Wednesday, January 12, 2011

SIMBA BINGWA WA KOMBE LA MAPINDUZI!!





Timu ya Simba jana usiku ilifanikiwa kutwaa Ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuwafungwa Mahasimu wao Yanga kwa magoli 2-0!! Mchezo huo ulipigwa kwenye Uwanja wa Amani na kushuhudia Simba ikijipatia magoli yake kupitia Mussa Hassan Mgosi na Shija Mkina!!

SHEREHE ZA MIAKA 47 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR!!




Viongozi ambao wamehudhuria Sherehe za Miaka Arobaini na Saba ya Mapinduzi ya Zanzibar!! Sherehe hizi zimefanyika kwa mara ya kwanza wakati Visiwa vya Zanzibar vikiongozwa na Dokta Ally Mohamed Shein ambapo aliweza kuhutubia maelfu waliojitokeza!!

Tuesday, January 11, 2011

MESSI, MOURINHO NA MARTA WATWAA TUZO ZA FIFA!!




Tuzo za Mwaka za Fifa zimetolewa!! Lionel Messi ametwaa Tuzo ya Mchezaji Bora akiwashinda Xavi Hanandez na Andrea Iniesta wote kutoka Barcelona!! Jose Antonio Mourinho akiibuka Kocha Bora wa Mwaka!! Wakati Mchezaji Bora upande wa wanawake akiwa Marta Vieira Da Silva na kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya Nne mfululizo!!

Monday, January 10, 2011

MICHUANO YA FA YAPAMBA MOTO!!










FA Cup Results
Chelsea 7-0 Ipswich
Leicester 2-2 Man City
Man Utd 1-0 Liverpool
Tottenham 3-0 Charlton

Tuesday, January 4, 2011

SALAMA ZA MWAKA MPYA KUTOKA KWA RAIS KIKWETE-NAWEKA KUMBUKUMBU SAWA!!

SALAM ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT.JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA,
TAREHE 31 DESEMBA, 2010

