkajielimisha juu ya Katiba, sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazoongoza utendaji kazi katika sehemu zenu za kazi. Uhalali wa maamuzi mtakayoyafanya hupimwa na sheria. Ukifanya maamuzi yanayokinzana na sheria utahojiwa wewe binafsi lakini pia utaibebesha Serikali mzigo wa hasara na fedheha itakayotokana na maamuzi hayo.
Lakini pia maamuzi yasiyofuata sheria yanaweza kuwa na madhara kwa wananchi. Heshimuni Katiba na fuateni sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika utekelezaji wa majukumu yenu. Katika semina hii masuala hayo yatafafanuliwa na kuzungumzwa. Kadhalika uhusiano wa Serikali na mihimili mingine ya dola yani Bunge na Mahakama utafafanuliwa.
Uwajibikaji wa Pamoja
Viongozi Wenzangu;
Wakati wote sisi sote tunapaswa kuzingatia kwamba Wizara ni moja, Serikali ni moja, lengo letu ni moja na hivyo wakati wote lazima tuwe na umoja, mshikamano na kauli moja. Serikali au Wizara isiyokuwa na umoja haiwezi kutimiza wajibu wake ipasavyo. Mawaziri na Makatibu Wakuu wasiokuwa na umoja hawatatimiza wajibu wao ipasavyo. Umoja ni kitu cha msingi sana. Unapokosekana kunakuwepo mifarakano na hatimaye huingia udhaifu katika kuamua na kutenda. Hali hiyo itasababisha wananchi kutohudumiwa ipasavyo na maendeleo yao kuathirika.
Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;
Hakikisheni kuwa katika Wizara zenu kuna umoja. Umoja huo uanzie kwenu nyinyi viongozi wakuu. Aghalabu ninyi mkiwa na umoja Wizara huwa na umoja, ninyi mkifarakana wafanyakazi nao hugawanyika. Kwa upande wa Serikali nako hali kadhalika, lazima Mawaziri wawe na umoja. Iwapo Mawaziri wana umoja, Serikali huwa na mshikamano na nguvu katika kuamua na kutenda. Wakati wote tuhakikishe kuwa tuna umoja na mshikamano miongini mwetu. Tuepuke kauli na matendo yatakayofarakanisha Mawaziri na hivyo kuleta mgawanyiko katika Serikali.
Lazima tukumbuke na kuzingatia dhana ya uwajibikaji wa pamoja. Lazima idhihirike katika ngazi ya Wizara na Serikali kwa jumla. Mawaziri, ninyi ndiyo viongozi wakuu katika Wizara zenu na Makatibu Wakuu ndiyo watendaji wakuu wa Wizara. Nyote mnawajibika katika nafasi zenu kwa maamuzi mnayoyafanya ya kisera na kiutendaji. Hamna budi kushirikiana, kushauriana na kuwekeana staha. Viongozi na watendaji wakuu wa Wizara hamna budi kujenga mahusiano mazuri na uwajibikaji wa pamoja. Haifurahishi kuona Waziri na Katibu Mkuu, au Waziri na Naibu Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu au Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu hawaelewani. Wanasemana na hata wakipingana hadharani, yaani mbele za wafanyakazi. Na baya zaidi pale wanapingana katika vyombo vya habari kuhusu maamuzi au utendaji wa Wizara au Serikali kwa ujumla. Hayo si maadili mema katika taasisi yoyote.
Uzoefu unaonesha kuwa jambo hili hutokea pale ambapo kunakuwa na kuingiliana katika majukumu au kwa kutozingatiwa kwa taratibu na maadili ya uongozi. Lazima ieleweke kuwa tukishaamua jambo kwa pamoja Wizarani au katika Baraza la Mawaziri ni uamuzi wetu sote hata kama wewe ulikuwa na mawazo tofauti. Wote tunao wajibu wa kuunga mkono na kuutetea. Kamwe hatutegemewi kuendelea kuupinga baada ya hapo. Kufanya hivyo ni kukiuka maadili ya uongozi na uwajibikaji wa pamoja. Kama unaona vigumu sana kuuafiki ni bora kutoka. Hairuhusiwi kupinga taasisi ambayo wewe umo ndani kama mmoja wa viongozi wake. Ni vyema hili likaeleweka vyema. Msitupe tabu ya kuulizana maswali na kuwasemea.
Kuwajibika Bungeni
Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;
Dhana hii ya uwajibikaji wa pamoja nayo inahusu pia shughuli za Serikali Bungeni. Miswada ya Serikali ni ya Mawaziri wote mmoja mmoja na kwa umoja wao. Mswada wa Sheria ukiletwa na Waziri mmoja, kila Waziri anao wajibu wa kuunga mkono na kuutetea. Haitegemewi na ni kinyume cha maadili cha hali juu kwa Waziri kupinga mswada wa Waziri mwenzake. Kwa kweli, tabia hii haivumiliki na anayetenda hayo amejitenga mwenyewe na Serikali.
Jambo lingine muhimu kwa Mawaziri ni kutambua kuwa kuhudhuria vikao vya Bunge ni jambo la lazima kama ilivyo kwa vikao vya Baraza la Mawaziri. Si jambo la hiari. Ni lazima Waziri ahudhuria vikao vya Bunge bila ya kukosa labda awe na sababu kubwa inayoelezeka na kukubalika. Kutembelea jimbo lako la uchaguzi ni jambo la lazima lakini siyo sababu ya kukufanya ukose vikao vya Bunge au Baraza la Mawaziri.
Uwajibikaji Kikazi na Kimaadili
Ndugu Viongozi;
Tulipokutana mara ya kwanza kule Dar es Salaam baada ya kuunda Serikali, nilizungumzia uadilifu. Napenda, leo tena kusisitiza jambo hili kwa sababu ya umuhimu wake. Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu ni viongozi wakubwa sana Wizarani, Serikalini na katika jamii. Kiongozi anatakiwa kuwa mfano mwema (role model) kwa watu anaowaongoza. Watu watamani kuwa kama yeye au kuishi kama yeye. Watu watamani kumuiga kwa uchapakazi wake, kwa tabia njema na matendo mema. Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Mkuu wasinyooshewe kidole kwa uvivu, uzembe, wizi, ubadhirifu wa mali ya umma, vitendo vya utovu wa uadilifu kama vile wizi, ulevi wa kupindukia, uzinzi, majigambo, ubabe na uonevu na dhuluma. Kuwa hivyo ni kupungukiwa sifa za msingi za uongozi. Huwakatisha tamaa wananchi na kuwafanya wapoteze imani na Serikali yao.
Uwajibikaji kwa Wananchi
Ndugu Viongozi;
Lazima tukumbuke kwamba Serikali yetu imewekwa madarakani na wananchi kwa ajili yao na siyo kwa ajili ya viongozi tuliopo madarakani. Serikali ipo kwa ajili ya kuwahudumia na kutatua matatizo yanayowakabili wananchi na kuwaletea maendeleo. Wananchi wanapenda kuona Serikali yao ina viongozi na watumishi waadilifu, wachapakazi hodari, wanaowasikiliza, wanaojali shida zao na wepesi wa kushughulikia na kutekeleza maamuzi mbalimbali ya Serikali. Ni wajibu wetu kama viongozi wakuu na watendaji wakuu kutimiza matarajio hayo ya wananchi.
Kuisemea Serikali
Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;
Moja ya mada ya semina hii inahusu mawasiliano ya Serikali. Kwa maneno mengine kuisemea Serikali. Hili ni jambo ambalo tuna udhaifu mkubwa. Sijui kwanini hatuwi wepesi kuyasemea mafanikio mengi tuliyoyapata tukaacha wasiotutakia heri wanaosema hatukufanya kitu wasikike mpaka waonekane wanasema kweli. Mwanazuoni mmoja bingwa wa habari aliwahi kusema kuwa “kufanya kitu bila kuufahamisha umma ni sawa kama kitu hicho hakijafanyika.” Mwingine anasema kuwa uongo ukisemwa mara nyingi hugeuka kuwa ukweli.
Uzoefu wa miaka mitano umeonyesha kwamba tumefanya mambo mengi lakini wananchi hawakuelezwa ipasavyo. Pia, tumeacha upotoshaji kufanywa bila ya kusahihishwa au kuchelewa sana kusahihishwa. Hivyo basi, wananchi wamekuwa wakijikuta wakiamini uongo na kulaumu au hata kuichukia Serikali kwa mambo ambayo ni potofu. Wangeambiwa ukweli mapema hawangefikia hapo. Lazima upungufu huo tuondokane nao. Lazima tuwe makini na hodari kuelezea shughuli zinazofanywa na Serikali, mafanikio yanayopatikana na changamoto zilizopo.
Aidha, tuwe wapesi kusahihisha upotoshaji wowote unaofanywa dhidi ya Serikali. Kutokufanya hivyo kumetugharimu sana. Hatuwezi kuendelea hivi wakati ninyi viongozi mpo, watu Mawizarani wapo, rasilimali zipo na vyombo vya habari vipo vinasubiri kupewa habari.
Ukuzaji Uchumi na Maendeleo
Ndugu Viongozi;
Nilieleza awali kuwa mojawapo ya majukumu ya msingi ya Serikali ni kuleta maendeleo ya nchi na watu wake. Hususan Serikali inalo jukumu la kukuza uchumi na kuwapatia wananchi huduma za msingi za kiuchumi na kijamii kwa lengo la kuongeza mapato na kuboresha hali ya maisha ya Watanzania. Hii ni kazi ya msingi sana kwa Serikali kufanya na lazima kufanikiwa. Kazi hiyo ndiyo moja ya sababu na shabaha pana ya Serikali kuwepo na sisi wote kuwapo. Kwangu mimi na ninyi wenzangu kuleta maendeleo na kukidhi matumaini ya Watanzania ni changamoto na mtihani wetu mkubwa sana.
Katika Semina hii masuala ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo yamepewa nafasi ya kuzungumzwa kwa upana. Pamoja na watoa mada wa ndani, tunawashukuru marafiki zetu wa Benki ya Dunia kwa kutuletea mabingwa wa uchumi na maendeleo kuja kuzungumza nasi. Naamini uzoefu na mifano ya nchi mbalimbali kuhusu kufanya mageuzi ya kiuchumi na kujiletea maendeleo kutatusaidia kuimarisha na kuboresha hatua tunazochukua nchini.
Ndugu Viongozi;
Hakika tumefanya mengi na mafanikio yanaonekana, lakini tunayo kazi kubwa sana mbele yetu ya kufanya. Tanzania ni miongoni mwa nchi 49 maskini sana duniani. Shabaha yetu kubwa ni kutoka hapa tulipo sasa na kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Yaani, tutoke kwenye pato la wastani la USD600 la sasa hadi pato la USD1,500 mpaka USD3,000 mwaka huo.
