Wednesday, December 1, 2010

KIKWETE KUHUDHURIA MKUTANO WA EAST AFRICA!!

Rais Jakaya Mrisho Kikwete anatarajia kwenda Mkoani Arusha leo mchana, kwa ajili ya kuhudhuria kikao cha kawaida cha Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kinachoanza kesho tarehe 2 Disemba.

Rais Kikwete anamaliza kipindi chake cha mwaka mmoja cha kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kumkabidhi uenyekiti kiongozi mwingine katika kikao hicho kama ilivyo katika taratibu za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Rais Kikwete alipokea uenyekiti kutoka kwa Rais Paul Kagame katika kikao cha Novemba mwaka jana , 2009.

Katika kikao cha wiki hii viongozi watapokea taarifa mbalimbali za Baraza la Mawaziri zinazohusu utekelezaji wa masuala yanayohusu Jumuiya na kujadili mambo mbalimbali.

Mapema leo asubuhi katika Ikulu ya Dar-Es-Salaam, Rais Kikwete amempokea Kijana wa Kitanzania Musa Lunyeka Dotto , mkazi wa kijiji cha Chabulongo, kata ya Kasamwa Wilaya ya Geita aliyeweka azma ya kusafiri kwa baiskeli kutoka Geita hadi Dar-Es-Salaam, kuja kumpongeza Rais Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuiongoza nchi.

Hata hivyo, Musa alipofika Singida Katibu wa Vijana wa CCM, mkoani humo alimshauri apande basi hadi Dar-es-salaam, na ndipo alipofika na leo kutimiza azma yake ya kumsalimia na kumpongeza Rais Kikwete.

Rais Kikwete amemshukuru kijana huyo kwa moyo wake huo na kuahidi kumsaidia zaidi katika shughuli zake za kilimo ili apate manufaa na mafanikio zaidi.

No comments:

Post a Comment