Ndugu Wananchi;
Habari za jioni.
Leo tunauaga Mwaka 2010 na kuukaribisha Mwaka 2011. Kama ilivyo ada, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kutujaalia uhai na kutuwezesha kuifikia siku hii adhimu. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi ambao hawakujaaliwa bahati hii kwa kuwa wametutangulia mbele ya haki.Tuzidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awape mapumziko mema.
Ndugu Wananchi;
Kwa namna ya kipekee mimi binafsi, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima na kuniwezesha kuendelea kuitumikia nchi yangu na ninyi wananchi wenzangu. Nawashukuruni sana wananchi wenzangu kwa kuendelea kuniunga mkono mimi na kuiunga mkono Serikali yetu ninayoiongoza. Mmefanya hivyo mwaka huu tunaoumaliza leo na tangu tuingie madarakani miaka mitano iliyopita mpaka sasa. Imani na upendo mliyotuonesha vimetupa faraja na ari ya kuendelea kuwatumikia kwa bidii zaidi. Nawaomba muendelee na moyo huo katika mwaka mpya tunaoukaribisha usiku wa leo. Mimi nawaahidi kuendelea kutumia vipaji vyangu vyote nilivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwatumikia wakati wote na kwa hali yoyote kama nilivyofanya mwaka huu tunaoumaliza leo na miaka ya nyuma.
Ndugu wananchi;
Mwaka 2010 ulikuwa na shughuli nyingi na mafanikio mengi licha ya kuwepo changamoto mbalimbali zilizojitokeza. Kwa ajili hiyo tunaingia mwaka 2011 tukiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri zaidi.
Hali ya Usalama Nchini
Ndugu Wananchi;
Hali ya usalama wa nchi yetu ni mzuri, mipaka iko salama na hakuna tishio lolote kutoka mahali popote au watu wowote linalotia mashaka. Uhalifu umeendelea kudhibitiwa na mafanikio yamekuwa yanapatikana. Taarifa ya Jeshi la Polisi ya hivi karibuni inaonyesha kuwa matukio ya uhalifu yamepungua mwaka huu ukilinganisha na mwaka uliopita.
Ndugu Wananchi;
Ni jambo la kujivunia kwamba tumemaliza mchakato wa uchaguzi mkuu kwa amani na salama. Tulikuwa na siku 70 za kampeni, moja ya kupiga kura na siku 6 za kusubiri matokeo bila ya kuwepo matukio ya uvunjifu wa amani yanayostahili kuzungumzwa. Sehemu zetu zote mbili za Muungano kulikuwa salama na Zanzibar ndiko kulikuwa na utulivu mkubwa zaidi kuliko miaka ya nyuma.
Hakika Tanzania tumeendelea kudumisha sifa yetu ya kuwa kisiwa cha amani na utulivu. Naomba sote tujipongeze, lakini tutoe pongezi maalum kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya mwaka huu ya kuhakikisha kuwa nchi yetu na watu wake wako salama.
Demokrasia Inazidi Kuimarika
Ndugu Wananchi, Watanzania Wenzangu;
Mwaka huu tumeshuhudia demokrasia ilivyozidi kuota mizizi, kukomaa, kustawi na kuimarika. Tumefanya Uchaguzi Mkuu wa nne chini ya mfumo wa vyama vingi kwa mafanikio makubwa. Sisi wenyewe ni mashahidi na dunia nzima ni mashahidi wa ukweli huo. Wakati tukitambua na kujipongeza kwa mafanikio haya, hatuna budi kujiwekea dhima ya kufanya mambo yetu vizuri zaidi katika chaguzi zijazo. Tufanye tathmini ya uchaguzi wetu uliopita ili tuimarishe na kudumisha yaliyo mazuri na kurekebisha yenye mapungufu.
Ndugu Wananchi;
Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa na ushindani mkali na nguvu ya vyama vya upinzani imeongezeka. Hili ni jambo jema kwa utawala bora na uwajibikaji nchini. Bila ya shaka Bunge litachangamka kama tunavyotarajia sote. Nimewakumbusha Mawaziri wajibu wao wa kuwa makini na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi Bungeni. Kwa upande wa Chama tawala hatuna budi kujipanga na kujijenga upya kwa kuzingatia mazingira mapya ya kisiasa nchini.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Naomba kurudia kukumbusha kuwa uchaguzi ulishaisha Oktoba 31, 2010 na malumbano ya kampeni za uchaguzi yalimalizika wakati ule. Sasa ni wakati wa kuendelea kufanya shughuli zetu za kawaida za kujiletea maendeleo yetu wenyewe na ya nchi yetu. Kuendeleza malumbano na kuendelea kuishi kama vile kampeni za uchaguzi bado zinaendelea siyo sahihi hata kidogo.
Najua wapo baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa ambavyo vimepanga mikakati ya kuendeleza malumbano ya uchaguzi na kutaka Watanzania waishi kama vile nchi ipo kwenye kampeni za uchaguzi. Wamepanga wakati wote kutafuta jambo au hata kuzua jambo ili kuwachochea wananchi waichukie Serikali. Wamepanga kuchochea migomo vyuoni na maandamano ya wananchi mara kwa mara. Kwao wao huo ndiyo mkakati wa kujijenga kisiasa ili kujiandalia ushindi kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.
Nawatanabaisha ndugu zangu myajue hayo ili msipoteze muda wenu muhimu wa kujiendeleza na kugeuzwa kuwa mbuzi wa kafara kwa ajili ya kuendeleza maslahi ya kisiasa ya watu fulani. Kwa jinsi watu hao walivyokuwa wabinafsi na wasivyokuwa na huruma na wenzao, wako tayari kuchochea ghasia bila kujali madhara yatakayowakuta watu watakaoshiriki. Wao hasa wanachotaka ni ghasia kutokea na vyombo vya dola kuingilia ati waiambie jumuiya ya kimataifa jinsi Serikali yetu ilivyo katili. Nawasihi ndugu zangu msiwasikilize wala kuwafuata wanasiasa hawa.
Nawaomba, wakiwafuata wakumbusheni kuwa wao wanazo fursa nyingi za kusema wayatakayo Bungeni na kwingineko, waache kuwatumia kama chambo au wahanga wa maslahi yao.
Uwajibikaji wa Mawaziri
Ndugu wananchi;
Tunaumaliza mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011 tukiwa na Serikali mpya yenye damu mpya nyingi na changa katika Baraza la Mawaziri. Nimejitahidi kuwapanga Mawaziri hao kwa namna ambayo wanaweza kutumia vyema maarifa yao na uzoefu wao kulisukuma kwa kasi, ari na nguvu zaidi, gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Nimeshakutana na kuzungumza nao wote kuhusu majukumu yao na wajibu wao.
Nimewasisitizia matumaini yangu kwao ya kuwa wachapa kazi hodari na kupiga vita rushwa, uzembe na ubabaishaji bila ya ajizi. Wawe watu waaminifu na waadilifu, watakaochukia maovu na kuyapiga vita kwa nguvu zao zote katika maeneo yao ya kazi. Wawe ni watu wenye moyo wa kuipenda nchi yetu na watu waliotayari kuitumikia kwa moyo na uwezo wao wote. Wawe karibu na watu wawasikilize na wawe wepesi kutatua shida zao. Aidha, nimewakumbusha kutambua kuwa ahadi kubwa ya CCM kwa Watanzania ni Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010, hivyo wahakikishe kuwa malengo ya Ilani kuhusu maeneo yao ya uongozi wanayatambua vizuri na kuyapangia mipango thabiti ya utekelezaji na kufuatilia kwa dhati utekelezaje wake. Nafurahi kwamba Mawaziri tayari wameanza kazi kwa kasi nzuri na wengine kwa kishindo. Naomba tuendelee kuwaunga mkono na kuwasaidia.
Nidhamu ya Matumizi
Ndugu Wananchi;
Miongoni mwa mambo ambayo nimesisitiza kwa Mawaziri ni kuhakikisha kuwa wanasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya Serikali na hasa nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma. Tunapata mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa ukusanya mapato. Ndugu zetu wa TRA wanastahili pongezi zetu kwa kazi waifanyayo. Pamoja na hayo hatuna budi kuongeza mapato ya Serikali maradufu juhudi zetu za kukusanya mapato, kwani mahitaji yanazidi kuongezeka wakati uwezo wa mapato hauongezeki kwa kasi hiyo hiyo.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa nidhamu ya matumizi bado hatujapiga hatua ya kunifanya nipoe moyo, ingawaje kuna mafanikio yanayoendelea kupatikana. Niliwakumbusha Mawaziri kuhusu kuwepo Kamati za Matumizi ya Fedha katika kila Wizara, Idara za Serikali na Halmashauri za Wilaya na Miji ambazo niliagiza ziundwe miaka mitatu iliyopita. Niliwakumbusha kuwa, wakuu wa taasisi hizo ndio wanaoongoza Kamati hizo na hivyo wao ndiyo wanaoongoza Kamati za Wizara zao. Nimewataka wahakikishe kuwa Kamati hizo zinatekeleza ipasavyo majukumu yake ili rasilimali za taifa zifanye kazi iliyokusudiwa. Halikadhalika, niliwataka wahakikishe kuwa Kamati za Idara na Mashirika chini ya Wizara zao zinafanya kazi kwa ukamilifu.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Halmashauri za Wilaya na Miji, mwaka huu tuliendelea kuziimarisha Idara za Uhasibu na Ukaguzi wa Ndani. Tutaendelea kuhakikisha kuwa kila Halmashauri ina Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wenye ujuzi na sifa zinazostahili za kitaaluma, uaminifu na uadilifu.
Siku za nyuma tulishafanya uamuzi wa kumfanya Mhasibu Mkuu wa Serikali kuwa na mamlaka ya kuangalia utendaji wa shughuli za fedha katika Halmashauri za Wilaya na Miji kama aliyonayo kwa Wizara na Idara za Serikali Kuu. Mwaka huu tumeamua kuwaunganisha Wakaguzi wote wa Ndani wa Wizara na Idara za Serikali chini ya Uongozi mmoja. Aidha, tumeunda nafasi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani ambaye Wakaguzi wa Ndani wote wa Wizara na Idara za Serikali watakuwa chini yake na kuwajibika kwake. Yeye atahusika na uteuzi wao na kuwapangia vituo. Tumeamua, pia, kuwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani atakuwa na mamlaka kwa Wakaguzi wa Ndani wa Halmashauri za Wilaya na Miji. Bila ya shaka hatua hii itasaidia kuimarisha uwajibikaji, nidhamu na uaminifu katika matumizi ya pesa na mali za umma.