Niliamua na kuelekeza kuwa yafanyike mapitio ya Vision 2025 na tuigawe miaka 15 iliyosalia katika mafungu matatu ya miaka mitano mitano. Tuwe na mipango ya maendeleo ya miaka mitatu tukianzia na huu unaowiana na kipindi chetu cha uongozi. Hii itatuongoza vizuri zaidi kuelekea na kufikia lengo. Kazi ya mapitio inaendelea kama ilivyo ile ya matayarisho ya mpango wa kwanza wa maendeleo. Katika Semina hii tutapata maelezo ya awali ya kazi inayoendelea.
Ndugu Viongozi na Ndugu Washiriki;
Tunao pia Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) ambao tumekuwa tunautekeleza tangu mwaka 2005. Tumekamilisha MKUKUTA I na hivi sasa tupo kwenye utekelezaji wa MKUKUTA II ambao utakamilika mwaka 2015. MKUKUTA umetusaidia sana katika kuainisha maeneo ya kipaumbele katika bajeti. Kwa ajili hiyo, imesaidia katika jitihada za Serikali za kupunguza umaskini na kuinua hali ya maisha ya Watanzania. Bila ya shaka tutapata nafasi ya kuelezwa maudhui ya MKUKUTA II ili tuelewe namna ya kuwianisha shabaha zake na shughuli tunazozifanya katika Wizara zetu.
Ndugu Mawazirina Ndugu Makatibu Wakuu;
Kuinua hali ya maisha ya Watanzania kuna sura mbili: upande mmoja kuna kuongeza kipato chao. Yaani wasiokuwa na shughuli wapate shughuli za kufanya (kukuza ajira) na wale wenye shughuli zikue na kuimarika ili mapato yao yaongezeke. Mazungumzo yahusuyo kukuza uchumi yatatoa fursa ya kuyajadili mambo haya. Upande wa pili unahusu upatikanaji wa huduma za kiuchumi na huduma za kijamii zilizo bora na zinazotosheleza mahitaji. Wananchi wanataka kuona miundombinu hasa ya barabara zinajengwa na kuimarishwa, umeme wa uhakika pamoja na huduma za maji, afya na elimu zinapatikana kwa kiwango kinachokidhi mahitaji na ubora unaostahili.
Tumejitahidi kwa kiasi kikubwa kuongeza upatikanaji wa huduma hizo katika miaka mitano hii. Lakini, kazi iliyo mbele yetu bado ni kubwa. Upande mmoja bado tunayo kazi ya kuwafikia wale ambao huduma hizo hazijawafikia. Na, upande mwingine tunayo kazi ya kuhakikisha ubora na uendelevu wa huduma pale inapopatikana. Kuyafanya hayo ni wajibu wa msingi wa Serikali, kinachotakiwa ni kujipanga vyema kwa mipango na rasilimali watu, vifaa na fedha ili kutimiza wajibu huo.
Mapato na Matumizi ya Serikali
Ndugu Viongozi;
Uwezo wa Serikali kutekeleza majukumu yake unategemea sana kuwepo kwa rasilimali fedha na jinsi fedha hizo zinavyotumika. Upatikanaji wa rasilimali fedha unategemea ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Serikali inapata mapato yake kupitia kodi na tozo mbalimbali. Kodi ndicho chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali na chombo kikubwa cha ukusanyaji wa mapato hayo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Katika miaka mitano hii mafanikio makubwa yamepatikana na mapato yameongezeka karibu mara tatu kutoka shilingi 177 bilioni kwa mwezi hadi shilingi 430 bilioni kwa mwezi hivi sasa.
Pamoja na nyongeza hiyo bado tunao uwezo wa kuongeza zaidi. Kuna watu wengi ambao bado hawajafikiwa na wigo wa kodi. Laiti wangefikiwa mapato ya Serikali yangekuwa makubwa zaidi ya ilivyo sasa. Tutafanyaje tufanikishe hilo ni changamoto yetu sote Serikalini. Tufanye nini ili tuzibe mianya inayovujisha mapato ya Serikali ni swali ambalo sote katika Serikali hatuna budi kutoa jibu muafaka. Kwa upande wa tozo mbalimbali karibu kila Wizara inazo tozo za namna hiyo. Wengi wenu hamjafikia hata theluthi moja ya malengo. Tutafanyaje ili tufikie malengo na kuyavuka ni swali ambalo kila mmoja wetu anatakiwa kujiuliza na kutoa majibu sahihi.
Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;
Sote tunajua kuwa licha ya tozo na kodi, chanzo kingine cha mapato ya Serikali ni mikopo na misaada kutoka Mabenki, Mataifa Rafiki, na Mashirika ya Fedha ya Kimataifa. Tumepata misaada na mikopo mingi ya kutoka nje katika kipindi kilichopita na muelekeo ni kuwa tutaendelea kupata zaidi katika miaka mitano ijayo. Tunatambua haja na hoja ya kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo kutoka nje kwa kuongeza mapato yetu ya ndani. Katika miaka mitano hii tumeendelea kupunguza utegemezi lakini nia yetu sote iwe kupunguza zaidi. Naamini tutafika kwenye shabaha hiyo iwapo tutaongeza mapato ya ndani. Naomba tuzungumzie namna ya kufikia shabaha hiyo.
Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;
Usimamizi wa matumizi ya fedha tunazokusanya kama mapato ni jukumu jingine kubwa kwetu sote. Tuna wajibu wa kuhakikisha kuwa fedha za walipa kodi zinatumika ipasavyo kuwaletea maendeleo wananchi. Katika kudhibiti matumizi ni muhimu kuelewa na kusimamia sheria, taratibu na kanuni za fedha na manunuzi ya umma kwa ufanisi wa hali ya juu. Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zinaonyesha kuongezeka kwa ubora lakini bado tunayo kazi ya kufanya kufikia kiwango cha kusema sasa tunapumua. Bado kuna makosa mengi katika kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za mapato na matumizi ya fedha za umma. Nataka tuzungumze kwa dhati tutafikaje kwenye ufanisi wa hali ya juu kwenye eneo hilo. Hali hii hatuwezi kuiacha iendelee kuboreka kwa kasi ndogo iliyopo sasa.
Viongozi na watendaji wakuu wa Serikali, mnatakiwa kuwa mfano kwa wafanyakazi mnaowaongoza kwa kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma. Hakikisheni bajeti hazikiukwi, fedha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na sheria na kanuni za fedha zinaheshimiwa. Niliagiza Kamati za Fedha ziundwe katika kila Wizara na Idara za Serikali zinayojitegemea. Je zimeundwa? Je zinafanya kazi? Hakikisheni zipo hai na zinatimiza wajibu wake. Zitasaidia sana kwa upande wa kuongeza mapato na kudhibiti matumizi katika Wizara.
Ulinzi na Usalama
Ndugu Mawaziri na Ndugu Makatibu Wakuu;
Katika semina hii tutapata nafasi ya kuzungumzia masuala ya ulinzi na usalama. Tutawasikiliza Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhusu usalama wa nchi. Pia tutamsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na Kamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi kuhusu uadilifu wa viongozi.
Maandalizi ya Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru
Ndugu Viongozi;
Kama mnavyofahamu mwaka huu tunaadhimisha miaka hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara. Tumeazimia kusherehekea siku hii kwa uzito unaostahili. Niliagiza tufanye mambo kadhaa muhimu ambayo ni pamoja na kufanya tathmini ya kina ya mafanikio tuliyoyapata, katika juhudi zetu za kujiletea maendeleo. Aidha, niliagiza Wizara, idara na taasisi za Serikali na hata sekta binafsi zifanye tathmini ya shughuli zao na kuandika vitabu ili kuhifadhi kumbukumbu hizo muhimu kwetu na kwa vizazi vijavyo.
Vile vile niliagiza yafanyike maonesho maalum katika Uwanja wa Maonyesho wa Julius Nyerere hapa Dar es Salaam na kote mikoani kwenye viwanja vya maonesho, kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali katika miaka 50 tangu Uhuru wa Tanzania Bara. Kwa kuwa tunakaribia nusu ya mwaka huu, ni vema sasa kukumbushana kuendelea na maandalizi ya sherehe hizo. Ni matumaini yangu kwamba kila Wizara inakaribia kukamilisha tathmini hiyo. Walio nyuma sana waongeze kasi. Tuliazimia pia kuwa tuanzishe mchakato wa kuipitia Katiba yetu. Tumeanza, lakini kuna upotoshaji mkubwa, lakini wajibu wetu sote tuliopo hapa kukabili hila na njama hizo chafu. Naamini tutafika salama. Kinachotakiwa ni mshikamano na umoja miongini mwetu.
Hitimisho
Ndugu Viongozi Wenzangu,
Ni matumaini yangu kwamba maneno haya ya utangulizi niliyosema, yatatupatia msingi wa tafakuri katika mijadala na mafunzo tutakayopatiwa katika siku nne zijazo hasa katika maeneo makuu ya semina ambayo ni pamoja na mfumo wa utawala na utendaji; uchumi na maendeleo; utawala bora; ulinzi na usalama; muungano; na masuala mtambuka.
Nimeambiwa kwamba semina hii itaendeshwa kwa utaratibu wa mihadhara kwa ajili ya kuwasilisha mada pamoja na majadiliano ya pamoja. Pia nimearifiwa kuwa kutakuwepo majadiliano katika vikundi ili kuchambua kwa undani zaidi mada zilizowasilishwa. Hivyo, rai yangu kwenu nyote muwe tayari kushiriki kwa ukamilifu katika majadiliano kwenye mihadhara kwa ukweli na uwazi bila kujali tofauti ya nyadhifa zenu. Wote muwe huru kutoa maoni yenu. Ndiyo maana tuko hapa.
Ndugu Viongozi,
Nawashukuru watoa mada waliokubali kuchangia ujuzi na uzoefu wao nasi. Baada ya kusema hayo sasa napenda kutamka kwamba Semina Elekezi kwa Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefunguliwa rasmi.

