Friday, March 12, 2010

BARABARA YA SONGEA-NAMTUMBO KUJENGWA!!

Waziri wa Miundombinu Daktari Shukuru Jumanne Kawambwa amewaahidi wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuwa Ujenzi wa barabara za SONGEA – NAMTUMBO na PERAMIHO – MBINGA zenye jumla ya kilometa 140 kwa kiwango cha lami utaanza kabla ya Mwezi Juni Mwaka huu.

Daktari Kawambwa aliyekuwa katika ziara ya siku tatu Mkoani RUVUMA kwa lengo la kukagua miundombinu ya barabara, Gati ya Bandari ya Mbambabay na Kivuko cha Mto RUHUHU amesema hivi sasa Serikali inakamilisha taratibu za mwisho za kuwapata wakandalasi ambao wataanza kazi mwezi Mei.

Akiwa katika ziara hiyo Wananchi katika maeneo tofautitofauti wameonesha kuwa na mashaka na kauli hiyo ya Ukweli wa Kuanza kwa ujenzi wa Lami, na mara zote ilimlazimu Daktari Kawambwa kuwaondoa shaka kuwa Jambo hilo sio Propaganda na wala halina uhusiano na Uchaguzi Mkuu Ujao.

Hata hivyo akiwa njiani Waziri wa Miundombinu amekutana na Changamoto ya gari lake aina Toyota Landcruiser VX V8 kukwama barabarani kutokana na Mvua nyingi na Ubovu Mkubwa wa barabara za SONGEA – MBAMBABAY na SONGEA – TUNDURU ambazo zinasababisha magari mengi kukwama.

Kabla ya kuondoka Mkoani RUVUMA Daktari Kawambwa pia ametembelea kiwanja cha Ndege cha SONGEA ambapo ameelezwa kuwa hakuna safari za ndege za abiria zinazofanyika kupitia kiwanja hicho kutokana na kukosa mafuta ya ndege na Maji, na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa RUVUMA kuendelea kufuatilia uwepo wa mafuta ya ndege na kuhakikisha watu waliovamia kiwanja hicho wanaondolewa. (Habari kwa Hisani ya Gerson Msigwa)

No comments:

Post a Comment