Hali ya Uchumi
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza mwaka 2010 hali ya uchumi wa nchi ikiwa ni ya kuridhisha. Inaelekea athari za miaka mitatu iliyopita zilizosababishwa na misukosuko mbalimbali ya uchumi wa dunia sasa zinanza kutoweka. Tunatarajia kuwa mwaka huu uchumi utakua kwa asilimia 7 ukilinganisha na asilimia 6 ya mwaka 2009. Matumaini yetu ni kuwa mwaka 2011 uchumi utakua kwa asilimia 7.2 kama mambo yatakwenda kama tunavyotarajia.
Mfumuko wa bei nao umeshuka sana kutoka wastani wa asilimia 12.1 mwaka 2009 hadi asilimia 5.5 Novemba, 2010. Ni dhamira yetu na matarajio yetu kuwa mfumuko wa bei utaendelea kuwa chini ya hapo. Kwa ajili hiyo hatuna budi kuhakikisha kuwa hali ya ipatikanaji wa chakula nchini inaendelea kuwa nzuri.
Kilimo na Chakula
Ndugu wananchi;
Hali ya upatikanaji wa chakula nchini ilikuwa nzuri katika mwaka 2010 lakini hatuna hakika hali itakuwaje katika mwaka 2011. Tunazo sababu za kutia shaka kwa sababu ya hali ya mvua kutokuwa nzuri katika maeneo mengi hapa nchini. Maeneo mengi yanayopata mvua za vuli katika mikoa ya Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara hali ilikuwa mbaya. Mvua zimekuwa pungufu sana na wakulima wengi hawakudiriki hata kupanda mazao. Kwa mikoa hii matumaini yetu tunayaweka kwa mvua za masika zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwezi Machi. Tuombe kwa Mola mvua zipatikane za kutosha tunusurike na baa la njaa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mikoa ya Kusini Nyanda za Juu na mingineyo inayopata mvua moja kuanzia mwezi Novemba au Desemba, mvua zilichelewa kuanza kunyesha. Hivi sasa zimeanza na zinaendelea vizuri. Tuzidi kumuomba Mungu ziendelee vizuri ili taifa liwe na hakika ya akiba ya kutosha ya chakula ambayo huchangiwa kwa zaidi ya asilimia 85 na mikoa ya ukanda huu.
Wataalamu wetu wa Idara ya Hali ya Hewa wametahadharisha kuwa hata maeneo haya huenda yakapata mvua chini ya kiwango cha kawaida. Kwa ajili hiyo, niwaombe ndugu zangu wa mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mbeya na Rukwa kuhakikisha kuwa wanazitumia vizuri mvua zinazonyesha sasa. Tukifanya hivyo athari za upungufu wa mvua tutazipunguza. Na, kwa wananchi wote kwa jumla nawaomba tuwe waangalifu katika matumizi ya akiba yetu ya chakula tuliyonayo. Wahenga walisema “tahadhari kabla ya hatari”. Tuzingatie maneno hayo ya hekima.
Hifadhi ya Chakula
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2010 tumeamua kuongeza akiba yetu ya chakula katika Hifadhi ya Taifa ili ifikie tani 400,000 ifikapo mwaka 2015. Tumeanza safari hiyo kwa dhati. Mwaka huu tumenunua tani 200,000 na kuzihifadhi. Kwa sababu hiyo tuliongeza fedha za kununulia chakula kutoka shilingi bilioni 18.2 hadi shilingi bilioni 60.26. Tutaendelea kukuza uwezo huo mpaka tufikie lengo letu.
Pembejeo za Kilimo
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumeongeza mbolea ya ruzuku na wakulima wengi zaidi watapata mbolea hiyo. Tutaendelea kufanya hivyo katika miaka ijayo kwa lengo la kuwafikia wakulima milioni 3.5 mpaka 4 miaka mitano ijayo. Aidha, tutaendelea kufuatilia na kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya upatikanaji na hasa usambazaji wa pembejeo kwa wakulima na wafugaji. Nasikitishwa sana na taarifa za vitendo vya wizi na udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya mawakala wa mbolea, mbegu na dawa za kilimo na mifugo wakishirikiana na baadhi ya watumishi wa umma wa ngazi mbalimbali.
Nimewataka Mawaziri husika na hasa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya na vyombo vya dola yaani Polisi na TAKUKURU kufuatilia mwenendo mzima wa usambazaji na upatikanaji wa mbolea, mbegu na dawa za ruzuku kwa wakulima na wafugaji. Wawatafute na kuwabaini wale wote wanaofanya vitendo viovu kinyume na taratibu zilizowekwa na kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu. Watu hawa ni wahujumu wa uchumi, ni adui wa wakulima, wafugaji na taifa zima kwa jumla. Hawastahili na wala wasionewe huruma hata chembe.
Ndugu wananchi;
Pamoja na mikakati tuliyojiwekea ya kuboresha kilimo, tutaendelea kuwekeza na kuhamasisha uwekezaji katika sekta nyingine ambazo tunazitegemea zisaidie kukuza uchumi na kupunguza umaskini kama vile viwanda, utalii, biashara, miundombinu ya barabara, reli, bandari, umeme, maji n.k. Kwa upande wa huduma ya fedha, Serikali itaendelea kuongeza mtaji kwenye Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ili irudie kuwa benki ya maendeleo na kutoa mikopo ya muda wa kati na mrefu kwa wawekezaji wetu. Ni dhamira yetu kuwa mwaka 2011 tuongeze kasi ya kuanzisha Benki ya Kilimo ili ikiwezekana ianze au matayarisho yafikie hatua nzuri ya kuweza kuanza mwaka unaofuata.
Matatizo ya Umeme
Ndugu wananchi;
Mwaka 2010 haukuwa na utulivu wa kutosha kwa upatikanaji wa umeme. Mara kadhaa kumekuwepo na matukio ya kukatika na mgao wa umeme kutokana na uharibifu wa mitambo ya kuzalisha umeme hasa katika kituo cha Songas na vituo vya TANESCO. Pamoja na hayo tatizo la msingi ni uwezo wa uzalishaji wa umeme kuwa mdogo kuliko mahitaji. Hivyo basi, hitilafu katika mtambo mmoja au kituo kimoja cha kuzalisha umeme huzua tatizo kubwa la upatikanaji wa umeme kwa nchi nzima.
Ndugu Wananchi;
Katika kukabiliana na tatizo hilo miaka mitano iliyopita, TANESCO kwa msaada wa Serikali, imeongeza uwezo wa kuzalisha umeme kwa MW 145 (MW 100 Ubungo na MW 45 Tegeta) kwa kutumia gesi asilia. Bahati mbaya mpango wa kuzalisha MW 300 kule Mtwara kwa kushirikiana na sekta binafsi, haukufanikiwa baada ya mwekezaji kushindwa kupata fedha kwa sababu ya mgogoro wa masoko ya fedha ya kimataifa. Kama tatizo hilo lisingekuwepo umeme huo ungekuwa unakamilika au kukaribia kutumika hivi sasa.
Kwa sasa TANESCO ina mipango kadhaa inayoendelea nayo ya kuongeza uzalishaji wa umeme nchini. Kwa msaada wa Serikali ndani ya miezi 12 ijayo, TANESCO itaongeza uzalishaji wa umeme kwa MW 160, (MW 100 Ubungo kwa kutumia gesi asilia na MW 60 Mwanza kwa kutumia dizeli nzito). Kwa kushirikiana na sekta binafsi pia, ndani ya miezi 36 ijayo TANESCO wanatarajia kukamilisha ujenzi wa vituo vya umeme huko Kinyerezi (MW 240) Somanga Fungu (MW 230) na Mtwara (MW 300). Inatarajiwa pia kwamba katika kipindi hicho mradi wa kuzalisha MW 200 pale Kiwira utakamilika.
Bei ya Umeme
Ndugu Wananchi;
Natambua kuwepo kwa mazungumzo, katika jamii kuhusu uamuzi wa EWURA wa kukubali ombi la Shirika la Umeme (TANESCO) kuongeza bei ya umeme. Wakati mwingine mazungumzo yamekuwa na hisia kali na hata jazba kutawala. Wizara, TANESCO na EWURA wameeleza kwa ufasaha misingi iliyotumika mpaka kufikia uamuzi huo. Sina maelezo mazuri zaidi ya hayo. Ninachotaka kusema mimi ni kuwaomba Watanzania wenzangu kutokukubali suala hili la kibiashara na kiuchumi kugeuzwa kuwa la kisiasa na kutafutiwa majawabu ya kisiasa.
Naomba tuamini na kukubali maelezo ya TANESCO na EWURA kwamba katika miaka minne hii gharama za uendeshaji, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme zimepanda kama zilivyopanda katika shughuli nyingine. Hivyo basi, kutaka bei ya umeme ibaki kama ilivyokuwa miaka minne iliyopita hautokuwa uamuzi sahihi kiuchumi na kibiashara kwa TANESCO. EWURA imefanya kazi nzuri ya kuchambua maombi ya TANESCO na kuyakubali yanayostahili na kuyakataa yasiyostahili kuwa sehemu ya bei. Kwa kufanya hivyo, watumiaji wa umeme wamelindwa wasibebeshwe mzigo usiostahili na Shirila la Umeme limewezeshwa ili lisiendeshe shughuli zake kwa hasara.
Mahusiano ya Kimataifa
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2010 Serikali iliendelea na jitihada za kupigania na kuendeleza maslahi ya Tanzania miongoni mwa mataifa duniani na mashirika ya kimataifa na kikanda. Kazi hiyo tumeifanya kwa mafanikio na faida zake tunaziona. Tumeshuhudia kuongezeka kwa misaada ya maendeleo, kupatiwa misamaha ya madeni, kuongezeka kwa wawekezaji na mitaji kutoka nje na kuzidi kuongezeka kwa watalii. Aidha, mauzo yetu nje pamoja na mapato na akiba yetu ya fedha za kigeni navyo vimeendelea kuongezeka.
Jina la nchi yetu limeendelea kung’ara katika medani za kimataifa. Tanzania imeendelea kushirikishwa katika masuala muhimu ya kikanda na kimataifa. Kwa mfano, Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin W. Mkapa aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuongoza Tume ya kuangalia mchakato wa kura ya maoni ya Sudan ya Kusini itakayofanyika tarehe 9 Januari, 2011.