MANCHESTER UNITED YAKARIBIA UBINGWA NCHINI UINGEREZA!!






Ushindi wa magoli 2-1 iliyoupata Manchester United mbele ya Chelsea umeifanya klabu hiyo kukaribia kutwaa taji lake la kumi na tisa la Ligi Kuu nchini Uingereza. Kwenye mchezo huo mkali uliopigwa Old Trafford umeshuhudia Manchester ikipata magoli yake kupitia Javier Hernandez na Nemanja Vidic huku Frank Lampard akifunga goli la Chelsea!! Kwa sasa Manchester United iliyobakiwa na michezo miwili inahitaji pointi moja kutwaa Ubingwa!!

Thursday, May 5, 2011

MANCHESTER UNITED YAKAMILISHA SAFARI YA WEMBLEY!!!




Klabu ya Manchester United imefanikiwa kutinga katika Fainal ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya baada ya kuifunga Schalke 04 kwa magoli 4-1!! Kwa matokeo hayo Manchester United imefanikiwa kuiondosha Schalke 04 kwa magoli 6-1!! Kocha Mkuu wa Man Utd Sir Alex Ferguson amekitaka kikosi chake kutowahofia wapinzani wao Barcelona ambao watakumbana nao huko Wembley tarehe 28 May!!

Wednesday, May 4, 2011

RAIS KIKWETE KWENYE MKUTANO WA KIUCHUMI HUKO SAUZI!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atakuwa mgeni maalum katika mjadala wa kimataifa kuhusu Visheni Mpya ya Kilimo katika Afrika (Achieving Africa’s New Vision for Agriculture) utakaofanyika mjini Cape Town, Afrika Kusini, Jumatano, Mei 4, 2011.

Rais Kikwete pia atatembelea Kituo cha Kimataifa cha Biashara (World Trade Centre) mjini humo humo kuona maandalizi yanayofanywa kwa ajili ya kuanzisha kituo kama hicho nchini Tanzania.

