Thursday, March 18, 2010

TUCTA WAZIDI KUBANWA!!!!

TAMKO LA SERIKALI JUU YA MGOMO WA TUCTA

Haki iliyotajwa hapo juu imeelezwa bayana katika sura ya saba ya sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004. Kanuni ya utendaji bora na taratibu za kufuatwa katika kutekeleza haki hiyo, imeelekezwa katika sehemu ya nne ya kanuni za utendaji bora toleo la Serikali namba 42 la tarehe 16/02/2007.

Katika sheria iliyotajwa hapo juu kila mfanyakazi anahaki ya kushiriki katika mgomo iwapo kuna mgogoro wa kimaslahi, na kila mwajiri ana haki ya kufungia nje wafanyakazi mahala pa kazi iwapo pana mgogoro wa kimaslahi.

Hata hivyo haki hii imejengewa utaratibu wa kuitekeleza ili kulinda uhai na usalama wa mali, ikiwa ni pamoja na haki za watu wengine ambao pia wana maslahi katika mahusiano hayo. Moja ya mambo yaliyozuiliwa ni kuitisha mgomo unaotokana na malalamiko au haki/ kutotendewa haki.

Kwa kifupi ninachosema ni kwamba mfanyakazi anayohaki ya kugoma kama vile mwajiri alivyo na haki ya kufungia nje mfanyakazi, lakini kwa makundi haya yote mawili ni lazima yazingatie kuwa ipo sheria na zipo kanuni zinazosimamia masuala haya.

Ni muhimu vilevile kufahamu kuwa katika suala la majadiliano baina ya Mwajiri na mfanyakazi wote wanakuwa na haki sawa, hakuna anayeweza kumwamrisha mwenzake, kwa hiyo ni mahala ambapo kila mmoja wao anapaswa kuacha jazba na kuwa na subira. Silaha kubwa ya pande zote mbili ni majadiliano.

KUHUSU TAMKO LA TUCTA LA KUTANGAZA MGOMO TAREHE 5/5/2010
Sisi kama Serikali ni dhahiri tamko hili au kauli hii imetushangaza na pia kiasi Fulani kutusikitisha kwani tunaamini kuwa hali ya mazungumzo ilivyokuwa inaendelea hakukuwa na haja ya kufikia hapo. Kila hoja waliyoieleza Serikali inaifanyia kazi kwa kushirikiana na wao, na wanalijua hilo.

Lakini pamoja na hayo, walipomwandikia barua Kamishna wa Kazi, yenye Ref. TUCTA/AP.15/3/9/2 ya 8/9/2010 kumwarifu juu ya nia yao ya kugoma, sie tulichukua hatua ya kuwajibu na kuwaita Wizarani, ili waje tuzungumze/tujadiliane barua Ref. CAB.360/223/01 ya 11/3/2010 cha kushangaza walikataa na kusema kuwa hawawezi kushiriki katika mazungumzo yoyote kwa sababu wao ni Kamati tu ya Utendaji wakati ambapo azimio la kugoma lilitolewa na Baraza Kuu la TUCTA Ref. TUCTA/P.15/17/5/37 ya 15/3/2010. Kwa bahati nzuri, wakati wanaliandikia barua hiyo ya kukataa kuja tarehe hiyo hiyo waliandika barua LESCO ya kutangaza nia yao ya kugoma ifikapo tarehe 5/5/2010 Ref. TUCTA/M.10/1/2/100 ya 15/3/2010 sababu walizotoa ni kama zifuatazo:-

1. Kutotekeleza mapendekezo ya Tume ya Mishahara ya NTUKAMAZINA ambayo iliteuliwa na Mheshimiwa Rais kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

2. Kutoliangalia swala zima la ukusanyaji wa kodi, hivyo kuwafanya wafanyakazi kuwa eneo kubwa pekee la kulipa kodi za juu wakati wafanyakabiashara wakilipa kodi ndogo na wakati mwingine kukwepa.

3. Wizara ya Kazi kutotangaza maamuzi yake kuhusu mapendekezo ya utafiti uhusuo Vima vya Chini katika sekta binafsi, kinyume na Sheria inavyoagiza.

4. Wizara ya Kazi kushindwa kuunda Bodi mpya za mishahara za Sekta Binafsi tangu zile za zamani zilipomaliza muda wake 1 Aprili 2009.

5. Wizara ya Kazi kushindwa kuitisha vikao vya LESCO ambacho ni chombo cha kuishauri Serikali kuhusu masuala ya wafanyakazi tangu chombo hicho kizinduliwe mwezi Agost 2009 licha ya Rais kuagiza likutane katika kikao chetu cha 4/5/2009 Ikulu Dar es Salaam.

6. Ofisi ya Waziri anayehusika na Menejiment ya Utumishi wa Umma kushindwa kuitisha vikao vya majadiliano yanayohusu maslahi ya Watumishi wa Umma kama sheria ya majadiliano (The Public Service Negotiating Machinery) Act 2003 inavyoagiza.

7. Serikali kutokuwa makini katika kurekebisha malipo dhaifu yatokanayo na Mifuko ya Pensheni ya Wastaafu hivyo kuwafanya Wastaafu wengi kupata mafao duni ya uzeeni.

Kwa kuwa sasa wamefuata mkondo wa sheria unaotakikana kwa kuiandikia LESCO, naamini sasa sheria itachukua mkondo wake katika kutukutanisha pande zote mbili. Sheria inaitaka LESCO kufanya hivyo ndani ya siku 30.

Nina imani hili litafanyika na nina imani pia kuwa ufumbuzi utapatikana kabla ya hiyo tarehe 5/5/2010.

Imesainiwa
Alhaj. Prof. Juma . A. Japuya (Mb)
WAZIRI WA KAZI, AJIRA NA MAENDELEO YA VIJANA

No comments:

Post a Comment