Katika kura hiyo, wananchi wa Sudan ya Kusini wataamua iwapo wawe taifa huru au waendelee kuwa sehemu ya Sudan kama ilivyo sasa na Wananchi wa Jimbo la Abyei watapiga kura ya kuamua wawe upande upi: Sudan Kusini au Sudan Kaskazini. Tunamtakia heri Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ili akamilishe jukumu hilo kwa mafanikio. Wakati huo huo tunawatakia wananchi wa Sudan ya Kusini na Sudan, kwa jumla, kuendesha zoezi hilo kwa amani na salama ili watu wapate fursa ya kuamua matakwa yao kwa uhuru.
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka huu tunaoumaliza leo Umoja wa Mataifa umetupatia heshima nyingine kubwa. Shirika la Afya Duniani limeniteua mimi na Waziri Mkuu wa Canada Mheshimiwa Stephen Harper kuwa Wenyeviti Wenza wa kuongoza Tume ya Kimataifa kuhusu Afya ya Akina Mama na Watoto. Lengo kuu la Tume hiyo ni kuzisaidia nchi zinazoendelea ziweze kutekeleza Malengo ya Milenia kuhusu kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Tume yetu ina kazi ya kupendekeza mfumo wa kutoa taarifa juu ya maendeleo ya afya za akina mama na watoto na kufuatilia utekelezaji wa ahadi za nchi tajiri kuzisaidia nchi masikini kukabiliana na changamoto za afya za akina mama na watoto. Aidha, tunalo jukumu la kupendekeza mfumo wa kufuatilia jinsi fedha zinazotolewa, zinavyotumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Tunatarajia kuanza kazi Januari 2011 na kuwasilisha Ripoti yetu kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kunako Mei 2011.
Michezo
Ndugu Wananchi;
Nafurahi kama tunavyofurahi wote kuwa kwa upande wa michezo, mwaka huu tumeumaliza vizuri. Timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, imefanikiwa kushinda Kombe la Challenge kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati baada ya kufanya hivyo mara ya mwisho miaka 16 iliyopita yaani mwaka 1993. Timu yetu ya Soka ya Wanawake, Twiga Stars, nayo kwa mara ya kwanza, iliweza kufikia fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake.
Hatuna budi kuyatambua na kuyaenzi mafanikio hayo tuliyoyapata. Wakati huo huo tuwatake wanamichezo wetu kuwa na ari ya kufanya vizuri zaidi. Nimetoa changamoto kwa TFF na timu yetu ya taifa kujiwekea lengo la kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012. Wakiamua hivyo, itabidi waanze sasa kufikiria na kufanya maandalizi ya namna ya kufanikisha lengo hilo.
Napenda kutumia nafasi hii kuwahakikishia wanamichezo wote na Watanzania wenzangu, kuwa nitaendelea kuziunga mkono kwa hali na mali timu zetu zinazoshiriki michezo mbali mbali. Mwaka huu nitakuwa na mazungumzo na viongozi wa riadha ili tuelewane kuhusu namna ya kufufua michezo hiyo ambayo miaka ya nyuma ilililetea taifa letu sifa kubwa.
Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru
Ndugu Wananchi;
Mwaka mpya tunaouanza usiku wa leo una umuhimu wa kipekee katika uhai na historia ya nchi yetu. Tarehe 9 Desemba 2011 nchi yetu itatimiza miaka hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara. Haya si mafanikio madogo hata kidogo. Ni mafanikio makubwa sana ambayo hatuna budi kuyafurahia na kuyasherekea kwa uzito unaostahili.
Katika miaka 50 ya Uhuru wetu tumefanya mambo mengi mazuri ya kujivunia katika nyanja mbalimbali. Tumedumisha uhuru na umoja wa nchi yetu. Kwa hakika hali yetu ilivyo leo kisiasa, kiutamaduni, kiuchumi, kijamii, kiusalama na kimaendeleo kwa jumla, ni tofauti sana na hali ilivyokuwa wakati Tanzania Bara inapata uhuru wake tarehe 9 Desemba, 1961. Natambua pia kwamba katika miaka 50 hii, nchi yetu na watu wake wamekumbana na kukabili changamoto nyingi. Zipo nyingi tulizoziweza na zipo ambazo tunaendelea kuzikabili na tunayo mipango thabiti ya kuhakikisha tunafanikiwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa kutambua umuhimu wa aina yake wa maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, 2011, tumekubaliana na viongozi wenzangu Serikalini kuwa tusherehekee siku hiyo kwa uzito unaostahili.
Ndugu Wananchi;
Tumekubaliana pia, tufanye mambo manne muhimu katika maadhimisho hayo. Kwanza, nautangaza mwaka 2011 kuwa ni Mwaka wa Maadhimisho ya Miaka Hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara. Kilele chake kitakuwa tarehe 9 Desemba, 2011 ambapo kutafanyika sherehe kubwa na za aina yake nchi nzima ambapo wananchi watashirikishwa kwa ukamilifu.
Pili, tufanye tathmini ya kina ya mafanikio tuliyoyapata, katika juhudi zetu za kujiletea maendeleo katika miaka hamsini hii. Kila Wizara, idara na taasisi za Serikali na hata sekta binafsi zifanye tathmini ya eneo lake. Tathmini hizo ziandikwe katika vitabu ili kuhifadhi kumbukumbu hizo muhimu kwetu na kwa vizazi vijavyo. Vitabu na nyaraka hizo vitakuwa kumbukumbu zenye manufaa makubwa kwa wenzetu watakaokuwepo mwaka 2061 wakati wa kusherehekea miaka 100 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Itarahisisha kazi yao ya kufanya tathmini wakati huo.
Tatu, kwamba yafanyike maonyesho maalum katika Uwanja wa Maonyesho wa Julius Nyerere hapa Dar es Salaam na kote mikoani kwenye viwanja vya maonyesho, kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali katika miaka 50 tangu Uhuru wa Tanzania Bara.
Ndugu Wananchi;
Jambo la nne ambalo tulilokubaliana kufanya ni kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya Nchi yetu kwa lengo la kuihuisha ili hatimaye tuwe na Katiba inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne. Katiba yetu ya sasa tuliyoachiwa na waasisi wa taifa letu, imeifanyia nchi yetu mambo mengi mazuri na kuifikisha Tanzania na Watanzania hapa tulipo. Tunayo nchi moja huru, ya kidemokrasia na inayoendesha mambo yake kwa kuzingatia utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na mgawanyo wa madaraka miongoni mwa mihimili mikuu ya dola. Nchi yenye amani, utulivu na watu wake ni wamoja, wanaopendana na kushirikiana na maendeleo yanazidi kupatikana.
Pamoja na hayo, mwaka 2011, nchi yetu inatimiza miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, miaka 47 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar na miaka 47 ya Muungano wa nchi zetu mbili. Yapo mabadiliko mengi yaliyotokea katika nyanja mbalimbali za maisha ya nchi yetu na watu wake katika kipindi hiki. Kwa ajili hiyo ni vyema kuwa na Katiba inayoendana na mabadiliko na matakwa na hali ya sasa. Katiba ambayo italipeleka taifa letu miaka 50 ijayo kwa salama, amani, umoja na kuwepo maendeleo makubwa zaidi.
Ndugu Wananchi;
Ndiyo maana tukaamua kuanzisha mchakato huu na kwa ajili hiyo, nimeamua kuunda Tume maalum ya Katiba, yaani Constitutional Review Commission. Tume hiyo itakayoongozwa na Mwanasheria aliyebobea, itakuwa na wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii yetu kutoka pande zetu mbili za Muungano. Jukumu la msingi la Tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato utakaowashirikisha wananchi wote bila kubagua, vyama vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanataaluma na makundi mbalimbali ya watu wa nchi yetu kote nchini, katika kutoa maoni yao juu ya wayatakayo kuhusu Katiba ya nchi yao.
Baada ya kukamilisha kukusanya maoni, Tume itatoa mapendekezo yake yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya Kikatiba kwa kufanyiwa maamuzi. Baada ya makubaliano kufikiwa, taifa letu litapata Katiba mpya kwa siku itakayoamuliwa ianze kutumika.
Ndugu Wananchi;
Ni matumaini yangu kuwa mchakato huo utaendeshwa vizuri, kwa amani na utulivu kama ilivyo sifa ya nchi yetu na mazoea yetu ya kujadiliana bila kugombana. Wananchi watapewa fursa ya kutosha ya kutoa maoni yao kwa uhuru na pawepo kuvumiliana kwa hali ya juu pale watu wanapotufautiana kwa mawazo. Pasiwepo kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana wala kushinikizana. Naomba washiriki waongozwe kwa hoja badala ya jazba. Tukiwa na jazba, hasira na kushinikizana kamwe hatutaweza kutengeneza jambo jema. Na inapohusu Katiba ya Nchi itakuwa hasara tupu. Haitakuwa endelevu na kulazimika kufanyiwa marekebisho mengi mwanzoni tu baada ya kutungwa.
Nawaomba Watanzania wenzangu wenye maoni yao wajiandae kushiriki kwa ukamilifu katika mchakato huu. Katoeni maoni yenu mazuri yatakayowezesha nchi yetu kuwa na Katiba itakayokidhi matakwa yetu ya sasa na ya miaka 50 ijayo.
Hitimisho
Ndugu Wananchi, Watanzania Wenzangu;
Napenda kumalizia salamu zangu za Mwaka mpya kwa kumshukuru tena Mwenyezi Mungu kwa rehema zake alizotujaalia mwaka 2010. Tuendelee kumuomba atujaalie baraka tele katika Mwaka ujao wa 2011: Tumuombe nchi yetu iendelee kuwa ya amani na utulivu, watu wake waendelee kuwa wamoja, wanaopenda na kushirikiana, uchumi wetu uendelee kustawi, tupate mvua za kutosha na neema ziwe tele kila mahali.
Kwa furaha na matumaini makubwa nawatakia heri na fanaka katika mwaka mpya 2011. Namtakia kila mmoja wetu mafanikio mema katika shughuli zake za kujiletea maendeleo na kuendeleza hali yake ya maisha.
Mwisho, kabisa nawaomba tuukaribishe na kuusherehekea Mwaka mpya kwa usalama na amani. Heri ya Mwaka Mpya!! Happy New Year!!
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Monday, January 3, 2011