Aidha, kesho hiyo hiyo, Rais Kikwete atashiriki katika mjadala maalum wa maandalizi ya kuanzishwa kwa Soko la Mazao nchini (Commodity Exchange) ambalo maandalizi yake yanafanywa kwa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia (WB).

Rais Kikwete atashiriki katika shughuli hizo muhimu kwa uchumi na maendeleo ya Tanzania ikiwa sehemu ya ushiriki wake katika Mkutano wa Uchumi Duniani – Kanda ya Afrika (World Economic Forum-Africa) unaofanyika mjini Cape Town, Afrika Kusini.

Mwaka jana, mkutano huo ulifanyika mjini Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika nje ya mji wa Cape Town katika historia yake.

Rais Kikwete ameondoka nchini Jumanne, Mei 3, 2011, kwenda Cape Town kwa ajili ya mkutano huo wa siku mbili ambako pia atashiriki katika shughuli nyingine tatu kuhusu uchumi na maendeleo.

Washiriki wengine wa mkutano wa Visheni Mpya ya Kilimo katika Afrika, ambako Rais Kikwete atakuwa mgeni maalum, ni pamoja na viongozi mbalimbali duniani wa serikali, biashara na uchumi, mashirika ya kimataifa, mashirika yasiyokuwa ya kimataifa, wasomi na vyama vya wakulima duniani.

BARCELONA WATANGULIA WEMBLEY!!







Klabu ya Barcelona imefanikiwa kutinga hatua ya Fainal ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya baada ya kuoondoa kwenye mashindano Real Madrid kwa kwenda sare ya 1-1. Mchezo huo umetawaliwa na lwama lukuki kutoka kwa wachezaji wa Real Madrid ambao wanashutumu maamuzi!!

Monday, May 2, 2011

MAREKANI YATANGAZA KIFO CHA OSAMA BIN LADEN!!!




Rais wa Marekani, Barack Hussein Obama ametangaza kifo cha Kiongozi wa mtandao wa Al Qaeda Osama Bin Laden ambacho kimetokea nchini Pakistan!! Rais wa Marekani ametangaza kuwa Haki imepatikana kutokana na kifo hicho!! Taarifa kutoka Vyombo vya Habari vya Marekani zinaeleza kuwa tayari Mwili wa Osama Bin Ladeba ameshazikwa Baharini!!

HOTUBA YA RAIS KIKWETE KWENYE MEI MOSI HUKO MOROGORO!!

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWENYE KILELE

CHA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI,

MEI MOSI, 2011 MOROGORO



Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA),

Ndugu Ayoub Omari Juma;

Mheshimiwa Jaji Mkuu;

Mheshimiwa Gaudensia Kabaka (Mb) Waziri wa Kazi na Ajira;

Mhe. Col Issa Machibya, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro;

Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge Mliopo Hapa;

Ndugu Alexio Musindo, Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO)

Kanda ya Afrika Mashariki;

Kaimu Katibu Mkuu, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi ,

Ndugu Nicholaus Mgaya;

Waheshimiwa Mabalozi Mliopo Hapa;

Mwenyekiti wa, Chama cha Waajiri Tanzania (ATE),

Dr. Aggrey Mlimuka;

Wawakilishi wa Vyama vya Siasa na Serikali;

Ndugu Wafanyakazi na Wananchi Wenzangu;

Mabibi na Mabwana:



Shukrani

Nakushukuru sana ndugu Ayoub Omari Juma, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika sherehe za mwaka huu za kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani. Hongereni kwa maandalizi mazuri ya sherehe hii ambayo naambiwa yamesimamiwa na Chama cha Walimu Tanzania. Si ajabu yamefana kiasi hiki kwani tusingetegemea kitu pungufu kuliko hiki kutoka kwa Walimu.

Napenda pia kutoa shukrani na pongezi kwa wenyeji wetu, viongozi na wananchi wa mkoa wa Morogoro wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huu Lt. Col. Issa Salehe Machibya. Tunawashukuru kwa mapokezi mazuri na kazi kubwa na nzuri waliyofanya ya kufanikisha sherehe hizi. Waswahili wanasema “usione vinaelea vimeundwa“ na waundaji si wengine bali ni viongozi na wananchi wa Manispaa ya Morogoro. Tunawashukuru na kuwapongeza sana.

Poleni kwa Msiba

Ndugu Rais wa TUCTA;

Ndugu Wafanyakazi;

Narudia tena kuwapeni pole kwa msiba mkubwa uliowakuta tarehe 4 Aprili, 2011 kutokana na kifo cha Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli marehemu Sylvester Rwegasira. Kifo chake cha ghafla ni pigo kubwa siyo tu kwa familia yake iliyopoteza mlezi na wafanyakazi waliopoteza kiongozi mahiri, bali pia kwa taifa letu kwa jumla. Sote tumepoteza mtu muhimu. Tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe mapumziko mema. Amin.

Pongezi kwa Wafanyakazi Bora

Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;

Niruhusuni nitumie fursa hii, pia, kuwapongeza wafanyakazi waliotunukiwa tuzo za ufanyakazi bora siku ya leo. Wahenga wamesema, “Chanda chema huvishwa pete”. Wenzetu leo wamevishwa pete ya ushindi inayotambua uchapakazi wao, ufanisi wao na nidhamu yao kazini. Wakati tunawapongeza kwa ushindi nawaomba, wao wenyewe, wachukulie tuzo walizopata kuwa ni changamoto ya kuwataka waongeze bidii zaidi kazini ili waendelee kuwa wafanyakazi wa mfano kwa wengine. Naomba waelewe kuwa wapo wenzao wengi wazuri ambao hawakubahatika kwa sababu nafasi ni moja tu. Kwa wafanyakazi wengine tuzo walizopata wenzenu iwe kichocheo kwenu kuongeza bidii na nidhamu kazini ili mwaka ujao nanyi muwe wapokea tuzo. “Inawezekana, timiza wajibu wako”.

Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Waajiri;

Utaratibu huu wa kutambua na kutunuku utendaji kazi mzuri wa wafanyakazi ni jambo jema. Unasaidia kuongeza ari ya kazi na ufanisi kazini. Aidha, huhamasisha wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na maarifa. Lazima tuudumishe na kuuboresha hasa kwa aina ya zawadi wanazopata wafanyakazi bora.

Kauli Mbiu ya Mwaka Huu

Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;

Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Gaudencia Kabaka kwa maelezo yake ya utangulizi. Yameweka msingi mzuri kwa mimi kuweka lami. Aidha, nakushukuru sana Rais wa TUCTA kwa maneno yako ya hekima ya kunikaribisha kuzungumza na hadhara hii. Nawashukuru sana kwa risala yenu iliyosomwa kwa ufasaha na Kaimu Katibu Mkuu wa TUCTA, Ndugu Nicolas Mgaya. Risala yenu imejitosheleza kwa hoja na ina ushauri mwingi mzuri kuhusu mikakati ya kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi. Napenda kuwahakikishia kuwa tumeupokea kwa mikono miwili ushauri huo na tutaufanyia kazi.

Nakubaliana na ujumbe wa kauli mbiu yenu ya mwaka huu kwamba “Serikali isipojali haki zenu, wafanyakazi watakuwa watumwa ndani ya nchi yao”. Ni ukweli uliowazi kwamba Serikali inao wajibu wa kulinda haki za wafanyakazi nchini. Lakini ni kweli pia kwamba wajibu wa kulinda haki za wafanyakazi hauko mikononi mwa Serikali pekee. Upo pia kwa waajiri na wafanyakazi wenyewe kupitia au kwa kuongozwa na vyama vyao. Mimi naamini, wote tukitimiza wajibu wetu ipasavyo, tutaweza kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowakabili wafanyakazi hapa nchini.