CUF NA HARAKATI ZAO ZA KISIASA!!!

CUF – Chama cha Wananchi tumeamua kujipanga na kujizatiti upya ili kuboresha zaidi mafanikio yaliyopatikana 2010 na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote tulizozipata mwaka 2010 ili kuleta mafanikio mazuri yatakayoweza kutimiza malengo yetu ya miaka mitano (2011 – 2015).

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana;

1.Uwepo wa mshikamano ndani ya chama ambapo viongozi na wanachama awamekuwa hawahitilafiani katika masuala ya msingi

2.Utaratibu wa shughuli za chama umefanywa kwa kufuata katiba ya chama na misingi mikuu ya uendeshaji wa chama bila kugongana kitarataibu na kiutendaji.

3.Mafanikio ya uteuzi wa wagombea wa urais jamhuri ya muungano na Zanzibar ambapo tulisimamisha wagombea wanaokidhi sifa za kuongoza chi kwa mafanikio makubwa.

4.Kushiriki katika uchaguzi mkuu na kupata mafanikio;

·Wabunge 0 mwaka 2005 hadi 2 mwaka 2010 upande wa Tanganyika .

·Wabunge 19 mwaka 2005 hadi 22 mwaka 2010 upande wa Zanzibar.

·Madiwani 96 mwaka 2005 hadi 152 mwaka 2010 upande wa Tanganyika.

5.CUF kimezidi kuimarisha utaifa mwaka 2010,kwa kuwa chama cha kipekee cha kitaifa ambapo tumeafanikiwa kupata wawakilishi na wabunge kutoka katika kila upande wa muungano.

·Kwa mfano,tumepata wabunge Bara,unguja na Pemba .

·CCM wamepata wabunge bara na unguja peke yake.

·CHADEMA wamepata wabunge bara peke yake.

6.Tumefanikiwa kuendelea kupata wabunge wengi wa kuchaguliwa kuliko vyama vingine vyote vya upinzani,mwaka huu 2010 tumepata wabunge 24 waliochaguliwa kwa kura na wananchi.

7.Kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar kulikotokana na kura za maoni ya wananchi wa Zanzibar walipoamua kuwa kuanzia uchaguzi wa 2010 chama kitakachoshinda uchaguzi kwa upande wa Zanzibar kitatoa rais na kitakachokuwakuwa cha pili kitatoa makamu wa kwanza wa rais,na kwa mafanikio makubwa baada ya uchaguzi CUF ikawa ya pili Zanzibar na hivyo maamuzi ya wananchi ya kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa yakatekelezwa na sasa CUF imekuwa chama cha kwanza cha upinzani Tanzania kuingia serikalini kwa mujibu wa katiba upande wa Zanzibar.

8.Kufanikiwa kuwasilisha rasimu ya mapendekezo ya katiba mpya kwa waziri wa sheria na katiba japokuwa Polisi walitumia nguvu kubwa kuzuia CUF imeonesha ukomavu mkubwa sana kuwa wakitetea jambo la kidemokrasia la kudai haki za watu hawaogopi dola,kwa hiyo CUF inabaki kuwa chama cha kipekee katika kuwapigania watanzania.

CHANGAMOTO;
Nafasi ya urais tumerudi nyuma kutoka nafasi ya 2 mwaka 2005 hadi nafasi ya tatu mwaka 2010.

MALENGO YA CUF 2011 – 2015

1.Kushika hatamu za dola bara na Zanzibar kupitia michakato yote ya uchaguzi itakayojitokeza

2.Kuendeleza na kuimarisha umoja ndani ya chama.

3.Kutoa elimu ya uraia kupitia michakato ya kisiasa na kijamii.

4.Kuingiza wanachama wengi wapya ndani ya chama.

5.Kuendeleza madai ya katiba mpya na siyo marekebisho ya katiba hadi tupate katiba mpya itakayokuwa na maoni ya watanzania wote.

6.Kuendeleza michakato ya kuviweka pamoja vyama vya upinzani ili sote kwa pamoja kama wapinzani tuwe na dira ya pamoja na hii isaidie kutowayumbisha watanzania wanapoenda kuchagua viongozi.

Friday, December 31, 2010

HAPPY NEW YEAR TO ALL!!


Nawatakia Heri ya Mwaka Mpya wadau wote wa Blogu hii na nawashukuru kwa kile ambacho imekifanya na kuchangia Blogu hii kufika hapa!! Kumbuka tarehe Moja ya kila mwezi January Nurdin Selemani mmiliki wa Blogu huu huwa anazaliwa!!

Thursday, December 30, 2010

LIVERPOOL KIMEO, CHELSEA IKIFUFUKA, ARSENAL NGUVU YA SODA!!







Waswahili husema mwaka wa hasara ni hasara tu hata ufanyaje na ng'ombe wa maskini hazai!! Klabu ya Liverpool imeendelea kudhihirisha hili baada ya kupata kichapo cha nyumbani kutoka kwa Wolverhampton kwa goli moja kwa nunge!! Matokeo ya michezo mingine ni kama inavyoonekana:
Chelsea 1-0 Bolton
Liverpool 0-1 Wolverhampton
Wigan 2-2 Arsenal

Monday, December 27, 2010

ANCELOTTI AKALIA KUTI KAVU CHELSEA!!



Kocha Mkuu wa Chelsea Carlo Ancelotti amekalia kuti kavu baada ya timu yake kupata kichapo cha magoli 3-1 kutoka kwa Arsenal!! Licha ya dalili kuonesha kibarua chake kipo mashakani kutokana na kutoshinda michezo sita mwenyewe amesisitiza ataendelea kuwepo na sasa anataka kusajili zaidi January!!

CHELSEA KIMEO KWA ARSENAL!!





Washika Magobole wa Jiji la London Arsenal wamefanikiwa kumaliza uteja mbele ya Chelsea baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 3-1!! Magoli ya Ale Song, Cecs Fabregas na Theo Walcott ndiyo yaliyomaliza uteja wa Arsenal!!

Sunday, December 26, 2010

LIGI KUU ENGLAND YAENDELEA KUCHANJA MBUGA KWA KASI!!








Ligi Kuu nchini England maarufu kama Barclays Premium League imeendelea siku ya Boxing Day na kushuhudia Manchester United ikiendelea kujichimia kileleni mwa Ligi. Matokeo yote yalikuwa hivi:
Aston Villa 1-2 Tottenham
Blackburn 0-2 Stoke
Bolton 2-0 West Brom
Fulham 1-3 West Ham
Man Utd 2-0 Sunderland
Newcastle 1-3 Man City
Wolverhampton 1-2 Wigan

Monday, December 20, 2010

GOLIKIPA BORA KWA UPANDE WANGU!!


Anaitwa Muteba Kidiaba Golikipa wa Klabu ya TP Mazembe ambaye style yake ya ushangiliaji imemzolea umaarufu mkubwa!! Lakini pia ni golikipa anayejua wajibu wake pindi anapokuwa golini kutetea Klabu na hata Timu yake ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC!!

TP MAZEMBE NA HISTORIA KWENYE SOKA!!


Klabu ya TP Mzembe hatimaye imeweza kuandika historia na kuudhihirishia ulimwengu kuwa hata Klabu za Bara la Afrika zinaweza kusakata soka la uhakika!! TP Mazembe ambao walishindwa kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa ya Dunia mbele ya Inter Milan watakumbukwa daima kwa kile ambacho wamekifanya!! Hii inawadhihirishia wale ambao walikuwa wanahoji jinsi ambavyo walitwaa Ubingwa wa Klabu Bingwa Barani Afrika!!

NAWEKA KUMBUKUMBU SAWA!!


Kwa kweli wanazi wa kabumbu wanasubiri kwa hamu mwezi February ufike ili washuhudie kile ambacho wenyewe wanakiita fainali ya mapema kati ya Barcelona na Arsenal!! Ngoja tusubiri ili tujue mambo yatakuwaje kwa kweli!!

CUF WAMSHUKIA MZEE MWINYI SAKATA LA KATIBA MPYA!!

CUF – Chama cha Wananchi tumeshitushwa na kauli aliyoitoa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania wa awamu ya nne Mhe. Ali Hassan Mwinyi wiki iliyopita ya kutoona sababu ya kufanya mabadiliko ya Katiba kwa sasa.

Kwa mujibu wa vyombo vya Habari alidai kuwa haungi mkono wazo la kufanya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa sasa, hii ni kwa maslahi ya nani?

CUF – Chama Cha Wananchi tunasisitiza tumeshitushwa na kauli hii iliyotolewa na mtu ambaye anaheshima kubwa katika nchi hii, tunaingia shaka kwamba hakubaliani na mabadiliko hayo kufanyika sasa hivi kwa sababu hana maslahi nayo hadi hapo dhamira yake ya matumizi ya Katiba hiyo itakapokamilika hasa ukizingatia miongoni mwa wanafamilia yake wana fursa kubwa ya kuwania urais katika nchi hii.

CUF – hatuanimi kuwa mapungufu yaliyomo katika Katiba hiyo yeye hayatambui, ila inatudhihirishia wazi kuwa kuna uwezekano mkubwa yeye akiwa Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Mapinduzi kuitumia au hata kushauri vifungu vyenye utata vya katiba hiyo, kutumika kwa maslahi ya CCM.

CUF – Tunahimiza mabadiliko ya katiba ni lazima, iwapo kama tunataka demokrasia ya kweli, hatuwezi kuwa na katiba yenye Tume isiyokuwa huru ambayo Rais aliyeiteua anaweza kuivunja wakati wowote hata kwa sababu nyingine yeyote au kwa sababu ya tabia mbaya lakini wakati huo huo chombo cha kisheria kama mahakama hakina uwezo wa kuchunguza lolote lililotendwa na tume hiyo ya uchaguzi (ibara ya 74).