Ndugu Rais wa TUCTA;

Napenda kuwahakikishieni kuwa Serikali inatambua ukweli huo na wajibu wake huo. Serikali yetu na zile za awamu zilizopita zimekuwa zinachukua hatua za kulinda na kuendeleza maslahi ya wafanyakazi. Viwango vya mafanikio vimekuwa vinapishana. Yapo mambo ambayo tumeweza kupata mafanikio makubwa na yapo ambayo mafanikio yake si makubwa sana. Hata hivyo, juhudi zimekuwa zinaendelea. Hakuna upuuzaji na wala hakuna upungufu wa utashi wa kisiasa wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili wafanyakazi.

Ndugu Wafanyakazi,

Utashi wa Serikali katika kutekeleza wajibu wake wa kulinda haki za wafanyakazi nchini umejidhihirisha wazi kupitia hatua za kisheria na za kiuchumi ambazo imekuwa inatekeleza. Kwa upande wa sheria, napenda kutambua sheria tatu ambazo zipo kwa ajili ya kulinda na kuendeleza haki na maslahi ya wafanyakazi nchini. Sheria hizo ni: Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2001, Sheria ya Taasisi za Kazi ya mwaka 2004 na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.

Ninyi viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi mnatambua vyema kuwa katika sheria hizi haki na wajibu wa wafanyakazi na waajiri vimeainishwa vizuri. Aidha, utaratibu na mifumo ya kulinda haki hizo na uhusiano na mawasiliano baina yao imefafanuliwa vyema. Vile vile, vyombo vya utekelezaji vimetajwa pamoja na majukumua ya kila chombo.

Ndugu Rais wa TUCTA;

Wakati tunaingia madarakani tulijikuta tunalo jukumu la kihistoria la kuhakikisha kuwa sheria hizo zinatekelezwa kama ilivyokusudiwa. Sheria ya Utumishi wa Umma tuliifanyia marekebisho mwaka 2008 kwa lengo la kuweka utaratibu wa haki zaidi wa ajira na kuwapandisha vyeo watumishi wa umma na kutambua kanuni za mahusiano bora kazini (Code of good conduct).

Kwa sheria ya Taasisi za Kazi na ile ya Ajira na Mahusiano Kazini tulitengeneza Kanuni zake na hivyo kuwezesha kuanza kutumika. Kwa ajili hiyo, mfumo wa ushirikishaji wafanyakazi kuhusu masuala ya mishahara yao na maslahi mengineyo ukaanzishwa rasmi. Miongoni mwa hayo ni kuundwa kwa Baraza la Majadiliano kwa upande wa sekta ya umma, Baraza la Ushauri la Masuala ya Kazi, Uchumi na Kijamii (LESCO), Baraza la Usuluhishi na Upatanishi na Bodi za Mishahara za Kisekta kwa upande wa sekta binafsi. Serikali yetu imekamilisha jukumu lake la kuhakikisha kuwa vyombo hivyo vinaundwa na kufanya kazi yake ipasavyo.

Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;

Haya ni mapinduzi makubwa katika kulinda haki na kuendeleza maslahi ya wafanyakazi nchini. Wafanyakazi wameongezewa fursa ya kutoa maoni yao na kauli yao kusikika katika kujadili viwango vya ujira wao na waajiri wao. Inawezekana si kila wanachotaka wafanyakazi kikatekelezwa au wakakipata kwa kiwango kile walichotaka, lakini hawatoki mikono mitupu. Pia, hoja zao zinakuwa zikisikika na wao wamewasikia waajiri wanachosema. Hakika hatua tuliyofikia si ndogo hata kidogo. Kwa upande wa LESCO, naambiwa kuwa katika Bara la Afrika pengine ni sisi na Afrika ya Kusini tu ndiyo wenye chombo cha namna hiyo.

Wajibu wa Waajiri na Serikali

Ndugu Wafanyakazi;

Katika kulinda na kuendeleza haki za wafanyakazi, waajiri nao wana wajibu wa kuhakikisha kwamba wanafuata matakwa ya sheria za kazi za nchi. Aidha, wanao wajibu wa kudumisha mahusiano mema kazini kwa manufaa yao wenyewe na wafanyakazi wao. Nimesikia kilio cha wafanyakazi kwamba pamoja na kuwepo sheria na mifumo ya kulinda haki za wafanyakazi, wapo baadhi ya waajiri wanapuuza yote hayo. Wapo ambao hawaheshimu sheria zihusuzo ajira wala mishahara na maslahi ya wafanyakazi wao. Wapo pia wanaokataza wafanyakazi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi na hawaruhusu matawi ya vyama hivyo kufunguliwa katika maeneo yao ya kazi.

Ni vyema waajiri wote wakatambua kwamba kufanya hivyo ni kosa la jinai na wanastahili adhabu kali. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, Msajili wa Vyama Huru vya Wafanyakazi na Kamishna wa Kazi msimamie sheria kwa ukamilifu. Wabaneni kisawasawa waajiri wote ili waheshimu sheria za kazi za nchi. Wasiotii wachukuliwe hatua na kuwajibishwa ipasavyo. Mamlaka mnayo, yatumieni. Asiwatishe mtu ye yote kwani sheria zinawalinda. Aidha, wabaneni Maafisa wa Kazi na Wakaguzi wa Kazi watimize ipasavyo wajibu wao. Baadhi yao wanalalamikiwa kuwa hawatendi haki na wanaonekana kuegemea sana upande wa waajiri wanaowakandamiza wafanyakazi.

Mheshimiwa Waziri;

Sisemi kuwa maafisa hao wasiwe wakweli kama wafanyakazi hawana haki. Ninachosema ni kuwa lazima hisia hizi hasi za kuwa wanawapendelea waajiri zifutike kwa wao kutenda haki na waonekane wanafanya hivyo. Msichelee kuwawajibisha wanaopindisha sheria. Si vibaya mkafanya uhamisho wa maofisa wenu waliokaa kituo kimoja kwa muda mrefu. Wahenga wanasema: “mazoea yana taabu”





Wajibu wa Wafanyakazi

Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;

Kwa upande wenu, yaani vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi wenyewe, nanyi mnao wajibu muhimu katika juhudi za kulinda na kuendeleza haki za wafanyakazi. Wajibu wenu wa msingi ni ule wa kudai haki zenu bila woga huku mkizingatia sheria na kununi za kufanya hivyo. Ndiyo maana vyama vya wafanyakazi vipo. Timizeni ipasavyo wajibu wenu huo. Kila kilio kina wenyewe.

Ili malengo yenu yafanikiwe kwa urahisi ni muhimu sana kwenu kuhakikisha kuwa wanachama wenu wanazifahamu vyema sheria na kanuni za kazi zinazowahusu. Mfanyakazi anayejua sheria atafahamu vyema nini cha kudai na akidai vipi ili apate mafanikio. Atafanya hivyo kwa kujiamini na hatimaye atafanikiwa. Kamwe mfanyakazi huyo hatokuwa mtumwa.

Ndugu Wafanyakazi;

Pamoja na hayo lazima vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi kutambua kuwa ulinzi wa haki za wafanyakazi huanzia kwa wafanyakazi kutekeleza vyema wajibu wao na majukumu yao katika kazi zao. Kwa kawaida waajiri huwapenda na kuwaenzi wafanyakazi hodari wa kazi na waaminifu na huchukia wavivu, wezi, wasiokuwa waadilifu na watovu wa nidhamu.