CUF – Tunaendelea kuwasihi, watanzania wote waumini wa dini zote, vyama vyote vya siasa, Taasisi zote nchini, asasi za kiraia, wanaharakati wa aina zote, kuungana kwa pamoja kudai mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayokidhi mahitaji ya watanzania wote.

Wednesday, December 1, 2010

MAN UTD YAANGUKIA PUA, ARSENAL IKIUA CARLING CUP!!




Manchester United imekumbana na shubiri baada ya kupata kichapo cha kwanza msimu huu cha magoli manne kwa nunge wakati Arsenal wakitinga Nusu Faila ya Carling Cup kwa kuichabanga Wigan Athletics kwa magoli mawili kwa buyu!!

KIKWETE KUHUDHURIA MKUTANO WA EAST AFRICA!!

Rais Jakaya Mrisho Kikwete anatarajia kwenda Mkoani Arusha leo mchana, kwa ajili ya kuhudhuria kikao cha kawaida cha Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kinachoanza kesho tarehe 2 Disemba.

Rais Kikwete anamaliza kipindi chake cha mwaka mmoja cha kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kumkabidhi uenyekiti kiongozi mwingine katika kikao hicho kama ilivyo katika taratibu za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Rais Kikwete alipokea uenyekiti kutoka kwa Rais Paul Kagame katika kikao cha Novemba mwaka jana , 2009.

Katika kikao cha wiki hii viongozi watapokea taarifa mbalimbali za Baraza la Mawaziri zinazohusu utekelezaji wa masuala yanayohusu Jumuiya na kujadili mambo mbalimbali.

Mapema leo asubuhi katika Ikulu ya Dar-Es-Salaam, Rais Kikwete amempokea Kijana wa Kitanzania Musa Lunyeka Dotto , mkazi wa kijiji cha Chabulongo, kata ya Kasamwa Wilaya ya Geita aliyeweka azma ya kusafiri kwa baiskeli kutoka Geita hadi Dar-Es-Salaam, kuja kumpongeza Rais Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuiongoza nchi.

Hata hivyo, Musa alipofika Singida Katibu wa Vijana wa CCM, mkoani humo alimshauri apande basi hadi Dar-es-salaam, na ndipo alipofika na leo kutimiza azma yake ya kumsalimia na kumpongeza Rais Kikwete.

Rais Kikwete amemshukuru kijana huyo kwa moyo wake huo na kuahidi kumsaidia zaidi katika shughuli zake za kilimo ili apate manufaa na mafanikio zaidi.

Tuesday, November 30, 2010

KIKWETE AKETI KIKAO CHA KWANZA NA BARAZA LA MAWAZIRI!!

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatatu, Novemba 29, 2010, amekutana rasmi kwa mara ya kwanza na Baraza la Mawaziri lake jipya pamoja na Naibu Mawaziri na kuwapa maelekezo ya awali ya nini anakitarajia kutoka kwa wateule wake hao.

Mawaziri wote 29 na Naibu Mawaziri wote 21 ambao Rais Kikwete aliwaapisha rasmi kushika nyadhifa zao katika sherehe iliyofanyika Jumamosi iliyopita, Novemba 27, 2010, wamehudhuria mkutano huo kwenye Chumba cha Baraza la Mawaziri, Ikulu, Dar es Salaam.

Katika mkutano huo uliochukua kiasi cha saa tatu, Rais alianza kwa kuwaeleza mawaziri kuwa katika kipindi hiki cha pili cha uongozi wake hakutakuwepo na muda wa kupoteza, na wala hatakuwa tayari kukubali maelezo ya kwa nini utekelezaji wa majukumu ya msingi umeshindikana.

Kwa mara nyingine amewapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri hao akisisitiza: “Mnastahili pongezi hasa ukizingatia ukweli kwamba nyinyi mmebahatika kuteuliwa kutoka kwenye orodha ndefu ya wabunge wengi wenye sifa za kushika nafasi mlizo nazo. Nimewateua kwa imani kuwa pamoja nanyi, tutatimiza matumaini ya wananchi wa Tanzania waliokichagua Chama cha Mapinduzi kiendelee kuongoza nchi yetu.”

Ameongeza: “Ni imani yangu kuwa kwa mshikamano na ushirikiano wetu kama timu moja ya ushindi, tutatekeleza majukumu yote kwa uadilifu, uaminifu na ufanisi wa hali ya juu. Ufanisi wa Waziri ama Naibu Waziri katika utekelezaji wa majukumu yake unategemea sana ufahamu na uelewa wake wa masuala muhimu yanayohusu Nchi, Serikali na Wizara anayoiongoza.”

Katika mkutano huo ambao ameuelezea kama wa Utangulizi wakati inaandaliwa Semina Elekezi, Rais Kikwete amewaelezea wateule wake maana ya Baraza la Mawaziri na majukumu yake, na kutaka kila Waziri ahakikishe anatayarisha kalenda yake ya masuala muhimu ambayo anataka yajadiliwe na Baraza la Mawaziri kwa mwaka.

Rais Kikwete pia amewaeleza wateule wake kuhusu wajibu wa Mawaziri katika Bunge akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila waziri kuhudhuria vikao vyote vya Bunge, na kuwa ndani ya Bunge mawaziri wote wa Serikali lazima wawajibike kwa pamoja.

“Ni muhimu ieleweke kuwa kama ilivyo kwa maamuzi ya Baraza la Mawaziri, uwajibikaji wa Mawaziri Bungeni ni wa Pamoja. Kwa hiyo, Hoja ya Serikali Bungeni ni Hoja ya Mawaziri Wote na siyo Waziri anayewasilisha hoja tu,” amesema Rais Kikwete.

Rais pia amewakumbusha wateule wake kuhusu uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility) katika kuongoza nchi, akisisitiza kuwa uwajibikaji huo unaelezwa kwa ufasaha katika Hati Maalum (Instrument) ya Majukumu ya kila Wizara.

Kuhusu uhusiano kati ya Waziri na Rais, na kati ya Waziri na Waziri Mkuu, Rais amesema kuwa pamoja na kwamba shughuli zote za utendaji Serikalini hutekelezwa kwa niaba ya Rais, lazima mawaziri wakumbuke kuwa Waziri Mkuu ndiye msimamizi wa shughuli za kila siku za Serikali.

Rais Kikwete pia ametaka kujengeka mahusiano mazuri kati ya Waziri na Naibu Waziri wake akisisitiza: “Jambo la msingi la kuzingatia ni kwamba uhusiano mzuri baina ya viongozi hawa ni nguzo muhimu katika mafanikio ya Wizara. Kwa hiyo, ili kuepuka migongano katika utekelezaji ni muhimu mipaka ya kazi za Waziri na Naibu Waziri ikaheshimika na pia ni wajibu wa Waziri kumpangia kazi Naibu Waziri katika Wizara husika.

Katika mkutano huo, Rais Kikwete pia amezungumzia uhusiano kati ya Waziri na Katibu Mkuu; uhusiano kati ya Waziri wa Nchi Asiyekuwa na Portfolio na Katibu Mkuu; uhusiano kati ya Naibu Waziri na Katibu Mkuu, na uhusiano kati ya Waziri na Waziri wa Sekta Nyingine.