Wafanyakazi wenyewe na Vyama vya wafanyakazi viwakumbushe wafanyakazi kujiepusha na vitendo vya uvivu, utoro, wizi, ubadhirifu na utovu wa nidhamu. Wasipojiepusha na hayo wanaifanya kazi ya kutetea na kulinda haki zao kuwa ngumu kwao na wadau wengine kama sisi. Lazima wakati wote tukumbuke kuwa kila haki ina wajibu.

Ajira na Utandawazi

Ndugu Rais wa TUCTA;

Katika risala yenu mmelizungumzia tatizo la ajira na kukumbusha umuhimu wa kulitafutia ufumbuzi. Nakubaliana nanyi kwamba lipo tatizo kubwa la ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana na ni tatizo linalozidi kukua mwaka hadi mwaka.

Tunalitambua tatizo hili na tunayo mikakati ya kukabiliana nalo. Tulifanikiwa katika lengo letu la kuongeza ajira milioni moja katika miaka mitano iliyopita. Na ukweli ni kwamba tulivuka lengo kwa zaidi ya ajira 330,000. Hata hivyo, tatizo ni kubwa sana kiasi kwamba mafanikio tuliyopata yamekuwa kama vile kuweka tone la maji baharini. Tunautambua ukweli huu na tumejipanga kuendelea kukabiliana na tatizo hili. Lengo letu ni kufanya maradufu ya safari iliyopita. Niruhusuni nielezee mtazamo wetu na hatua tunazokusudia kuchukua kukuza ajira nchini.

Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;

Ajira zinaongezeka iwapo uchumi unakua. Yaani shughuli za uzalishaji mali na utoaji wa huduma zinapoongezeka ndipo watu zaidi wa kufanya kazi huhitajika na hivyo ndivyo ajira zinavyokuzwa. Ni muhimu tutambue pia kwamba kuongezeka kwa uzalishaji mali na utoaji wa huduma kunategemea kuongezeka kwa uwekezaji. Bila ya uwekezaji kuongezeka hakuna uzalishaji mali wala utoaji huduma utakaoongezeka na hivyo hakutakuwepo na ongezeko la ajira.

Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;

Ndiyo maana Serikali yetu imekuwa inatoa msukumo maalum wa kuhamasisha na kuvutia uwekezaji nchini. Tunafanya hivyo kwa upande wa Serikali na ule wa sekta binafsi. Serikali ikiwekeza katika ujenzi wa shule, zahanati, barabara na miradi mingineyo, ajira huzalishwa wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi. Kwa mfano, ujenzi wa sekondari za kata na upanuzi wa shule za msingi, licha ya kuajiri watu wengi wakati wa ujenzi, umewezesha walimu wapya 83,075 kuajiriwa katika miaka mitano iliyopita. Hivi sasa kuna nafasi wazi za walimu 74,996 zinazohitaji kujazwa.

Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;

Kwa upande wa sekta binafsi, mikakati yetu inahusu kutengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza vitega uchumi vyao nchini. Katika miaka mitano iliyopita miradi ipatayo 3,881 yenye thamani ya kiasi cha dola za Marekani milioni 27,330 ilisajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji (TIC). Miradi hiyo ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji inategemewa kuzalisha ajira 444,343. Bado uwekezaji kutoka nje ni mdogo ukilinganisha na fursa za uwekezaji zilizopo nchini. Ni dhamira yetu kuongeza juhudi ya kuvutia wawekezaji zaidi kuja nchini na kuzalisha ajira. Madamu msukosuko wa uchumi wa mwaka 2009 na 2010 ulisababisha kasi ya uwekezaji kupungua duniani na nchini umekwisha, matumaini ya kufanikiwa yapo. Lazima tuchemke kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini.

Ajira ya Wageni

Ndugu Rais wa TUCTA;

Katika risala yenu pia, mmelalamikia wageni kupata ajira zinazostahili kuwa za wananchi. Hayo ni makosa yanayosababishwa na watendaji katika mamlaka za utoaji wa vibali. Nakuomba Mheshimiwa Waziri Gaudencia Kabaka na namuomba Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani kuhakikisha kuwa maofisa wahusika katika Wizara zenu wanatimiza ipasavyo wajibu wao kuhusu suala hili. Ni dhambi kuacha Watanzania hawana ajira na kuwapendelea wageni pale isipostahili. Nawaomba wafanyakazi msichoke kutoa taarifa ili makosa hayo yarekebishwe.

Wawakezaji Wazawa

Ndugu Wafanyakazi;

Kwa wawekezaji wa ndani, mikakati yetu inalenga kutengeneza mazingira mazuri kwa wajasiriamali wadogo, wakati na wakubwa kuvutika na kuwekeza nchini kwao. Miongoni mwa hatua ambazo tumekuwa tunachukua ni pamoja na kupunguza urasimu na kurahisisha taratibu za kupata leseni, kuanzisha miradi na kupata mikopo kutoka asasi za fedha.

Kwa upande wa wajasiriamali wadogo, kwa sababu ya mazingira mazuri tuliyoyatengeneza yamekuwapo mashirika kadhaa yanayotoa mikopo midogo midogo (micro finance schemes). Wengi wamenufaika. Na sisi Serikalini tumeendelea kuimarisha mifuko inayotoa mikopo yenye masharti nafuu kama vile Mfuko wa Vijana na Mfuko wa Wanawake na tumeanzisha Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi.

Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita mifuko hii imekopesha fedha nyingi kwa Watanzania wengi ambao wamewekeza katika shughuli mbalimbali zilizozalisha ajira kwa watu wengi pamoja na wao wenyewe kujiajiri.

Kwa upande wa Mfuko wa Vijana, kwa mfano, SACCOS mbili katika kila Halmashauri na Manispaa zote za Tanzania Bara ziliainishwa na kukopeshwa. Kwa ajili hiyo, jumla ya SACCOS 238 zilikopeshwa shilingi bilioni 1.19 hadi Desemba, 2010. Mfuko wa Dhamana wa Mradi wa Usawa wa Jinsia na Ajira Bora kwa Wanawake ulitoa jumla ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.23 kwa wajasiriamali 3,800 kupitia SACCOS za wanawake. Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi nao uliweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 45.44 ambapo wajasiriamali 72,113 walifaidika na SACCOS zipatazo 192 na vikundi vya uzalishaji mali na kiuchumi vipatavyo 86 vilifaidika na fedha hizo. Fursa nyingi za ajira zimezalishwa na mifuko hii, ndiyo maana ni sera ya Serikali kuiendeleza na kuongeza uwekezaji.

Ndugu Wananchi;

Tutaongeza fedha katika mifuko ya Serikali ili watu wengi zaidi wanufaike miaka ijayo. Aidha, tutaendelea kuboresha mazingira ili asasi za kutoa mikopo midogo ziongezeke, ziimarike na kunufaisha wengi. Hata hivyo, riba zinazotozwa na nyingi ya asasi hizi zinalalamikiwa kuwa kubwa mno kiasi cha kuwakwaza wakopaji. Badala ya juhudi zao kuwa za kujinasua na umaskini wanajikuta wanatumia muda wao mwingi na mapato yao mengi kuhangaikia kulipa riba ya mikopo. Nawaomba wenye asasi zinazokopesha wasikilize kilio hiki kwa moyo wa huruma. Waangalie viwango vya riba na taratibu za malipo. Mkopaji kulipa kila wiki hakumpi nafasi ya kujijenga na hivyo kushindwa kujikomboa na umaskini.