Rais Kikwete pia amefafanua kuhusu uhusiano kati ya Wizara na Wadau Wengine; uhusiano baina ya Wizara, Mikoa na Halmashauri; uhusiano na Taasisi Zilizo Chini ya Wizara; uhusiano na Wasaidizi wa Mawaziri pamoja na utekelezaji wa Maagizo ya Viongozi wa Kitaifa.
Rais Kikwete pia amewaeleza Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhusu nyaraka muhimu ambazo wanapaswa kukabidhiwa na kuzipitia watakapofika kwenye nafasi zao mpya za kazi. Nyaraka hizo ni pamoja na Taarifa ya Makabidhiano ya Ofisi, Katiba, Ilani ya Chama Tawala, Dira ya Taifa, na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA).

Aidha, Rais Kikwete amewaeleza wateule wake kuhusu umuhimu wao kufahamu Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu, Mikakati, Mipangomkakati, Mpango na Bajeti ya Wizara, Mpango wa Kazi wa Wizara na Masharti ya Kazi ya Waziri.

Rais Kikwete vile vile amekumbusha Mawaziri na Naibu Mawaziri wake kuwa suala la vita dhidi ya rushwa ni suala la kikatiba na kuwataka kuhakikisha kuwa Mpango wa Pili wa Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Rushwa (NACSAP-11) unatekelezwa.

Pia amewataka Mawaziri kusimamia mapato ya Serikali yasiyotokana na kodi na kudhibiti matumizi ya Serikali.
Rais Kikwete pia amewataka viongozi hao kuzingatia maadili ya uongozi ikiwa ni pamoja na kusimamia sheria za nchi, kuheshimu sheria katika shughuli na mambo yao binafsi na pia kutunza siri za Serikali kwa mujibu wa kiapo chao.

Rais Kikwete pia amesisitiza umuhimu wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuwasiliana na wananchi kwa maana ya kueleza mafanikio ya Serikali na mipango ya Serikali katika kushughulikia matatizo ya wananchi.

Amewataka kuvitumia kikamilifu Vitengo vya Mawasiliano ya Serikali katika wizara zao ambavyo ndivyo vyenye jukumu la kutoa taarifa kuhusu Wizara inavyotelekeza majukumu yake.

“Uzoefu unaonyesha kuwa Mawaziri wengi ni wazito kufanya mawasiliano na wananchi hata pale ambako Wizara imefanya mambo mengi mazuri. Hivyo, Mawaziri muwe mstari wa mbele kuelezea mafanikio ya utendaji wa Serikali katika Wizara zetu,” ameelekeza Rais Kikwete na kuongeza:

“Lazima ujengwe utamaduni wa kudumu wa kuwasiliana na wananchi wote ambao ndio waajiri wetu kupitia kura zao. Mawaziri wote tumieni Vitengo vyenu vya Mawasiliano na vyombo vya habari kwa ustadi ipasavyo,” amefafanua Rais Kikwete.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

BARCELONA YAISHUSHIA MAAFA REAL MADRID!!







Barcelona hatimaye wamekaa kileleni mwa Ligi Kuu nchini Spain maarufu kama La Liga baada ya kuvuna ushindi wa magoli matano kwa nunge dhidi ya wapinzani wao Real Madrid!!

Monday, October 11, 2010

MATOKEO YA SYNOVATE YASHUKIWA!!!

CUF – Chama cha Wananchi tumesikitishwa na taarifa ya utafiti wa taasisi ya Synovate iliyotolewa jana Oktoba 10, jijini Dar es Salaam na kuripotiwa na vyombo vya habari leo hii namna inavyojichanganya, kwani idadi ya wanaomkubali Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi Jakaya Kikwete ni wengi kuliko vyama vingine, wakati huo huo wanaokiri kutoridhishwa na huduma zake ni wengi.

Kwa mujibu wa vyombo vya Habari, ripoti hiyo inaonyesha Dkt. Jakaya Kikwete anakubalika kwa asilimia 61, Dkt. Willbrod Slaa ana asilimia 16 na Prof. Ibrahim Lipumba ana asilimia 5, lakini wakati huo huo inaeleza ripoti hiyo kuwa katika utendaji wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete watu wengi waliohojiwa hawakuridhika na huduma zinazotolewa katika upatikanaji wa ajira (84%), bei za vyakula (72%), maji safi ya kunywa (49%), afya(48%), mapambano dhidi ya rushwa(61%) na mapambano dhidi ya kuondoa umasikini(86%).

Katika ripoti hiyo hiyo, pamoja na kuonyesha wananchi wasivyoridhishwa na utendaji wa serikali hiyo ya Jakaya Kikwete, lakini bado wana imani na Rais Kikwete kwa asilimia 84, Baraza la Mawaziri (68%), Jeshi la Polisi (45%), Baraza la Mitihani (50%), mahakama (52), taasisi za huduma za afya (50%), TAKUKURU (46%) na vyama vya upinzani (48%).

Kwa upande wa elimu ya msingi ripoti inaonyesha kuwa wanaoridhika na utolewaji bora wa elimu ni asilimia 82, na kwa elimu ya sekondari wanaoridhika na utolewaji wa elimu bora ni asilimia 77.

CUF – Chama cha Wananchi tunasema iwapo kama ni kweli taarifa iliyoripotiwa ndivyo ilivyo tunasikitishwa namna taaluma ya utafiti inavyotumika vibaya, kwani hayamkiniki mtu mwenye akili timamu hata kama hakwenda shule, hata awe mtoto wako nyumbani, wakati akijua fika, tena kwa uhakika kwamba wewe umeshindwa kumpatia huduma muhimu (kama ripoti inavyoonyesha) na akawa bado eti ana imani na wewe na watendaji wako, huu ni uzushi mtupu.

CUF – Chama cha Wananchi tunaitaka taasisi ya Syonovate iwaombe radhi watanzania, kwani ripoti yao inaonyesha kuwa, wananchi wa nchi hii bado ni mbumbumbu wa kumpenda mtu kwa sura yake na wakaendelea kuwa na imani nae hata kama wanatambua fika ameshindwa kuwapatia huduma muhimu, huku ni kuwadhalilisha Watanzania na kazi kubwa inayofanywa na vyama vya upinzani, taasisi zisizo za kiserikali na vyombo vya habari juu ya kuelimisha umma.

CUF – Tunawatahadharisha Watanzania kuwa makini katika kipindi hiki cha uchaguzi, kwani taasisi mamluki zitatumia taaluma zao kuwapotosha na kuwavunja moyo mliokuwa nao wakukataa ufisadi na dhuluma inayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi dhidi ya mali asili na mapato ya nchi, ili siku ya uchaguzi Oktoba 31, wananchi msijitokeze kwa wingi kwa kudhani kuwa CCM bado inakubalika, TUNAWASIHI WANANCHI WA TANZANIA WALIOJIANDIKISHA KUPIGA KURA, JITOKEZENI KWA WINGI SIKU YA KUPIGA KURA NA MFANYE MAAMUZI SAHIHI YA KULETA MABADILIKO.