Wajasiriamali wa Kati na Wakubwa

Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;

Kwa upande wa wajasiriamali wa kati na wakubwa wa Kitanzania, tulielekeza nguvu zetu katika kuwajengea fursa na uwezo wa kukua. Tuliendeleza mifuko miwili maalum kwa ajili hiyo yaani Small and Medium Enterprises Credit Scheme na Export Guarantee Scheme. Aidha, kuanzia mwaka wa jana tulianza kuchukua hatua thabiti za kuijenga upya Benki ya Rasilimali ili irejee kufanya kazi ya benki ya uwekezaji kama ilivyokusudiwa ilipoanzishwa. Tuliipa mtaji wa shilingi bilioni 50 na tutafanya hivyo mwaka huu mpaka 2015. Dhamira yetu ni kuwapatia wawekezaji wazawa taasisi ya fedha itakayowawezesha kupata mikopo ya muda wa kati na mrefu. Kwa ajili hiyo wataweza kuwekeza katika shughuli za uzalishaji mali na huduma kama vile viwanda, mahoteli, kilimo, utalii, uchukuzi n.k.



Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;

Tayari watu wameanza kunufaika na mikopo hiyo na uwekezaji unaendelea na ajira zinazidi kuzalishwa. Dhamira yangu ni kuona sekta nyingi na wajasiriamali wengi zaidi wananufaika na mikopo kutoka Benki ya Rasilimali. Naamini juhudi hizi na zile ambazo tunazozielekeza kukuza kilimo zitaongeza sana ajira nchini katika miaka michache ijayo. Kwa upande wa kilimo, pamoja na mikopo inayotolewa sasa kupitia TIB, tunategemea kukamilisha uanzishaji wa Benki ya Kilimo katika mwaka ujao wa fedha.

Kuanzishwa kwa Benki hiyo itakuwa kichocheo kikubwa cha kuleta mapinduzi ya kilimo nchini. Kilimo ndiyo sekta inayowaajiri Watanzania wengi kuliko zote nchini ingawa watu hawaoni kama kujishughulisha na kilimo ni ajira. Hizi ni fikra potofu. Bahati mbaya sana vijana wengi hawapendi kujishughulisha na kilimo kwa sababu ya mazingira magumu ya kazi hiyo na kuwaachia wazee wao. Naamini mageuzi tunayoendelea kufanya chini ya mkakati wa Kilimo Kwanza yakisaidiwa na Benki ya Kilimo itakayoanzishwa yataibadili hali hiyo na kuvutia watu wengi pamoja na vijana kujishughulisha nayo.

Ajira Katika Soko la Pamoja

Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi,

Jumuiya ya Afrika Mashariki nayo inatoa fursa mpya za ajira kwa Watanzania. Utekelezaji wa Umoja wa Forodha umekuza mauzo ya Tanzania katika nchi wanachama na hivyo kuchochea uzalishaji na ajira kuongezeka nchini. Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki iliyoanza kutumika tarehe 1 Julai, 2010 inafungua milango kwa bidhaa, mitaji, ajira na huduma kutoka nchi wanachama wa Jumuiya kutowekewa vikwazo vya kuvuka mipaka kwenda nchi nyingine.

Hatua hii inatoa fursa kwa Watanzania kuweza kupata ajira katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Hivyo hivyo na watu wa nchi hizo nao watapata fursa ya kuajiriwa katika nchi yetu. Tulichokubaliana kwa upande wa ajira ni kuwa kila nchi itaainisha ajira inazofungua kwa watu wa nchi wanachama kuweza kuajiriwa. Zoezi hili limeanza na linaendelea hivi sasa.





Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;

Hii ni fursa nzuri kwa Watanzania kupata ajira, tunachotakiwa kufanya ni kujipanga vizuri ili tunufaike na soko pana zaidi la ajira katika nchi hizo. Tunatakiwa kuangalia mitaala ya shule zetu na vyuo vyetu ili wahitimu wetu waweze kuwa na sifa za kupata ajira katika nchi za Afrika Mashariki. Kadhalika tuzingatie sifa nyingine muhimu za kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na uaminifu. Naamini tunaweza kabisa kuwa hivyo na kufanya hivyo. Watanzania tunayo sifa ya kumudu magumu mengi hata changamoto hii nayo tutaikabili na kushinda.

Maslahi ya Wafanyakazi

Ndugu wafanyakazi,

Kilio chenu cha kuboreshewa mishahara na kupunguziwa kiwango cha kodi tumekipokea kwa uzito unaostahili. Jambo hili mlishalileta siku za nyuma na tumechukua hatua, tunaendelea na tuaendelea kuchukua hatua. Tangu tuingie madarakani, Serikali yetu imekuwa inachukua hatua za makusudi za kuboresha mishahara ya watumishi wa umma na wale wa sekta binafsi. Kwa mfano, kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kimeongezeka kutoka shilingi 65,000 kwa mwezi mwaka 2006 hadi kufikia shilingi 135,000 kwa mwezi mwaka 2010. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 107.

Aidha, tumekuwa tunaboresha mishahara ya kada mbalimbali za utumishi wa umma kwa makundi yao. Hatua hizi zimepunguza kasi ya watumishi wa umma katika baadhi ya kada kuhamia sekta binafsi na hata wale waliohama kurudi. Mkakati huo tutauendeleza kwa kada ambazo hatujazifikia bila kusahau wale tuliokwishawafikia kuwaboresha zaidi.

Ndugu Rais wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi;

Kwa upande wa sekta binafsi, hatua yetu ya kuhakikisha kuwa Bodi za Mishahara za Kisekta zinaundwa na kufanya kazi imeanza kuzaa matunda. Kima cha chini kimepanda kutoka shilingi 48,000/= kwa mwezi hadi shilingi 80,000/= mpaka shilingi 300,000/= kutegemea na aina ya shughuli afanyayo mwajiri.

Vile vile, katika miaka mitano hii, kodi ya mapato imepunguzwa kutoka asilimia 18.5 hadi asilimia 14 na VAT imeshuka kutoka asilimia 20 hadi asilimia 18. Hatua zote hizo zimeleta nafuu ya kiasi fulani.

Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;

Pamoja na hatua hizo bado mishahara ya wafanyakazi nchini ni midogo ukilinganisha na gharama za maisha. Tunatambua hoja na haja ya kuendelea kuongeza mishahara mwaka hadi mwaka mpaka tufikie pale tunapotaka sote tufike, yaani mshahara wa kumudu gharama za maisha.

Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna upungufu wa dhamira wala utashi wa kisiasa wa kufanya hivyo, kwa upande wangu binafsi au wa wenzangu Serikalini. Yale tuliyoyafanya katika miaka mitano iliyopita ni uthibitisho tosha wa ukweli huo. Ahadi ninayopenda kurudia tena leo ni kuwa tutaiendeleza kazi tuliyoianza mwaka hadi mwaka. Hata hivi sasa katika mchakato unaoendelea wa kutayarisha bajeti ya mwaka ujao wa fedha, wahusika wanaangalia namna ya kupandisha kima cha chini cha mashahara na nafuu nyinginezo.

Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;

Uwezo wa kimapato wa Serikali ndiyo kikwazo kinachotupunguzia kasi ya kuboresha mishahara ya watumishi wa umma. Wakati wote tumekuwa tunajikuta tupo katika mtihani kuhusu kuweka uwiano mzuri baina ya matumizi ya mishahara na matumizi kwa ajili ya shughuli nyinginezo za Serikali. Busara inaelekeza kuwa kiasi cha fedha zinazotumika kulipa mishahara kisiwe kikubwa mno na kubakiza kiasi kidogo kwa ajili ya Serikali kutekeleza majukumu yake mengine ya utawala, ulinzi na usalama, maendeleo na utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi wake.

Changamoto kubwa tuliyonayo ni jinsi ya kuongeza zaidi mapato ya Serikali ili tuwe na fedha za kutosha kuwalipa wafanyakazi mishahara inayokidhi gharama za maisha na kubaki na pesa nyingi zaidi kwa Serikali kuendesha shughuli zake na kuhudumia wananchi wake. Katika miaka mitano iliyopita tumefanya juhudi kubwa ya kuongeza mapato ya Serikali na tumepata mafanikio yanayotia moyo. Mapato yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 177.1 kwa mwezi mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 390.7 kwa mwezi mwaka 2010.

Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;

Mafanikio hayo ndiyo yaliyotuwezesha kuongeza mishahara kwa kiasi tulichofikia sasa. Hivyo basi, jawabu la tatizo lipo katika kuongeza zaidi mapato ya Serikali. Hiyo ndiyo dhamira yetu na tumejipanga kimkakati kufanya hivyo. Ndiyo maelekezo yangu ya msingi niliyoyatoa kwa wenzetu wa Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato nilipowatembelea mwezi Februari, 2011. Kinachotakiwa ni wafanyakazi wenzetu katika asasi hizo kufanya kazi kwa bidii na uaminifu na walipa kodi kuwapa ushirikiano.

Ndugu Rais wa TUCTA;

Nafurahi kwamba katika risala yenu mmetoa mawazo mengi mazuri kuhusu namna ya kuongeza mapato ya Serikali, kubana matumizi na kuboresha mishahara ya wafanyakazi. Mawazo yenu yanashabihiana sana na mawazo yetu na baadhi ya mambo tunayofanya na tunayoyafikiria kuyafanya katika kuboresha mapato ya Serikali na maslahi ya watumishi wa umma. Tupeni nafasi tukayafanyie kazi.

Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;

Nimeagiza pia kuwa Serikali yetu ianze kufikiria mambo mbalimbali yatakayowanufaisha wafanyakazi na kuinua hali zao za maisha. Hususan nimeagiza tuangalie uwezekano wa wafanyakazi kupata mikopo ya gharama nafuu watakayoitumia kununua au kujenga nyumba au kununua vyombo vya usafiri au vyombo vya nyumbani. Tumekuwa tunatoa mikopo kwa Waheshimiwa Wabunge, sasa tufanye hivyo kwa watumishi wa Serikali nao. Nafurahi kuwa Azimio la kuanzisha mfuko wa mikopo ya watumishi wa umma lilipitishwa na Bunge katika kikao kilichopita.

Vile vile, nimeagiza tutoe kipaumbele kwa ujenzi wa nyumba za kuishi watumishi wa umma hasa wale wa vijijini na vyombo vya ulinzi na usalama ili tuboreshe mazingira yao ya kazi. Ni kazi ambayo tunaifanya hivi sasa ila tunataka tuipe msukumo mkubwa zaidi.

Wafanyakazi wa Sekta Binafsi

Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi;

Kwa upande wa wafanyakazi katika sekta binafsi, tutaendelea kusimamia Mabaraza ya Mishahara ya Kisekta ili yafanye kazi zake ipasavyo na kuhakikisha kwamba maslahi ya watumishi katika sekta hiyo yanaboreshwa. Kwa hatua tulizokwishazichukua tangu yaundwe, mafanikio yake yameanza kuonekana. Hata hivyo, wafanyakazi wangeweza kunufaika zaidi. Naambiwa kwamba wafanyakazi wengi katika sekta binafsi wapo katika mazingira magumu. Wapo wengi ambao ni vibarua wa kutwa na wengine wako hivyo kwa maisha yao yote. Aidha, wanapata ujira mdogo.

Waajiri wanakwepa wajibu wao stahiki kwa wafanyakazi wao ambao ndiyo wanaofanya watajirike. Kuwasaidia wafanyakazi kudai na kupata haki zao ni moja ya agenda muhimu za Serikali yetu. Naomba vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi tusaidiane na kushirikiana katika jambo hili. Haya ni mapambano yetu sote. Tukishirikiana na kusaidiana tutashinda.

Kuboresha Pensheni/Malipo ya Uzeeni

Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Wafanyakazi,

Nawashukuru sana kwa maneno yenu ya pongezi kuhusu hatua tulizochukua juu ya kurekebisha na kuboresha mafao ya wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii. Nami nafurahi kwamba, lile tatizo la mafao ya wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaaam waliokuwa katika mfumo wa SSSS tumelipatia ufumbuzi. Wafanyakazi hao sasa wameingizwa katika mfumo wa PPF kama wenzao wengine. Kwa ajili hiyo Serikali italipa shilingi bilioni 9.46 kufidia michango ambayo haikuwahi kulipwa ili ndugu zetu hawa waweze kulipwa mafao yao chini ya mfumo wa PPF.

Jambo la pili ni kuwa nafurahi Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imekwishaundwa na imekwishaanza kazi. Tena wameanza vizuri. Kupitia mamlaka hii sasa masuala yahusuyo afya ya mifuko, uwianishaji wa mafao baina ya mifuko na uboreshaji wa mafao yatapatiwa ufumbuzi wa uhakika na kwa wakati. Chombo hiki ni kipya, lazima tukiunge mkono. Sisi katika Serikali tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kukilea. Naomba vyama vya wafanyakazi na mifuko ya hifadhi kukipa ushirikiano unaostahili ili kiweze kufanikisha majukumu yake ipasavyo.

Kuhusu mchakato wa Katiba, napenda kuwahakikishia kuwa hakuna atakayebaguliwa. Tunataka watu wote wapate fursa ya kushiriki. Jipangeni kushiriki kwa ukamilifu. Tusiruhusu watu wachache wanaotaka kuhodhi mjadala huu kwa kutaka maoni yao tu ndiyo yasikilizwe na kuwazuia wengine wasitoe maoni yao. Tukiruhusu tabia hiyo huenda tusipate Katiba ambayo itawakilisha maoni ya wengi bali kikundi fualni kilicho hodari kupiga kelele bila hoja.

Hitimisho

Ndugu Rais wa TUCTA, Ndugu Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi na Ndugu Wafanyakazi;

Nimezungumza kwa muda mrefu. Nimejitahidi katika hotuba yangu kutoa maelezo ya ufafanuzi kwa takriban kila jambo lililotajwa katika risala yenu. Yapo baadhi ambayo sikuyazungumzia lakini siyo kwamba nimeyapuuza. Kila jambo mlilolitaja tutalifanyia kazi. Nia yetu ni kujenga nchi yetu na katika kufanya hivyo natambua kuwa wafanyakazi ni mhimili muhimu sana. Ni wajibu wetu kuwasikiliza, ni wajibu wetu kushirikiana nanyi na ni muhimu kushughulikia musuala yenu ipasavyo. Kila mmoja wetu anamuhitaji mwenzake. Narudia tena kuwahakikishia ushirikiano wangu binafsi na ule wa wenzangu wote Serikalini wakati wote.

Naomba nimalize kwa kusema kuwa kwa ushirikiano na mshikamano baina ya utatu wetu, yaani Wafanyakazi, Waajiri na Serikali hakuna litakalotushinda na hakuna mfanyakazi wa Tanzania atakayekuwa mtumwa katika nchi yake.

Nawashukuru tena viongozi wa TUCTA kwa kunialika kwenye sherehe hizi muhimu. Hongereni kwa sherehe zilizofana sana.

Mungu Ibariki Afrika!

Mungu Ibariki Tanzania !

Asanteni kwa Kunisikiliza.